Hamia kwenye habari

Simulizi la Noa na Gharika Kuu​—Je, Ni Hekaya Tu?

Jibu la Biblia

 Gharika ilitukia kihalisi. Mungu aliileta ili kuwaharibu watu waovu, lakini alimwagiza Noa ajenge safina ili kuwahifadhi watu wazuri na wanyama. (Mwanzo 6:11-20) Tunaweza kuamini kwamba Gharika ni tukio halisi kwa sababu imerekodiwa katika Biblia, ambayo “[imeongozwa] na roho ya Mungu.”—2 Timotheo 3:16.

 Simulizi la kweli au hekaya?

 Biblia inaonyesha kwamba Noa alikuwa mtu halisi na Gharika lilikuwa tukio halisi, si hekaya.

  •   Waandikaji wa Biblia waliamini kwamba Noa alikuwa mtu halisi. Kwa mfano, waandikaji wa Biblia Ezra na Luka walikuwa wanahistoria makini sana. Katika orodha yao ya majina ya vizazi vya taifa la Israeli, jina la Noa lipo. (1 Mambo ya Nyakati 1:4; Luka 3:36) Waandikaji wa Injili Mathayo na Luka walirekodi maneno ya Yesu kuhusu Noa na Gharika.—Mathayo 24:37-39; Luka 17:26, 27.

     Pia, nabii Ezekieli na mtume Paulo walimtaja Noa kuwa mfano wa imani na uadilifu. (Ezekieli 14:14, 20; Waebrania 11:7) Je, inapatana na akili kwa waandikaji hao kutaja mtu wa kubuniwa kuwa mfano wa kuigwa? Ni wazi kwamba Noa pamoja na wanaume na wanawake wengine wa imani ni mifano mizuri ya kuigwa kwa sababu walikuwa watu halisi.—Waebrania 12:1; Yakobo 5:17.

  •   Biblia inatoa habari hususa kuhusu Gharika. Simulizi la Biblia kuhusu Gharika halianzi kama hekaya zinazoanza kwa maneno, “Hapo zamani za kale.” Badala yake, Biblia inataja mwaka, mwezi, na siku inayohusiana na matukio ya Gharika. (Mwanzo 7:11; 8:4, 13, 14) Pia, inataja vipimo vya safina ambayo Noa alijenga. (Mwanzo 6:15) Habari hizo hususa zinaonyesha kwamba Biblia inaitaja Gharika kuwa simulizi lenye mambo hakika, bali si hekaya.

 Kwa nini Gharika ilitokea?

 Kulingana na Biblia, kabla ya Gharika “uovu wa mwanadamu ulikuwa mkubwa.” (Mwanzo 6:5) Ilisema pia kwamba “dunia ilikuwa imeharibika machoni pa Mungu wa kweli” kwa sababu ilikuwa imejaa ukatili na maadili mapotovu.—Mwanzo 6:11; Yuda 6, 7.

 Biblia inasema kwamba mengi kati ya matatizo hayo yalisababishwa na malaika waovu waliotoka mbinguni ili kufanya ngono na wanawake. Malaika hao walikuwa na watoto walioitwa Wanefili, ambao waliwatendea wanadamu kikatili. (Mwanzo 6:1, 2, 4) Mungu aliamua kuondoa uovu duniani na kuwaruhusu watu wazuri waanze upya.—Mwanzo 6:6, 7, 17.

 Je, watu walijua kwamba kungekuwa na Gharika?

 Ndiyo. Mungu alimwambia Noa mambo ambayo yangetukia na akamwagiza ajenge safina ili kuiokoa familia yake na pia wanyama. (Mwanzo 6:13, 14; 7:1-4) Noa aliwaonya watu kuhusu uharibifu uliokuwa ukija, lakini walipuuza maonyo yake. (2 Petro 2:5) Biblia inasema: “Hawakujali mpaka Gharika ikaja na kuwafagilia mbali wote.”—Mathayo 24:37-39.

 Safina ya Noa ilionekanaje?

 Safina ilikuwa sanduku kubwa lenye umbo la mstatili lenye urefu wa mita 133, upana wa mita 22, na kimo cha mita 13. * Ilijengwa kutokana na mbao za mti wenye utomvu, na ikafunikwa kwa lami ndani na nje. Ilikuwa na ghorofa tatu na ilikuwa na vyumba kadhaa. Kulikuwa na mlango ubavuni mwake na inaelekea kulikuwa na dirisha upande wa juu. Inaelekea pia ilikuwa na paa lililoinuka katikati kwa kadiri fulani ili kuruhusu maji yatiririke.—Mwanzo 6:14-16.

 Ilimchukua Noa muda gani kujenga safina?

 Biblia haisemi ilimchukua Noa muda gani kujenga safina, lakini inaonekana kwamba alitumia makumi ya miaka kufanya hivyo. Noa alikuwa na umri wa miaka 500 hivi alipomzaa mwana wake wa kwanza, naye Noa alikuwa na umri wa miaka 600 Gharika ilipoanza. *Mwanzo 5:32; 7:6.

 Mungu alimwambia Noa ajenge safina baada ya wana wake watatu kuwa wameshakua na kuoa, na huenda hilo lingechukua miaka 50 au 60. (Mwanzo 6:14, 18) Kwa kutegemea uwezekano huo, inapatana na akili kusema kwamba huenda ujenzi wa safina ulikamilishwa baada ya miaka 40 au 50.

^ Biblia inataja vipimo vya safina kwa kutumia mikono. “Kipimo cha kawaida cha mkono katika Kiebrania kilikuwa sentimita 44.45.”—The Illustrated Bible Dictionary, Toleo Lililorekebishwa, Sehemu ya 3, ukurasa wa 1635.

^ Kuhusu muda ambao watu kama Noa waliishi, ona makala yenye kichwa “Je, Kweli Watu wa Nyakati za Biblia Waliishi kwa Muda Mrefu Sana?” katika Mnara wa Mlinzi la Desemba 1, 2010.