MATHAYO 27:57–28:2 MARKO 15:42–16:4 LUKA 23:50–24:3 YOHANA 19:31–20:1

  • MWILI WA YESU WASHUSHWA KUTOKA KWENYE MTI

  • MWILI WATAYARISHWA KWA AJILI YA KUZIKWA

  • WANAWAKE WAPATA KABURI LIKIWA TUPU

Siku inakaribia kwisha Ijumaa alasiri, Nisani 14. Siku ya Sabato, Nisani 15 itaanza jua litakapotua. Tayari Yesu amekufa lakini wezi wawili walio kando yake bado wako hai. Kulingana na Sheria, maiti hazipaswi kubaki “mtini usiku kucha,” badala yake, zinapaswa kuzikwa “siku hiyohiyo.”—Kumbukumbu la Torati 21:22, 23.

Isitoshe, kipindi cha Ijumaa mchana kinaitwa Matayarisho kwa sababu watu huandaa vyakula na kumalizia kazi ambazo zinapaswa kufanywa kabla ya Sabato. Jua litakapotua, Sabato “kuu” itaanza. (Yohana 19:31) Hii ni kwa sababu Nisani 15 itakuwa siku ya kwanza ya siku saba za Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu, na kwa kawaida siku hiyo huwa ni Sabato. (Mambo ya Walawi 23:5, 6) Pindi hii, siku hiyo ya kwanza itakuwa siku moja na siku ya Sabato, siku ya saba ya juma.

Basi Wayahudi wanamwomba Pilato aharakishe kifo cha Yesu na wezi wawili walio kando yake. Jinsi gani? Kwa kuagiza miguu yao ivunjwe. Hilo litawazuia wasitumie miguu yao kuinua miili yao ili kupumua. Wanajeshi wanakuja na kuvunja miguu ya wale wezi wawili. Lakini wanaona kwamba Yesu amekufa, basi hawaivunji miguu yake. Hilo linatimiza andiko la Zaburi 34:20: “Anailinda mifupa yake yote; haujavunjwa hata mmoja.”

Ili kuhakikisha kabisa kwamba Yesu amekufa, mwanajeshi mmoja anamchoma Yesu ubavuni kwa mkuki, na kutoboa sehemu iliyo karibu na moyo wake. ‘Mara moja damu na maji vinatoka.’  (Yohana 19:34) Hilo linatimiza andiko lingine: “Watamtazama yule waliyemchoma.”—Zekaria 12:10.

Pia, Yosefu kutoka jiji la Arimathea, ambaye ni “tajiri” na mshiriki anayeheshimiwa wa Sanhedrini, yuko hapo Yesu anapouawa. (Mathayo 27:57) Anafafanuliwa kuwa “mtu mwema na mwadilifu,” ambaye “alikuwa akiungojea Ufalme wa Mungu.” Kwa kweli, akiwa “mwanafunzi wa Yesu lakini kwa siri kwa sababu aliwaogopa Wayahudi,” hakuunga mkono uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo katika kesi ya Yesu. (Luka 23:50; Marko 15:43; Yohana 19:38) Kwa ujasiri, Yosefu anamwomba Pilato amruhusu auchukue mwili wa Yesu. Pilato anamwita mwanajeshi anayesimamia, ili ahakikishe kwamba Yesu amekufa. Kisha Pilato anampa Yosefu ruhusa.

Yosefu ananunua kitani bora na safi, kisha anaushusha mwili wa Yesu kutoka kwenye mti. Anaufunga mwili huo kwa kitani ili kuutayarisha kwa ajili ya mazishi. Nikodemo “aliyemjia [Yesu] usiku mara ya kwanza,” anasaidia kufanya matayarisho hayo. (Yohana 19:39) Analeta karibu pauni 100 za Kiroma (kilogramu 33) za mchanganyiko wa bei ghali wa manemane na udi. Mwili wa Yesu unafungwa kwa vitambaa vilivyo na manukato hayo, kulingana na desturi za mazishi ya Wayahudi.

Yosefu anamiliki kaburi lililo tupu ambalo limechimbwa katika mwamba ulio hapo karibu, nao wanaulaza mwili wa Yesu humo. Kisha jiwe kubwa linaviringishwa mbele ya kaburi hilo. Wanafanya hivyo haraka haraka, kabla Sabato haijaanza. Huenda Maria Magdalene na Maria mama ya Yakobo Mdogo wamekuwa wakisaidia kuutayarisha mwili wa Yesu. Sasa wanaharakisha kurudi nyumbani ili “kutayarisha manukato na mafuta yenye marashi” ambayo wataupaka mwili wa Yesu baada ya Sabato.—Luka 23:56.

Siku inayofuata, ambayo ni siku ya Sabato, wakuu wa makuhani na Mafarisayo wanaenda kwa Pilato na kusema: “Tumekumbuka mjanja huyo alipokuwa hai alisema, ‘Nitafufuliwa baada ya siku tatu.’ Kwa hiyo, amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu, ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu, ‘Alifufuliwa kutoka kwa wafu!’ Kisha udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa kwanza.” Pilato anawaambia: “Mnaweza kuweka walinzi. Nendeni mkalilinde jinsi mnavyotaka.”—Mathayo 27:63-65.

Asubuhi na mapema siku ya Jumapili, Maria Magdalene, Maria mama ya Yakobo, na wanawake wengine wanaleta manukato kwenye kaburi ili waupake mwili wa Yesu. Wanaulizana: “Ni nani atakayetuviringishia lile jiwe kutoka kwenye mwingilio wa kaburi?” (Marko 16:3) Lakini tetemeko la ardhi limetokea. Isitoshe malaika wa Mungu ameliviringisha lile jiwe na kuliondoa, walinzi hawapo, na kaburi liko tupu!