MATHAYO 21:19-27 MARKO 11:19-33 LUKA 20:1-8

  • MTINI ULIONYAUKA​—SOMO KUHUSU IMANI

  • WAULIZA KUHUSU MAMLAKA YA YESU

Yesu anaondoka Yerusalemu Jumatatu alasiri na kurudi Bethania, upande wa mashariki wa mteremko wa Mlima wa Mizeituni. Inawezekana kwamba usiku huo anakaa nyumbani kwa rafiki zake, yaani, Lazaro, Maria, na Martha.

Sasa ni asubuhi ya Nisani 11. Yesu na wanafunzi wake wako njiani tena, wakirudi Yerusalemu ambako atakuwa hekaluni kwa mara ya mwisho. Na ni siku yake ya mwisho ya huduma ya hadharani kabla ya kusherehekea Pasaka, kuanzisha Ukumbusho wa kifo chake, kisha akabili kesi na kuuawa.

Wakiwa njiani kutoka Bethania kwenye Mlima wa Mizeituni kuelekea Yerusalemu, Petro anauona mtini ambao Yesu aliulaani asubuhi ya siku iliyotangulia. Anasema hivi akiwa amesisimka: “Rabi, ona! ule mtini ulioulaani umenyauka.”—Marko 11:21.

Lakini kwa nini Yesu aliufanya mtini huo unyauke? Anaonyesha sababu anapojibu hivi: “Kwa kweli ninawaambia, mkiwa na imani nanyi msiwe na shaka, hamtafanya tu nilichoufanyia mtini huo, bali hata mkiuambia mlima huu, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ jambo hilo litatendeka. Na mambo yote mnayoomba katika sala, mkiwa na imani, mtapokea.” (Mathayo 21:21, 22) Basi anarudia jambo alilosema hapo awali kwamba imani inaweza kuhamisha mlima.—Mathayo 17:20.

Kwa hiyo, kwa kuufanya mti huo unyauke, Yesu anafundisha somo muhimu kuhusu uhitaji wa kuwa na imani katika Mungu. Anasema: “Mambo yote mnayosali na kuomba, iweni na imani kwamba mmeyapokea, nanyi mtayapata.” (Marko 11:24) Hilo ni somo muhimu sana kwa wafuasi wote wa Yesu! Somo hilo hasa linawafaa mitume kwa sababu ya majaribu makali ambayo watakabili hivi karibuni. Pia kuna uhusiano mwingine kati ya ule mtini ulionyauka na ubora wa imani.

Kama mtini huo, taifa la Israeli liko kinyume na jinsi linavyoonekana. Watu wa taifa hilo wako katika agano pamoja na Mungu, na kwa nje huenda wanaonekana kwamba wanafuata Sheria. Hata hivyo, kwa ujumla taifa zima limethibitisha kwamba halina imani na halizai matunda mazuri. Hata wanamkataa Mwana wa Mungu! Hivyo, kwa kuufanya mtini usiozaa unyauke, Yesu anaonyesha matokeo yatakayolipata taifa hilo lisilozaa matunda, na lisilo na imani.

Muda mfupi baadaye, Yesu na wanafunzi wake wanaingia Yerusalemu. Kama ilivyo desturi yake, Yesu anaingia hekaluni na kuanza kufundisha. Wakuu wa makuhani na wazee wa watu, labda wakikumbuka jambo ambalo Yesu aliwafanyia watu waliokuwa wakibadili pesa siku iliyotangulia, wanamuuliza: “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Au ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?”—Marko 11:28.

Yesu anawajibu: “Nitawauliza swali moja. Mkinijibu, nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Nijibuni.” Sasa wapinzani wake ndio wanaopaswa kujibu. Makuhani na wazee wanashauriana jinsi watakavyojibu: “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, kwa nini hamkumwamini?’ Lakini je, tutathubutu kusema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’?” Wanafikiria kwa njia hiyo kwa sababu wanauogopa umati, “kwa maana umati wote uliamini kwa kweli Yohana alikuwa nabii.”—Marko 11:29-32.

Wale wanaompinga Yesu wanashindwa kutoa jibu linalofaa. Basi wanasema: “Hatujui.” Naye Yesu anawaambia: “Nami siwaambii ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”—Marko 11:33.