Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Yesu​—Njia, Kweli, na Uzima

 SURA YA 45

Ana Nguvu Kuliko Kikosi cha Roho Waovu

Ana Nguvu Kuliko Kikosi cha Roho Waovu

MATHAYO 8:28-34 MARKO 5:1-20 LUKA 8:26-39

  • AWAFUKUZA ROHO WAOVU, WAINGIA KWENYE NGURUWE

Wanafunzi wanaporudi tena ufuoni baada ya lile tukio lenye kutisha, wanashuhudia jambo linalowashtua sana. Wanaume wawili wakali sana walio na roho waovu, wanatoka kwenye makaburi yaliyo hapo karibu na na kumkimbilia Yesu! Mmoja wao anatajwa sana, labda kwa sababu ndiye mkatili zaidi na amekuwa na roho waovu kwa muda mrefu zaidi.

Mwanaume huyo aliye na hali yenye kuhuzunisha amekuwa akitembea uchi. Usiku na mchana anapaza sauti “makaburini na milimani na kujikatakata kwa mawe.” (Marko 5:5) Ni mkali sana hivi kwamba watu wanaogopa kupita kwenye barabara hiyo. Baadhi yao wamejaribu kumfunga, lakini anakata minyororo na kuvunja pingu alizofungwa miguuni. Hakuna mtu aliye na nguvu za kumdhibiti.

Mtu huyo anapomkaribia Yesu na kuanguka miguuni pake, roho waovu wanaomwongoza wanamfanya apaze sauti: “Kwa nini unanisumbua, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Zaidi? Ninakuapisha kwa Mungu usinitese.” Yesu anaonyesha kwamba ana mamlaka juu ya roho waovu, anamwamuru: “Mtoke mtu huyu, wewe roho mwovu.”—Marko 5:7, 8.

Ukweli ni kwamba, mwanaume huyo ana roho wengi waovu. Yesu anapouliza, “Unaitwa nani?” anajibu: “Jina langu ni Kikosi, kwa sababu tuko wengi.” (Marko 5:9) Kikosi cha Roma kina maelfu ya wanajeshi; basi, mtu huyo anasumbuliwa na roho wengi waovu wanaofurahia kumwona akiteseka. Wanamsihi Yesu “asiwaamuru waende katika shimo refu lisilo na mwisho.” Huenda wanatambua jambo linalowasubiri, wao pamoja na kiongozi wao, Shetani.—Luka 8:31.

Hapo karibu kuna kundi la nguruwe kama 2,000 hivi wanaolisha, wanyama hao si safi kulingana na Sheria na Wayahudi hata hawapaswi kuwafuga. Roho waovu wanamsihi: “Turuhusu tuingie ndani ya wale nguruwe.” (Marko 5:12) Yesu anawaambia waende, nao wanaingia ndani ya nguruwe hao. Kisha nguruwe wote 2,000 wanaruka poromoko na kuzama baharini.

 Watu waliokuwa wakiwachunga nguruwe wanapoona hivyo, wanakimbia kwenda kupeleka habari jijini na mashambani. Watu wanakuja kuona kile kilichotokea. Wanapofika, wanaona kwamba sasa yule mtu aliyetokwa na roho waovu amepona na ana akili timamu. Hata amevaa nguo na amekaa miguuni pa Yesu!

Watu wanaomwona au kusikia kumhusu mtu huyo wanashikwa na woga, nao hawaelewi ni mambo gani mengine yatakayotokea. Wanamsihi Yesu aondoke katika eneo lao. Yesu anapopanda mashua ili kuondoka, yule mtu aliyekuwa na roho waovu anamsihi aende pamoja naye. Lakini Yesu anamwambia: “Nenda nyumbani kwa watu wako wa ukoo, ukawaambie mambo yote ambayo Yehova amekufanyia na jinsi alivyokuonyesha rehema.”—Marko 5:19.

Kwa kawaida Yesu anawaambia watu anaowaponya wasimwambie mtu yeyote kwa sababu hataki watu wamwamini kupitia habari za kusisimua. Katika kisa hiki, mtu huyo aliyekuwa na roho waovu ni uthibitisho ulio wazi wa nguvu za Yesu naye anaweza kuwatolea ushahidi watu ambao hawawezi kumwona Yesu uso kwa uso. Ushahidi wake unaweza pia kupunguza habari mbaya kuhusu wale nguruwe waliokufa. Basi mtu huyo anaenda na kuanza kutangaza kotekote katika Dekapoli jinsi Yesu alivyomtendea.