YOHANA 6:48-71

  • KULA MWILI WAKE NA KUNYWA DAMU YAKE

  • WENGI WAKWAZIKA NA KUACHA KUMFUATA

Katika sinagogi fulani huko Kapernaumu, Yesu anafundisha kwamba yeye ndiye mkate wa kweli kutoka mbinguni. Inaonekana maneno hayo yanahusiana na mambo aliyowaambia watu waliorudi kutoka upande wa mashariki wa Bahari ya Galilaya, wale waliokula mikate na samaki alioandaa huko.

Yesu anaendeleza mazungumzo kwa kusema: “Mababu zenu walikula mana nyikani na bado wakafa.” Kinyume chake anaeleza: “Mimi ndio mkate ulio hai ambao ulishuka kutoka mbinguni. Yeyote akila mkate huu ataishi milele; na kwa kweli, mkate nitakaotoa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”—Yohana 6:48-51.

Katika majira ya kuchipua ya mwaka wa 30 W.K., Yesu alimwambia Nikodemo kwamba Mungu aliupenda ulimwengu sana hivi kwamba akamtoa Mwana wake awe Mwokozi. Sasa Yesu anakazia uhitaji wa kula mwili wake kwa kuonyesha imani katika dhabihu ambayo atatoa. Hiyo ndiyo njia ya kupokea uzima wa milele.

Hata hivyo, watu hawakubaliani na maneno ya Yesu. Wanauliza: “Mtu huyu anawezaje kutupatia mwili wake tule?” (Yohana 6:52) Yesu anataka waelewe kwamba anamaanisha mwili wa mfano bali si mwili halisi. Maneno anayoongezea yanaonyosha kwamba anamaanisha hivyo.

“Msipokula mwili wa Mwana wa binadamu na kunywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Yeyote akila mwili wangu na kunywa damu yangu ana uzima wa milele, . . . kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Yeyote anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu hubaki katika muungano nami.”—Yohana 6:53-56.

Wazia jinsi jambo hilo linavyowaudhi Wayahudi wanaomsikiliza! Huenda wakafikiri kwamba Yesu anadokeza zoea la kula nyama ya binadamu au kuvunja sheria ya Mungu dhidi ya kula damu. (Mwanzo 9:4; Mambo ya Walawi 17:10, 11) Lakini Yesu hazungumzii kula mwili au kunywa damu kihalisi. Anaonyesha kwamba wote wanaotaka uzima wa milele ni lazima waonyeshe imani katika dhabihu ambayo atatoa atakapotoa mwili wake mkamilifu wa kibinadamu na kumwaga damu yake. Ingawa hivyo, wengi kati ya wanafunzi wake hawaelewi jambo analofundisha. Baadhi yao wanasema: “Maneno hayo yanashtua; ni nani anayeweza kuyasikiliza?”—Yohana 6:60.

Yesu anapotambua kwamba baadhi ya wanafunzi wake wananung’unika, anauliza: “Je, jambo hili limewakwaza? Basi, itakuwaje mtakapomwona Mwana wa binadamu akipanda kurudi kule alikotoka? . . . Maneno niliyowaambia ni roho na ni uzima. Lakini kuna wengine kati yenu ambao hawaamini.” Baada ya hapo, wengi kati ya wanafunzi wake wanaondoka na hawamfuati tena.—Yohana 6:61-64.

Basi Yesu anawauliza mitume wake 12 swali hili: “Je, ninyi pia mnataka kwenda?” Petro anamjibu: “Bwana, tutaenda kwa nani? Wewe una maneno ya uzima wa milele. Tumeamini na tumejua kwamba wewe ndiye Mtakatifu wa Mungu.” (Yohana 6:67-69) Maneno hayo yanaonyesha ushikamanifu mkubwa sana, ingawa kufikia wakati huu Petro na mitume wengine hawaelewi kikamili jambo ambalo Yesu anafundisha!

Akiwa amefurahishwa na jibu la Petro, Yesu anasema: “Niliwachagua ninyi 12, sivyo? Lakini mmoja wenu ni mchongezi.” (Yohana 6:70) Yesu anazungumza kuhusu Yuda Iskariote. Inawezekana kufikia wakati huu Yesu ametambua kwamba Yuda ameanza kuongozwa na tamaa mbaya.

Lakini bado Yesu anaridhika sana kujua kwamba Petro na wale mitume wengine hawajashawishiwa kuacha kumfuata wala kuacha kushiriki katika kazi ya kuokoa uhai ambayo anafanya.