Mitume 12 wamefurahia safari yao ya kuhubiri katika eneo lote la Galilaya, nao wanamsimulia Yesu “mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha.” Inaeleweka kwamba wamechoka. Ingawa hivyo, hata hawana muda wa kula kwa sababu watu wengi sana wanakuja na kwenda. Basi, Yesu anasema: “Twendeni faraghani mahali pasipo na watu ili mpumzike kidogo.”—Marko 6:30, 31.

Wanapanda mashua, labda karibu na Kapernaumu, na kuelekea eneo lisilo na watu mashariki ya Mto Yordani mbele ya Bethsaida. Hata hivyo, watu wengi wanawaona wakiondoka, na wengine wanasikia kuhusu jambo hilo. Wanakimbia pamoja kandokando ya bahari, na mashua inapofika huko tayari wamefika.

Anapotoka kwenye mashua, Yesu anauona umati naye anausikitikia, kwa maana wao ni kama kondoo wasio na mchungaji. Basi anaanza “kuwafundisha mambo mengi” kuhusu Ufalme. (Marko 6:34) Pia, anawaponya ‘wale wanaohitaji kuponywa.’ (Luka 9:11) Muda unapozidi kusonga, wanafunzi wanamwambia: “Mahali hapa hapana watu na muda umesonga sana; uambie umati uondoke, waende vijijini wakajinunulie chakula.”—Mathayo 14:15.

Yesu anawajibu: “Si lazima waondoke; ninyi wapeni chakula.” (Mathayo 14:16) Ingawa tayari Yesu anajua jambo atakalofanya, anamjaribu Filipo kwa kumuuliza: “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” Anamuuliza Filipo kwa sababu anatoka Bethsaida, eneo lililo hapo karibu. Lakini, bado suluhisho sio kununua mikate. Kuna wanaume karibu 5,000. Na huenda jumla ya watu ni mara mbili ya idadi hiyo, tukihesabu wanawake na watoto! Filipo anajibu: “Mikate ya dinari 200 [dinari moja ni mshahara wa siku moja] haiwezi kutosha hata tukimpa kila mmoja wao kipande kidogo.”—Yohana 6:5-7.

Labda ili kuonyesha kwamba haiwezekani kuwalisha watu hao wote, Andrea anasema: “Hapa kuna mvulana mdogo aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Je, hivi vitawatosha watu wengi hivi?”—Yohana 6:9.

Ni majira ya kuchipua, kabla tu ya Pasaka ya mwaka wa 32 W.K., na kwenye vilima kuna nyasi za kijani. Yesu anawaagiza wanafunzi wake wawaambie watu waketi kwenye nyasi katika vikundi vya watu 50 na 100. Anachukua ile mikate mitano na samaki wawili na kumshukuru Mungu. Kisha anamega ile mikate na kugawa wale samaki. Yesu anawapatia wanafunzi ili wawagawie watu. Kwa kushangaza, watu wote wanakula mpaka wanashiba!

Baadaye Yesu anawaambia wanafunzi wake: “Kusanyeni vipande vilivyobaki, ili chochote kisipotee.” (Yohana 6:12) Wanakusanya chakula kilichobaki na kujaza vikapu 12!