Visehemu vya damu. Visehemu vya damu hutokana na zile sehemu nne kuu za damu, yaani, chembe nyekundu, chembe nyeupe, chembelele (platelets), na utegili (plasma). Kwa mfano, chembe nyekundu zina protini inayoitwa himoglobini. Dawa ambazo zinatengenezwa kutokana na himoglobini ya binadamu au mnyama hutumiwa kutibu wagonjwa wenye upungufu wa damu au waliopoteza damu nyingi.

Utegili—ambao asilimia 90 yake ni maji—una homoni mbalimbali, chumvi, vimeng’enya, na lishe, kutia ndani madini na sukari. Pia, utegili huwa na vigandisha-damu, kingamwili zinazopigana na magonjwa, na protini kama vile albumini. Mtu akipata ugonjwa fulani, madaktari wanaweza kupendekeza adungwe sindano yenye kingamwili (gamma globulin), ambayo inatengenezwa kutokana na utegili wa watu ambao tayari wana kinga ya ugonjwa huo. Protini fulani (interferons na interleukins) zinaweza kutolewa katika chembe nyeupe za damu na kutumiwa kutibu magonjwa fulani ya virusi na kansa mbalimbali.

Je, Wakristo wanaweza kukubali matibabu yanayohusisha visehemu vya damu? Biblia haitoi maagizo ya moja kwa moja, kwa hiyo kila mtu anapaswa kujiamulia kulingana na dhamiri yake mwenyewe mbele za Mungu. Huenda wengine wakakataa visehemu vyote, wakisema kwamba kulingana na Sheria ambayo Mungu aliwapa Waisraeli, damu ambayo ilitolewa kwa kiumbe ilipaswa ‘kumwagwa kwenye udongo.’ (Kumbukumbu la Torati 12:22-24) Ingawa wengine wanakataa kutiwa damu mishipani  au sehemu zake kuu, huenda wakakubali matibabu yanayohusisha kisehemu fulani. Kwa maoni yao, visehemu vinavyotokana na damu haviwakilishi tena uhai wa kiumbe ambaye damu yake ilitumiwa.

Unapofanya maamuzi kuhusu visehemu vya damu, fikiria maswali yafuatayo: Je, ninaelewa kwamba kukataa visehemu vyote kunamaanisha sitakubali matibabu fulani yanayotia ndani dawa fulani za kupigana na magonjwa au zinazoweza kusaidia damu kuganda ili iache kuvuja? Je, ninaweza kumweleza daktari kwa nini nakataa au nakubali kisehemu kimoja cha damu au zaidi?

Mbinu zinazotumiwa na madaktari. Zinatia ndani uzimuaji wa damu (hemodilution) na uokoaji wa chembe za damu (cell salvage). Uzimuaji wa damu hufanywa kwa kutoa damu ya mgonjwa na kuielekeza kando na badala yake kumtia umajimaji fulani, kisha damu iliyokuwa imeelekezwa kando hurudishwa katika mwili wa mgonjwa. Uokoaji wa chembe za damu ni mbinu ambayo hutumiwa kukusanya na kurudisha damu inayotoka mwilini wakati wa upasuaji. Damu inayotoka mahali palipokatwa au panapovuja, husafishwa au kuchujwa na kurudishwa katika mwili wa mgonjwa. Kwa sababu madaktari hutumia mbinu hizo kwa njia tofauti-tofauti, Mkristo anapaswa kujua jambo ambalo daktari wake anakusudia kufanya.

Unapofanya maamuzi kuhusu mbinu hizo za matibabu, jiulize: ‘Ikiwa kiasi fulani cha damu yangu kitaelekezwa nje ya mwili wangu na huenda hata mtiririko ukakatizwa kwa muda fulani, je, dhamiri yangu itaniruhusu kuiona damu hiyo kuwa sehemu  ya mwili wangu, na hivyo basi isiwe lazima “[kuimwaga] kwenye udongo”? (Kumbukumbu la Torati 12:23, 24) Je, dhamiri yangu iliyozoezwa na Biblia itanisumbua ikiwa wakati wa matibabu sehemu ya damu yangu itatolewa, ichanganywe na dawa fulani, na kurudishwa mwilini mwangu? Je, ninaelewa kwamba kukataa matibabu yote yanayohusisha matumizi ya damu yangu kunamaanisha kwamba sitakubali kupimwa damu, sitakubali damu yangu ipitishwe katika mashini ya kuchuja na kusafisha damu  kisha kurudishwa mwilini mwangu, wala sitakubali mashini inayofanya kazi badala ya moyo na mapafu?’

Mkristo anapaswa kujiamulia jinsi damu yake itakavyotumiwa wakati wa matibabu. Hilo linahusu pia njia za kupima magonjwa na matibabu ya kisasa ambayo yanahusisha kutoa kiasi kidogo cha damu, na labda kuichanganya na dawa fulani kisha kuirudisha mwilini.