Yesu aanzisha maadhimisho mapya; asalitiwa na kutundikwa mtini

BAADA ya Yesu kuhubiri na kufundisha kwa miaka mitatu na nusu, alijua kwamba anakaribia mwisho wa maisha yake duniani. Viongozi wa dini Wayahudi walikuwa wakipanga njama ya kumuua, lakini wakawaogopa watu walioamini kwamba yeye ni nabii. Wakati huohuo, Shetani alimshawishi mmoja wa mitume 12 wa Yesu—Yuda Iskariote—akawa msaliti. Viongozi wa dini walimpa Yuda vipande 30 vya fedha ili amsaliti Yesu.

Usiku wake wa mwisho, Yesu aliwakusanya mitume wake kuadhimisha Pasaka. Baada ya Yuda kuondoka, Yesu alianzisha maadhimisho mapya, Mlo wa Jioni wa Bwana. Akachukua mkate, akashukuru, akawapa wale mitume 11 waliobaki. Akasema: “Huu unamaanisha mwili wangu ambao utatolewa kwa ajili yenu. Endeleeni kufanya hivi kwa kunikumbuka mimi.” Alifanya vivyo hivyo kuhusiana na kikombe na kusema: “Kikombe hiki kinamaanisha agano jipya kwa msingi wa damu yangu.”—Luka 22:19, 20.

Yesu alikuwa na mengi ya kuwaambia mitume wake usiku huo. Aliwapa amri mpya—kwamba wapendane bila ubinafsi. Aliwaambia: “Kwa jambo hili wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo kati yenu wenyewe.” (Yohana 13:34, 35) Aliwahimiza wasiruhusu mioyo yao itaabike kwa sababu ya mambo yenye kuhuzunisha yaliyokuwa karibu kutokea. Yesu alisali sana kwa ajili yao. Wakaimba nyimbo za sifa na kuondoka.

Wakiwa katika bustani ya Gethsemane, Yesu akapiga magoti na kumimina moyo wake katika sala. Punde si punde askari-jeshi wenye silaha, makuhani, na watu wengine wakaja kumkamata. Yuda akakaribia na kumtambulisha Yesu kwao kwa kumbusu. Askari-jeshi hao walipomkamata Yesu, mitume wakatoroka.

Yesu akiwa mbele ya mahakama kuu ya Wayahudi, alijitambulisha kuwa Mwana wa Mungu. Mahakama hiyo ilimhukumu kuwa na hatia ya kukufuru na anastahili kifo. Baada ya hapo Yesu akapelekwa kwa Gavana Mroma, Pontio Pilato. Ingawa hakumpata Yesu kuwa na hatia, alimkabidhi Yesu kwa umati uliotaka auawe.

Kisha Yesu akapelekwa Golgotha, ambapo askari-jeshi Waroma walimtundika mtini. Kimuujiza, giza likaingia katikati ya mchana. Baadaye, alasiri hiyohiyo, Yesu akafa na kukawa na tetemeko kubwa la nchi. Mwili wake ukalazwa katika kaburi lililokuwa limechongwa katika mwamba. Siku iliyofuata, makuhani wakalifunika kaburi na kuweka mlinzi katika mwingilio wake. Je, Yesu angeendelea kuwa kaburini? Hapana. Muujiza mkubwa kuliko yote ulikuwa karibu kutokea.

—Inatoka kwenye Mathayo, sura ya 26 na 27; Marko sura, ya 14 na 15; Luka, sura ya 22 na 23; Yohana, sura ya 12 hadi 19.

^ fu. 15 Unaweza kupata habari zaidi kuhusu thamani ya kifo cha Yesu, tazama Sura ya 5 ya kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa?