Mungu auharibu ulimwengu mwovu; amwokoa Noa na familia yake

WANADAMU walipozidi kuongezeka, dhambi na uovu zilizidi duniani. Enoko, nabii aliyekuwa peke yake, alionya kwamba siku moja Mungu atawaharibu waovu. Hata hivyo, uovu ulizidi. Malaika fulani walimwasi Yehova kwa kuacha makao yao mbinguni, wakajivika miili ya kibinadamu, wakaja duniani na kujitwalia wanawake kuwa wake zao. Mahusiano hayo yasiyo ya kawaida yalitokeza Wanefili, majitu yenye kukandamiza yaliyozidisha jeuri na umwagaji damu duniani. Mungu alihuzunika sana kuona uumbaji wake ukiharibiwa.

Baada ya kifo cha Enoko, kuna mtu mmoja aliyekuwa tofauti kabisa na ulimwengu mwovu uliomzunguka. Aliitwa Noa. Yeye na familia yake walijitahidi kufanya yaliyo sawa machoni pa Mungu. Mungu aliamua kuwaharibu waovu. Hata hivyo, hakutaka kumwangamiza Noa na wanyama pamoja nao. Kwa hiyo Mungu akamwambia ajenge safina—chombo kikubwa chenye umbo la sanduku. Humo, Noa na familia yake wangehifadhiwa wakiwa hai, pamoja na wanyama wa aina mbalimbali, na kuokoka gharika ya dunia nzima. Noa alimtii Mungu. Kwa makumi ya miaka ambayo Noa alijenga safina hiyo, alikuwa pia “mhubiri wa uadilifu.” (2 Petro 2:5) Aliwaonya watu kuhusu Gharika iliyokuwa ikikaribia, lakini wakampuuza. Wakati ulipofika, Noa na familia yake wakaingia katika safina pamoja na wanyama. Mungu akaufunga mlango wa safina. Mvua ikanyesha.

Mvua ikamwagika bila kukoma kwa siku 40, mchana na usiku, mpaka dunia yote ikafunikwa. Waovu wote wakaangamia. Miezi kadhaa baadaye, maji yalipopungua, safina ikatua juu ya mlima. Kufikia wakati ambapo Noa na familia yake pamoja na wanyama wangeweza kutoka nje ya safina, mwaka mzima ulikuwa umepita. Noa alionyesha shukrani zake kwa kumtolea Yehova toleo. Mungu alikubali toleo hilo na kumhakikishia Noa na familia yake kwamba hataleta tena gharika ili kuondolea mbali kila kitu chenye uhai kutoka katika uso wa dunia. Yehova aliandaa upinde wa mvua uwe ishara ya kuwakumbusha ahadi hiyo yenye kufariji.

Baada ya Gharika, Mungu aliwapa wanadamu amri kadhaa mpya. Aliwaruhusu kula nyama za wanyama. Hata hivyo aliwakataza wasile damu. Pia aliwaamuru wazao wa Noa waijaze dunia, lakini baadhi yao wakaasi. Watu walijiunga na Nimrodi katika uasi nao wakaanza kujenga mnara mkubwa katika jiji la Babeli, ambalo baadaye lilikuja kuitwa Babiloni. Lengo lao lilikuwa kukaidi amri ya Mungu ya kuijaza dunia. Hata hivyo, Mungu alivunja mipango ya waasi hao kwa kuvuruga lugha yao moja na kuwafanya wazungumze lugha mbalimbali. Kwa kuwa hawakuweza kuwasiliana, waliuacha mradi huo na kutawanyika.

—Inatoka kwenye Mwanzo sura ya 6 hadi 11; Yuda 14, 15.