Yehova aleta mapigo juu ya Misri, na Musa awaongoza wana wa Israeli kutoka katika nchi hiyo. Mungu awapa Waisraeli Sheria kupitia Musa

WANA wa Israeli waliishi Misri kwa miaka mingi, wakizidi kuongezeka na kupata ufanisi. Hata hivyo, Farao mpya alitokea. Mtawala huyo hakumjua Yosefu. Mtawala huyo mkatili aliyehofu idadi inayozidi kuongezeka ya Waisraeli, aliwafanya kuwa watumwa na kuagiza wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wauawe kwa kutupwa katika Mto Nile. Lakini mama mmoja mwenye ujasiri alimhifadhi mwana wake mchanga, akamweka katika kikapu na kumficha katikati ya matete. Binti ya Farao alimpata mtoto huyo, akamwita Musa, na kumlea katika nyumba ya kifalme ya Misri.

Musa alipokuwa na umri wa miaka 40, alijikuta taabani alipompiga Mmisri aliyekuwa akimpiga mtumwa Mwisraeli. Musa alikimbilia nchi ya mbali, alikoishi uhamishoni. Musa alipokuwa na umri wa miaka 80, Yehova alimtuma arudi Misri, asimame mbele ya Farao na kudai watu wa Mungu waachiliwe.

Farao alikataa katakata. Kwa hiyo Mungu akaleta mapigo kumi juu ya Misri. Kila mara Musa aliposimama mbele ya Farao na kumpa nafasi ya kuepuka pigo linalofuata, Farao alikuwa mkaidi, na kumwonyesha Musa na Mungu wake, Yehova, dharau. Mwishowe, pigo la kumi lilitokeza kifo cha wazaliwa wote wa kwanza nchini—isipokuwa wale wa familia zilizomtii Yehova kwa kutia alama miimo ya milango yao kwa damu ya mwana-kondoo aliyetolewa dhabihu. Malaika wa Mungu aliyetumwa kuwaangamiza wazaliwa wote wa kwanza alipita nyumba zilizokuwa na alama. Baadaye Waisraeli walifanya maadhimisho ya kila mwaka yanayoitwa Pasaka ili kukumbuka ukombozi huo wa pekee.

Baada ya kumpoteza mwana wake mwenyewe mzaliwa wa kwanza, Farao aliagiza Musa na Waisraeli wengine wote waondoke Misri. Mara moja wakapanga umati huo mkubwa uondoke Misri. Lakini Farao akabadili nia. Akawafuata akiwa na askari wengi na magari ya vita. Ilionekana kana kwamba Waisraeli hawana pa kwenda kwa kuwa walikuwa katika ufuo wa Bahari Nyekundu. Yehova alitenganisha maji ya Bahari Nyekundu, na hivyo Waisraeli wakapita katika sakafu kavu ya bahari, katikati ya kuta za maji! Wamisri walipoingia wakiwafuata, Mungu aliyaachilia yale maji, yakarudi kwa kishindo na kumfunika Farao pamoja na jeshi lake.

Baadaye, Waisraeli walipopiga kambi katika Mlima Sinai, Yehova alifanya agano pamoja nao. Akimtumia Musa kuwa mpatanishi, Mungu aliwapa Waisraeli sheria za kuwaongoza na kuwalinda katika nyanja zote maishani. Maadamu Waisraeli wangeukubali kabisa utawala wa Mungu, Yehova angekuwa pamoja nao na kulifanya taifa hilo kuwa baraka kwa wengine.

Hata hivyo, inasikitisha kwamba Waisraeli wengi hawakumwamini Mungu. Kwa hiyo, Yehova akafanya kizazi hicho kitange-tange nyikani kwa miaka 40. Kisha, Musa akamteua Yoshua, aliyekuwa mtu mnyoofu, achukue mahali pake. Hatimaye, taifa la Israeli likakaribia kuingia nchi ambayo Mungu alimwahidi Abrahamu.

—Inatoka kwenye Kutoka; Mambo ya Walawi; Hesabu; Kumbukumbu la Torati; Zaburi 136:10-15; Matendo 7:17-36.