Shetani alipotumia nyoka kunena na Hawa, Hawa alijiunga naye katika kumwasi Mungu

Watu wote wa roho ambao Yehova aliumba walikuwa wema. Halafu malaika mmoja akageuka akawa mbaya. Yeye ni Shetani Ibilisi. Shetani alitaka watu duniani wamwabudu yeye badala ya kuabudu Yehova. Hivi ndivyo ilivyotukia:

Katika bustani ya Edeni, mlikuwamo miti mingi iliyozaa matunda matamu sana. Yehova alimwambia Adamu na Hawa, mke wake, kwamba wangeweza kula kutokana nayo kama wapendavyo. Lakini ulikuwako mti mmoja ambao Mungu alisema hawapaswi kula kutokana nao. Alisema kwamba wakila kutokana nao, wangekufa hakika.—Mwanzo 2:9, 16, 17.

Siku moja Hawa alikuwa peke yake wakati nyoka aliposema naye. Bila shaka, kwa kweli si nyoka aliyeongea; ni Shetani Ibilisi aliyefanya ionekane kama kwamba ni nyoka aliyekuwa akisema. Shetani alimwambia Hawa kwamba kama angekula kutokana na tunda lililokatazwa, yeye angekuwa mwenye hekima kama Mungu. Alisema pia kwamba hangekufa kamwe. Taarifa zote mbili zilikuwa uwongo. Hata hivyo, Hawa aliamini Shetani akala tunda lile. Baadaye, alimpa Adamu baadhi yake, naye akala vilevile.—Mwanzo 3:1-6.

Kutokana na hadithi hii ya kweli, twajifunza kwamba Shetani ni mwasi na mwongo. Alimwambia Hawa kwamba akikosa kutii Mungu, hangekufa. Huo ulikuwa uwongo. Alikufa na ndivyo na Adamu. Shetani hakufa wakati huo, ijapokuwa atakufa hatimaye kwa sababu  alitenda dhambi. Hata hivyo, kwa sasa, yeye yuko hai naye huendelea kupoteza ainabinadamu. Angali ni mwongo, naye hujaribu kuwafanya watu wavunje sheria za Mungu.—Yohana 8:44.

Malaika Wengine Waasi

Baadaye, malaika wengine waligeuka wakawa wabaya. Malaika hao waliona wanawake wazuri duniani nao wakataka kuwa na mahusiano ya kingono pamoja nao. Kwa hiyo walikuja duniani wakavaa miili ya kiume ya kibinadamu. Kisha wakajitwalia wanawake. Hiyo ilikuwa kinyume cha kusudi la Mungu.—Mwanzo 6:1, 2; Yuda 6.

Malaika waovu walikuja duniani kufanya mambo yasiyo ya adili pamoja na wanawake

Pia ilitokeza taabu nyingi kwa ainabinadamu. Wake za malaika hao walizaa watoto, lakini hawakuwa watoto wa kawaida. Walikua wakawa majitu wajeuri na wakatili. Hatimaye dunia ikaja kujawa na jeuri sana hivi kwamba Yehova akaamua kuangamiza watu hao waovu kwa furiko kubwa. Wanadamu pekee waliookoka Furiko hilo walikuwa Noa mwadilifu na familia yake.—Mwanzo 6:4, 11; 7:23.

Hata hivyo, wale malaika waovu walirudi kwenye makao ya roho; wao hawakufa. Lakini waliadhibiwa. Hawakuruhusiwa kurudi katika familia ya Mungu ya malaika waadilifu. Zaidi ya hilo, Yehova hakuwaruhusu tena wavae miili ya kibinadamu. Na hatimaye watakufa wakati wa ile hukumu kuu.—2 Petro 2:4; Yuda 6.

 Shetani Atupwa Nje ya Mbingu

Shetani na malaika zake wabaya walitupwa nje ya mbingu

Mapema katika karne hii, kulikuwa na vita mbinguni. Kitabu cha Biblia cha Ufunuo hueleza yaliyotukia: “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli [Yesu Kristo aliyefufuliwa] na malaika zake [wema] wakapigana na yule joka [Shetani], yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake [wabaya]; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake [wabaya] wakatupwa pamoja naye.”

Matokeo yakawa nini? Masimulizi yaendelea: “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo.” Wale malaika wema wangeweza kushangilia kwa sababu Shetani na malaika zake wabaya, au roho, hawakuwamo tena mbinguni. Lakini namna gani watu duniani? Biblia husema: “Ole wa nchi na bahari! kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”—Ufunuo 12:7-9, 12.

Ndiyo, Shetani na waandamani wake waovu huwapoteza na kusababisha ole mkubwa kwa watu duniani. Malaika hao waovu wanaitwa mashetani. Wao ni maadui wa Mungu. Wote ni waovu.