“MIMI humshukuru Yehova mara nyingi sana kwamba nilijifunza kumhusu katika lugha yangu ya mama,” anasema Gulizar.

Kwa miaka minane, Gulizar alikuwa mhubiri ambaye hajabatizwa. Alibatizwa baada ya kuhudhuria mikutano katika lugha yake ya Kikurdi. Yeye ni miongoni mwa Wakurdi wengi ambao wamekubali kweli katika miaka ya karibuni nchini Georgia. Wakurdi ni nani?

Wakurdi wameishi katika eneo la Mashariki ya Kati kwa karne nyingi. Wasomi fulani wanafikiri kuwa Wakurdi  wametokana na Wamedi wa kale wanaotajwa katika Biblia. (2 Fal. 18:11; Mdo. 2:9) Lugha yao ni mojawapo ya lugha za Iran.

Leo, mamilioni ya Wakurdi wanaishi katika nchi mbalimbali, kutia ndani Armenia, Iraki, Iran, Siria, na Uturuki. Kuna Wakurdi 20,000 hivi nchini Georgia. Kwa ujumla, wao ni watu wanaomwogopa Mungu na wanaheshimu sana mambo ya kiroho.

Sasa nchini Georgia, kuna wahubiri 500 ambao ni Wakurdi na makutaniko matatu ya Kikurdi. Katika mwaka wa 2014, walifurahia sana kusanyiko la eneo la kwanza la Kikurdi jijini Tbilisi, lililokuwa na wajumbe kutoka Armenia, Ujerumani, Ukrania, na Uturuki.