Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

2017— Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova

 GEORGIA

Upendo Unashinda Mipaka Iliyowekwa na Wanadamu

Upendo Unashinda Mipaka Iliyowekwa na Wanadamu

MUDA mrefu kabla ya Sanel kuzaliwa, madaktari waliwaambia wazazi wake kwamba ikiwa atakuwa hai anapozaliwa, basi atakuwa na matatizo makubwa ya afya. Tangu siku aliyozaliwa, Sanel alihitaji kufanyiwa upasuaji. Wazazi wake waliishi katika eneo la Abkhazia, ambalo lilijipatia uhuru kutoka nchi ya Georgia, na hawakupata daktari ambaye angefanya upasuaji huo bila kutumia damu.

Wazazi wa Sanel waliwasiliana na Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali (HLC) ya eneo lao. * Akina ndugu katika halmashauri hiyo walifanikiwa upesi kupata daktari ambaye alikubali kufanya upasuaji huo bila kutumia damu huko Tbilisi, mji mkuu wa Georgia. Mama ya Sanel hangeweza kusafiri kwa kuwa hakuwa amepata nafuu baada ya kujifungua. Kwa hiyo, iliamuliwa kwamba nyanya (bibi) zake, ambao wote ni Mashahidi, wamsafirishe mtoto huyo hadi hospitali jijini Tbilisi.

Upasuaji huo ulifanikiwa, ingawa ulikuwa tata. Muda mfupi baadaye nyanya za Sanel waliandika hivi: “Tulikaa hospitalini kwa zaidi ya siku 20. Muda huo wote, akina ndugu na dada wa Georgia walitutembelea na kutupa msaada tuliohitaji. Walitutia moyo sana. Tumesoma mara nyingi kuhusu upendo unaoonyeshwa na undugu wetu, lakini sasa tumeushuhudia kwa njia ya pekee.”

^ fu. 4 Nchini Georgia, wazee wanaotumikia katika HLC wamepata zaidi ya madaktari 250 ambao wanakubali kufanya upasuaji bila kutumia damu.