JE, KUNA mtu aliyewahi kukuibia?— Ulihisije?— Aliyekuibia ni mwizi na hakuna mtu anayependa mwizi. Unafikiri ni nini kinachomfanya mtu awe mwizi? Je, alizaliwa hivyo?—

Tayari tumejifunza kwamba watu wanazaliwa wakiwa na dhambi. Kwa hiyo sisi sote hatujakamilika. Lakini hakuna anayezaliwa akiwa mwizi. Mwizi anaweza kutoka katika familia nzuri. Wazazi wake, ndugu zake, na dada zake labda ni wanyofu. Lakini tamaa yake mwenyewe ya vitu kama pesa na vitu anavyoweza kununua kwa pesa inaweza kumfanya awe mwizi.

Unafikiri mwizi wa kwanza alikuwa nani?— Hebu tufikirie jambo hilo. Mwalimu Mkuu alipokuwa mbinguni alimjua mtu huyo. Mwizi huyo alikuwa malaika. Lakini ikiwa Mungu aliwaumba malaika wakiwa wakamilifu, ilikuwaje malaika huyo akawa mwizi?— Kama tulivyojifunza katika Sura ya 8 ya kitabu hiki, alitaka kitu ambacho hakikuwa chake. Unakumbuka alitaka nini?—

Baada ya Mungu kuumba mwanamume na mwanamke wa kwanza, malaika huyo alitaka wamwabudu. Hakuwa na haki ya kudai ibada hiyo. Wao walipaswa kumwabudu Mungu. Lakini Shetani aliiba! Kwa kufanya Adamu na Hawa wamwabudu, malaika huyo akawa mwizi. Akawa Shetani Ibilisi.

Ni nini kinachomfanya mtu kuwa mwizi?— Ni kutamani kitu kisichokuwa chake. Tamaa hiyo inaweza kuwa yenye nguvu sana hivi kwamba inaweza kuwafanya hata watu wazuri watende mambo mabaya. Wakati mwingine watu wanaokuwa wezi  wanaendelea kuiba bila kuacha. Mmoja wao alikuwa mtume wa Yesu. Anaitwa Yuda Iskariote.

Yuda alijua kwamba ni kosa kuiba kwa sababu alifundishwa Sheria ya Mungu tangu utotoni. Hata alijua kwamba wakati mmoja Mungu aliongea kutoka mbinguni na kuwaambia watu wake hivi: ‘Msiibe.’ (Kutoka 20:15) Yuda alipokuwa mtu mzima, alikutana na Mwalimu Mkuu, akawa mmoja wa wanafunzi wake. Baadaye, Yesu hata akamchagua Yuda kuwa mmoja wa wale mitume 12.

Yesu na mitume wake walikuwa wakisafiri pamoja, wakila pamoja. Na pesa zao zote ziliwekwa ndani ya sanduku. Yesu alimpa Yuda hilo sanduku alitunze. Pesa hazikuwa za Yuda. Lakini unajua Yuda alifanya nini baadaye?—

Kwa nini Yuda aliiba?

Yuda alianza kuchukua pesa kutoka kwenye sanduku hilo ingawa hakupaswa kufanya hivyo. Alikuwa akichukua pesa hizo wakati wengine hawamwoni na hata alijaribu kutafuta njia ya kupata pesa nyingi zaidi. Akaanza kufikiria juu ya pesa kila wakati. Tuone tamaa hiyo mbaya ilitokeza nini siku chache tu kabla ya Mwalimu Mkuu kuuawa.

Maria dada ya Lazaro, rafiki ya Yesu alichukua mafuta yenye thamani sana na kummwagia Yesu miguuni. Lakini Yuda akalalamika. Unajua ni kwa nini?— Alidai kwamba mafuta hayo yangeuzwa na pesa zipewe maskini. Lakini hasa alitaka kuwe na pesa nyingi ndani ya sanduku ili baadaye aziibe.—Yohana 12:1-6.

Yesu akamwambia Yuda aache kumsumbua Maria kwa sababu Maria ameonyesha fadhili. Yuda hakufurahi Yesu alipomwambia hivyo, basi akawaendea makuhani wakuu waliokuwa maadui wa Yesu. Walitaka  kumkamata Yesu lakini walitaka kufanya hivyo usiku ili wasionekane na watu.

Yuda akawaambia makuhani: ‘Mkinipa pesa nitawaambia jinsi ya kumkamata Yesu. Mtanipa pesa ngapi?’

‘Tutakupa vipande 30 vya fedha,’ makuhani wakamjibu.—Mathayo 26:14-16.

Yuda akachukua pesa. Tendo hilo ni sawa tu na kumwuza Mwalimu Mkuu kwa watu hao! Je, kweli mtu anaweza kufanya jambo baya kama hilo?— Kwa kusikitisha, mambo huwa hivyo mtu anapokuwa mwizi na kuiba pesa. Anapenda pesa kuliko watu au hata Mungu.

Labda unawazia hivi, ‘Siwezi kamwe kupenda chochote kuliko vile ninavyompenda Yehova Mungu.’ Ni vizuri kwamba unahisi hivyo. Yesu alipomchagua Yuda kuwa mtume, labda hivyo ndivyo Yuda alivyohisi. Wengine ambao baadaye walikuwa wezi labda walihisi hivyo pia. Hebu tuzungumzie baadhi yao.

Akani na Daudi wanafikiria mambo gani mabaya?

Mmoja wao alikuwa mtumishi wa Mungu anayeitwa Akani na yeye aliishi mapema kabla ya Mwalimu Mkuu kuzaliwa. Akani  aliona vazi maridadi, dhahabu, na vipande vya fedha. Vitu hivyo havikuwa vyake. Biblia inasema kwamba vitu hivyo vilikuwa vya Yehova kwa sababu vilikuwa vimetolewa kwa maadui wa watu wa Mungu. Lakini Akani alivitamani sana mpaka akaviiba.—Yoshua 6:19; 7:11, 20-22.

Hebu ona mfano mwingine. Hapo zamani, Yehova alimchagua Daudi awe mfalme wa watu wa Israeli. Siku moja, Daudi alianza kumtazama mwanamke mrembo anayeitwa Bath-sheba. Aliendelea kumtazama Bath-sheba na kufikiria namna angeweza kumchukua ili awe mke wake. Lakini mwanamke huyo alikuwa mke wa Uria. Daudi alipaswa kufanya nini?—

Daudi alipaswa kuacha kufikiria kumchukua Bath-sheba. Lakini hakuacha.  Basi Daudi akampeleka nyumbani kwake. Kisha akapanga Uria auawe. Kwa nini Daudi alifanya mambo mabaya hivyo?— Kwa sababu aliendelea kumtamani mke wa mtu mwingine.—2 Samweli 11:2-27.

Absalomu alikuwa mwizi kwa njia gani?

Daudi aliomba msamaha, Yehova akamwacha aishi. Lakini kuanzia wakati huo, Daudi akawa na matatizo mengi sana. Absalomu mwana wake akataka kunyakua ufalme kutoka kwa Daudi. Basi, watu walipoenda kumwona Daudi, Absalomu aliwakumbatia na kuwabusu. Biblia inasema: “Absalomu akaendelea kuiba mioyo ya watu wa Israeli.” Aliwafanya watu waamini kwamba yeye anapaswa kuwa mfalme badala ya Daudi.—2 Samweli 15:1-12.

Umewahi kutamani kitu sana, kama Akani, Daudi, na Absalomu?— Iwapo kitu hicho ni cha mtu mwingine, kukichukua bila ruhusa ni wizi. Je, unakumbuka mwizi wa kwanza, Shetani, alitaka nini?— Alitaka watu wamwabudu yeye badala ya kumwabudu Mungu. Kwa hiyo Shetani alikuwa anaiba alipowafanya Adamu na Hawa wamtii.

Mtu akiwa na kitu, ana haki ya kuamua ni nani atakayekitumia. Kwa mfano, unaweza kwenda kucheza na watoto wengine nyumbani kwao. Je, ni vizuri kuchukua kitu huko na kupeleka kwenu?— Unaweza kukichukua tu ikiwa baba au mama ya watoto hao amekuruhusu. Ukichukua kitu chochote bila kuwaomba ni wizi.

Kwa nini unaweza kupata kishawishi cha kuiba?— Kwa sababu unataka kitu ambacho si chako. Hata kama hakuna mtu mwingine anayekuona, Yehova Mungu anakuona. Na tunapaswa kukumbuka kwamba Mungu anachukia wizi. Kwa hiyo kumpenda Mungu na kumpenda jirani kutakusaidia usiwe mwizi kamwe.

Biblia inaeleza wazi kwamba ni vibaya kuiba. Tafadhali soma Marko 10:17-19; Waroma 13:9; na Waefeso 4:28.