JE, UNAJUA mtu yeyote ambaye wakati wote hupenda kujitanguliza?— Anaweza kumsukuma mtu mwingine ili awe wa kwanza katika mstari. Umewahi kuona hilo likitendeka?— Mwalimu Mkuu aliona hata watu wazima wakijaribu kuwa wa kwanza, au kuwa mahali bora zaidi. Hakufurahia jambo hilo. Tuone kilichotendeka.

Umewahi kuona watu wakijaribu kujitanguliza?

Biblia inatuambia kwamba Yesu alialikwa kwenye karamu kubwa katika nyumba ya Farisayo, aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa dini. Baada ya Yesu kufika, alianza kuwatazama wageni wengine wakija na kuchagua mahali bora zaidi. Basi akawasimulia hadithi wale waliokuwa wamealikwa. Je, ungependa kuisikia?—

 Yesu alisema: ‘Ukialikwa kwenye karamu ya ndoa, usichague mahali bora, au pa maana zaidi.’ Unajua ni kwa nini Yesu alisema hivyo?— Alieleza kwamba labda kuna mtu mashuhuri zaidi aliyealikwa. Kwa hiyo, kama unavyoona kwenye picha, mwenye karamu anakuja na kumwambia: ‘Acha mtu huyu apate mahali hapa, na wewe nenda kule.’ Mgeni huyo anaonaje?— Anaaibika kwa sababu wale wageni wengine wote wanamwona akiondoka na kwenda mahali pa hali ya chini.

Yesu alikuwa akionyesha kwamba haifai kutaka mahali bora zaidi. Basi akasema: ‘Unapoalikwa kwenye karamu ya ndoa, nenda ukaketi mahali pa chini zaidi. Ndipo aliyekualika ajapo akuambie, “Rafiki, nenda juu zaidi.” Ndipo utakapokuwa na heshima mbele ya wageni wenzako wote walioalikwa.’ —Luka 14:1, 7-11.

Yesu alikuwa akifundisha somo gani aliposimulia kuhusu kukalia viti bora, au vya kwanza?

Umeelewa somo la hadithi hiyo ya Yesu?— Hebu tutoe mfano tuone kama umeelewa. Wazia unaingia katika basi ambalo limejaa watu. Je, ukimbilie kiti na kumwacha mtu mzima asimame?— Je, Yesu anaweza kufurahi ukifanya hivyo?—

Labda mtu atasema kwamba Yesu hajali yale tunayofanya. Lakini je, unaamini hivyo?— Yesu alipokuwa katika ile karamu kubwa nyumbani mwa Farisayo, alitazama watu wakichagua mahali pa kuketi. Je, hufikiri kwamba hata leo anapendezwa na yale tunayofanya?— Sasa Yesu akiwa mbinguni, bila shaka anatuona vizuri.

 Mtu anapojaribu kujitanguliza, matatizo yanaweza kutokea. Mara nyingi kunakuwa na mabishano, na watu wanakasirika. Wakati mwingine hayo yanatokea watoto wanaposafiri pamoja kwa basi. Mara tu milango ya basi inapofunguliwa, watoto hukimbia ili wawe wa kwanza. Wanataka kukaa mahali bora zaidi, karibu na madirisha. Ni nini kinachoweza kutokea?— Naam, wanaweza kukosana.

Kutaka kuwa wa kwanza kunaweza kuleta tatizo. Kulileta matatizo hata miongoni mwa mitume wa Yesu. Kama tulivyojifunza katika Sura ya 6 ya kitabu hiki, walibishana miongoni mwao kuhusu ni nani aliye mkubwa. Yesu alifanyaje wakati huo?— Aliwarekebisha. Lakini baadaye walibishana tena. Hebu tuone jinsi walivyoanza kubishana.

Mitume pamoja na wengine wanasafiri na Yesu kwa mara ya mwisho kwenda jijini Yerusalemu.  Yesu amekuwa akiwaambia kuhusu Ufalme wake, kwa hiyo Yakobo na Yohana wamekuwa wakiwazia kutawala wakiwa wafalme pamoja naye. Hata wameongea na mama yao Salome kuhusu jambo hilo. (Mathayo 27:56; Marko 15:40) Kwa hiyo wakiwa njiani kwenda Yerusalemu, Salome amjia Yesu, ainama mbele yake, na kuomba fadhili.

“Unataka nini?” Yesu auliza. Mama huyo anajibu akisema kwamba angependa wana wake wawili waketi kando ya Yesu, mmoja katika mkono wa kulia na mwingine mkono wa kushoto katika Ufalme wake. Wale mitume wengine kumi wanapojua kile ambacho Yakobo na Yohana wamemwambia mama yao awaulizie, unafikiri wanahisije?—

Salome anamwomba Yesu nini, na kunatokea nini?

Wanawakasirikia sana Yakobo na Yohana. Kwa hiyo Yesu anawapa mitume wake wote shauri zuri. Yesu anawaambia kwamba watawala  wa mataifa wanapenda kuwa na mamlaka nyingi na uwezo. Wanataka kuwa na cheo kikubwa ili kila mtu awatii. Lakini Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba hawapaswi kuwa hivyo. Badala yake, Yesu anasema: “Yeyote yule anayetaka kuwa wa kwanza katikati yenu lazima awe mtumwa wenu.” Fikiria jambo hilo! —Mathayo 20:20-28.

Unajua mtumwa hufanya nini?— Yeye huwahudumia wengine bila kutazamia wamhudumie. Yeye huchukua mahali pa chini sana, wala si mahali pa kwanza. Yeye hutenda kama mtu asiye wa maana sana. Na kumbuka Yesu alisema kwamba anayetaka kuwa wa kwanza anapaswa kuwatumikia wengine.

Unafikiri tunajifunza nini hapo?— Je, mtumwa anaweza kubishana na bwana wake kuhusu ni nani ataketi mahali bora zaidi? Au kweli anaweza kubishana kuhusu ni nani atakayekula kwanza? Unaonaje?— Yesu alieleza kwamba wakati wote mtumwa humtanguliza bwana wake.—Luka 17:7-10.

Kwa hiyo badala ya kujaribu kuwa wa kwanza, tunapaswa kufanya nini?— Tunapaswa kuwahudumia wengine. Na hiyo inamaanisha kuwatanguliza wengine. Inamaanisha kuwaona wengine kuwa bora kuliko sisi. Unaweza kufikiria njia ambazo unaweza kuwatanguliza wengine?— Hebu rejelea ukurasa wa 40 na 41 uone tena baadhi ya njia unazoweza kuwatanguliza wengine kwa kuwahudumia.

Kumbuka kwamba Mwalimu Mkuu aliwatanguliza wengine kwa kuwahudumia. Jioni ya mwisho aliyokuwa pamoja na mitume wake, hata aliinama akawaosha miguu. Sisi pia tukiwatanguliza wengine kwa kuwahudumia, tutamfurahisha Mwalimu Mkuu na Baba yake, Yehova Mungu.

Tusome maandiko mengine ya Biblia yanayotutia moyo kuwatanguliza wengine: Luka 9:48; Waroma 12:3; na Wafilipi 2:3, 4.