Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Jifunze Kutoka kwa Mwalimu Mkuu

 SURA YA 39

Mungu Amkumbuka Mwana Wake

Mungu Amkumbuka Mwana Wake

YESU alilia wakati rafiki yake Lazaro alipokufa. Unafikiri Yehova alihisi vibaya Yesu alipoteseka na kufa?— Biblia inasema kwamba Mungu anaweza ‘kuhuzunika’ na hata anaweza ‘kutiwa uchungu’ kutokana na mambo yanayotendeka.—Zaburi 78:40, 41; Yohana 11:35.

Unaweza kuwazia uchungu ambao Yehova alihisi alipomtazama Mwana wake mpendwa akifa?— Yesu alikuwa na hakika kwamba Mungu hangeweza kumsahau. Ndiyo sababu maneno yake ya mwisho kabla ya kufa yalikuwa: ‘Baba, naukabidhi uhai wangu mikononi mwako.’—Luka 23:46.

Yesu alikuwa na hakika kwamba atafufuliwa, na kwamba hangeachwa kaburini. Baada ya Yesu kufufuliwa, mtume Petro alinukuu yaliyoandikwa katika Biblia kumhusu Yesu, akisema: “Nafsi yake haikuachwa kuzimuni, wala mwili wake haukuona uharibifu.” (Matendo 2:31, King James Version; Zaburi 16:10) Mwili wa Yesu haukuharibika kaburini, yaani haukuoza na kunuka.

 Yesu alipokuwa duniani aliwaambia wanafunzi wake kwamba hangekufa kwa muda mrefu. Aliwaeleza kwamba ‘angeuawa, na siku ya tatu afufuliwe.’ (Luka 9:22) Hivyo basi, wanafunzi hawakupaswa kushangaa Yesu alipofufuliwa. Lakini, je, walishangaa?— Hebu tuone.

Ni karibu saa tisa hivi Ijumaa alasiri wakati Mwalimu Mkuu anapokufa mtini. Yosefu ni mshiriki tajiri wa Sanhedrini ambaye pia anamwamini Yesu kisiri. Anapogundua kwamba Yesu amekufa, anaenda kwa gavana Mroma, Pilato. Anaomba aruhusiwe kuuchukua mwili wa Yesu kutoka mtini ili auzike. Baadaye, Yosefu anabeba mwili wa Yesu mpaka kwenye bustani iliyo na kaburi, wanapozikwa wafu.

Baada ya mwili kuwekwa kaburini, jiwe kubwa likawekwa mbele yake. Basi kaburi likafungwa. Na sasa ni Jumapili, siku ya tatu. Kuna giza kwa sababu hakujapambazuka bado. Kuna watu wanaolinda kaburi. Wakuu wa makuhani wamewatuma watu hao kulilinda. Unajua ni kwa nini?—

Makuhani pia walisikia kwamba Yesu alisema angefufuliwa. Kwa hiyo ili kuwazuia wanafunzi wake wasiuibe mwili wa Yesu na kusema eti amefufuliwa, makuhani wanawaweka walinzi kulilinda kaburi. Kwa ghafula, ardhi inatikisika. Kunatokea nuru gizani. Ni malaika wa Yehova! Askari wanaogopa sana hata wanashindwa kusonga. Malaika anaenda kwenye kaburi na kuliondoa jiwe. Kaburi liko tupu!

Kwa nini kaburi liko tupu? Ni nini kimetokea?

Ndiyo, ni kama alivyosema mtume Petro baadaye: “Yesu huyo Mungu alimfufua.” (Matendo 2:32) Mungu alimfufua Yesu na kumpa mwili kama ule aliokuwa nao kabla ya kuja duniani. Alifufuliwa na mwili wa roho kama wa malaika. (1 Petro 3:18) Kwa hiyo  ni lazima Yesu awe na mwili wa nyama ili watu wamwone. Je, ndivyo anavyofanya?— Hebu tuone.

Sasa jua limeanza kuchomoza. Askari wameondoka. Maria Magdalene na wanawake wengine ambao ni wanafunzi wa Yesu wako njiani kuelekea kaburini. Wanasemezana: ‘Ni nani atakayetuondolea hilo jiwe zito?’ (Marko 16:3) Lakini wanapofika kaburini, jiwe tayari limeondolewa. Kumbe kaburi liko tupu! Mwili wa Yesu wa nyama haupo! Mara moja Maria Magdalene anakimbia kwenda kuwatafuta mitume wa Yesu.

Wale wanawake wengine wanabaki kaburini. Wanashangaa: ‘Yesu anaweza kuwa wapi?’ Ghafula watu wawili waliovaa mavazi yenye kung’aa wanatokea. Ni malaika! Wanawaambia wanawake hao: ‘Mbona mnamtafuta Yesu hapa? Amefufuliwa. Nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake.’ Wanawake hao wakatimua mbio wee! Wakiwa njiani wanakutana na mtu mmoja. Unajua ni nani?—

Kumbe ni Yesu ambaye ana mwili wa kibinadamu! Yeye pia anawaambia hao wanawake hivi: ‘Nendeni mkawaambie wanafunzi wangu.’ Wanawake hao wanafurahi. Wanawapata wanafunzi na kuwaambia: ‘Yesu yuko hai! Tumemwona!’ Maria tayari amewaambia Petro na Yohana kwamba kaburi liko tupu. Sasa wanakwenda huko kama unavyoona kwenye picha. Wanaangalia vitambaa ambavyo Yesu alifungiwa, lakini hawajui wafanyeje. Yesu yuko hai tena lakini wanashindwa kuamini.

Huenda Petro na Yohana wanafikiria nini?

Baadaye Jumapili hiyo, Yesu anawatokea wanafunzi wake wawili wakiwa barabarani kuelekea kijiji cha Emausi. Yesu anatembea na kuzungumza nao lakini hawamtambui kwa sababu hana mwili ule aliokuwa nao awali. Hawamtambui Yesu mpaka  anapokula na kutoa sala pamoja nao. Kwa sababu ya kujawa na shangwe, wanafunzi wanaharakisha kurudi Yerusalemu, ambao ni mwendo wa kilometa nyingi! Huenda ni muda mfupi tu baada ya hapo ambapo Yesu anamtokea Petro ili kumwonyesha kwamba Yeye yuko hai.

Kisha baadaye jioni ya Jumapili hiyo, wanafunzi wengi wamekusanyika katika chumba kimoja. Milango imefungwa. Ghafula Yesu yumo chumbani pamoja nao! Sasa wanajua kwamba Mwalimu Mkuu kwa kweli yuko hai tena. Wakajaa furaha iliyoje!—Mathayo 28:1-15; Luka 24:1-49; Yohana 19:38–20:21.

Kwa siku 40 Yesu anawatokea wanafunzi wake kwa miili mbalimbali ya kibinadamu kuwaonyesha kwamba yuko hai. Kisha anatoka duniani na kurudi mbinguni kwa Baba  yake. (Matendo 1:9-11) Upesi wanafunzi wanaanza kuwahubiria watu kwamba Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Hata makuhani wanapowapiga na kuwaua baadhi yao, hawaachi kuhubiri. Wanajua kwamba hata wakifa, Mungu atawakumbuka kama vile alivyomkumbuka Mwana wake.

Inapofika wakati ambao Yesu alifufuliwa, watu wengi hufikiria nini? Lakini wewe hufikiria nini?

Wanafunzi wa Yesu wa mapema walikuwa tofauti sana na watu wengi leo. Inapofika wakati ambao Yesu alifufuliwa, watu wa siku hizi hufikiria tu kula, kunywa, na kusherehekea. Lakini Biblia haisemi chochote kuhusu kusherehekea Ista. Inasema kuhusu kumtumikia Mungu.

Tunaweza kuwaiga wanafunzi wa Yesu kwa kuwaambia watu kwamba Mungu alifanya jambo la ajabu alipomfufua Mwana wake. Hatupaswi kuogopa hata wakitisha kutuua. Tukifa, Yehova atatukumbuka na kutufufua kama alivyomfufua Yesu.

Je, hatufurahi kujua kwamba Mungu anawakumbuka wanaomtumikia na kwamba atawafufua kutoka kwa wafu?— Mambo hayo yanapasa kutufanya tutake kujua namna tunavyoweza kumfurahisha Mungu. Je, unajua kwamba kwa hakika tunaweza kumfurahisha Mungu?— Tutazungumzia hayo kwenye sura inayofuata.

Imani katika ufufuo wa Yesu inapasa kuimarisha tumaini letu na imani yetu. Tafadhali soma Matendo 2:22-36; 4:18-20; na 1 Wakorintho 15:3-8, 20-23.