Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

 SURA YA 15

Jinsi ya Kuwa Mwenye Fadhili

Jinsi ya Kuwa Mwenye Fadhili

JE, UNAJUA ubaguzi ni nini?— Ubaguzi ni kuchukia mtu kwa sababu tu labda anaonekana kuwa tofauti na wewe au labda yeye ni wa kabila tofauti na lenu. Kwa hiyo kuwa na ubaguzi ni kuwa na hisia mbaya au maoni mabaya kuhusu mtu kabla ya kumjua vizuri.

Unafikiri ni sawa kumchukia mtu kabla ya kujua yeye ni mtu wa aina gani au kwa sababu tu yeye ni tofauti?— La, si vizuri kuwa na ubaguzi, na wala si tendo la fadhili. Hatupaswi kumtendea mtu vibaya eti kwa sababu tu yeye ni tofauti na sisi.

Hebu fikiria. Je, unajua mtu yeyote ambaye ana rangi tofauti na yako au wa kabila tofauti na lenu?— Labda hata unajua watu ambao wanaonekana tofauti kwa sababu waliumia au wana ugonjwa fulani. Je, unawaonyesha fadhili na upendo watu walio tofauti nawe?—

Tunapaswa tuwatendeeje wale ambao huenda wakawa tofauti na sisi?

Tukimsikiliza Mwalimu Mkuu, Yesu Kristo, tutakuwa wenye fadhili kwa kila mtu. Hatupaswi kumbagua mtu yeyote, hata awe ni wa nchi gani au rangi gani. Tunapaswa kumwonyesha fadhili. Ijapokuwa watu wote hawaamini hivyo, hilo ni somo ambalo Yesu alifundisha. Hebu tulizungumzie.

Myahudi mmoja mwenye ubaguzi alimjia Yesu na kumwuliza, ‘Nifanye nini ili nipate uzima wa milele?’ Yesu alijua kwamba labda mtu huyo anajaribu kumfanya aseme tunapaswa kuwaonyesha fadhili watu wa jamii yetu au taifa letu. Lakini badala ya  Yesu kujibu swali hilo, alimwuliza mtu huyo: ‘Sheria ya Mungu inasema tufanye nini?’

Huyo mtu akajibu: ‘Mpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote, na jirani yako kama wewe mwenyewe.’ Yesu akasema: ‘Umejibu vema. Endelea kufanya hivyo nawe utapata uzima wa milele.’

Hata hivyo, mtu huyo hakutaka kuwaonyesha fadhili au upendo watu wa jamii nyingine. Kwa hiyo akajaribu kutafuta sababu. Akamwuliza Yesu: “Ni nani kwa kweli aliye jirani yangu?” Huenda alitaka Yesu aseme: “Jirani zako ni rafiki zako,” au “Ni watu wa jamii yenu.” Ili kujibu swali hilo, Yesu alisimulia hadithi moja kuhusu Myahudi na Msamaria. Hadithi hiyo inasema hivi:

Mtu mmoja alikuwa akitembea barabarani kutoka jiji la Yerusalemu kwenda Yeriko. Mtu huyo alikuwa Myahudi. Akiwa njiani, wanyang’anyi walimshika. Wakamwangusha chini, wakachukua pesa, na nguo zake. Wakampiga na kumwacha akiwa mahututi kando ya barabara.

 Muda mfupi baadaye, kuhani akapitia barabara hiyo. Akamwona huyo mtu aliyekuwa amejeruhiwa sana. Wewe ungalifanya nini?— Kuhani huyo alipita kando ya barabara akaenda zake. Hata hakusimama. Hakujaribu hata kidogo kumsaidia mtu huyo.

Kisha mtu mwingine mwenye kushika dini sana akaja. Alikuwa Mlawi aliyetumikia hekaluni huko Yerusalemu. Je, yeye alisimama ili kumsaidia?— La. Alifanya tu kama yule kuhani.

Mwishowe, akaja Msamaria fulani. Je, unaweza kumwona kwenye kona ya barabara? Alimwona Myahudi huyo aliyejeruhiwa sana amelala pale. Tukumbuke kwamba Wasamaria na Wayahudi hawakupendana hata kidogo. (Yohana 4:9) Je, Msamaria huyo alimwacha mtu huyo  bila kumsaidia? Je, alisema: ‘Kwa nini nimsaidie huyu Myahudi? Hawezi kunisaidia nikiumia.’

Kwa nini Msamaria alikuwa jirani mwema?

Msamaria huyo alimwangalia mtu huyo aliyeanguka kando ya barabara, akamhurumia. Akaona hawezi kumwacha hapo afe. Kwa hiyo akashuka kutoka kwa punda aliyembeba, akamkaribia na kuanza kushughulikia majeraha yake. Akayatia mafuta na divai. Hii ingesaidia majeraha kupona. Kisha akayafunga kwa kitambaa.

Msamaria huyo akamwinua polepole mtu huyo aliyeumia na kumweka juu ya punda wake. Kisha wakateremka polepole mpaka kwenye hoteli ndogo. Msamaria huyo akapata mahali ambapo mtu huyo angekaa na kumtunza vizuri.

Sasa Yesu akamwuliza mtu yule aliyekuwa akizungumza naye: ‘Unafikiri ni nani kati ya hao watu watatu aliyekuwa jirani mwema?’ Ungesemaje? Je, ni yule kuhani, yule Mlawi, au ni yule Msamaria?—

Mtu huyo akajibu: ‘Yule mtu aliyesimama na kumshughulikia mtu yule aliyeumizwa ndiye jirani mwema.’ Yesu akamwambia: ‘Umesema vema. Nenda na ufanye vivyo hivyo.’ —Luka 10:25-37.

 Hiyo ni hadithi nzuri, sivyo? Inatusaidia kujua ni nani walio jirani zetu. Si rafiki zetu tu. Wala si tu watu walio na rangi kama yetu au wa kabila letu. Yesu alitufundisha kuwa wenye fadhili kwa watu hata wawe wametoka wapi, wanafanana vipi, au wanazungumza lugha gani.

Hivyo ndivyo Yehova Mungu alivyo. Yeye hana ubaguzi. Yesu alisema, ‘Baba yenu aliye mbinguni hufanya jua lake lichomoze kwa watu wabaya na wazuri, naye hufanya mvua yake inyeshe kwa watu wazuri na wabaya.’ Basi, tunapaswa kuwa wenye fadhili kwa watu wote, kama Mungu. —Mathayo 5:44-48.

Unawezaje kuwa jirani mwema?

Kwa hiyo ukiona mtu aliyeumia, utafanya nini?— Vipi ikiwa mtu huyo ni wa nchi nyingine au ni wa rangi tofauti na yenu? Yeye bado ni jirani yako, na unapaswa kumsaidia. Ikiwa unaona wewe ni mdogo sana na huwezi kumsaidia, omba msaada wa mtu mzima. Au unaweza kuita polisi au mwalimu. Kufanya hivyo ni kuonyesha fadhili kama yule Msamaria.

Mwalimu Mkuu anataka tuwe wenye fadhili. Anataka tuwasaidie wengine, bila kujali wao ni akina nani. Hiyo ndiyo sababu alisimulia hadithi ya Msamaria mwenye fadhili.

Kuhusu somo la kuwa mwenye fadhili kwa watu bila kujali wao ni wa rangi gani au nchi gani, soma Mithali 19:22; Matendo 10:34, 35; na 17:26..