WAKATI mwingine Yehova hufanya mambo kwa njia ya ajabu ili kuwalinda wale walio wachanga na wasio na uwezo wa kujilinda wenyewe. Ukitembea mashambani, utaona jinsi Yehova anavyofanya hivyo. Lakini labda mwanzoni huwezi kuelewa kinachotendeka.

Unaweza kumwona ndege anatua karibu nawe. Inaonekana ameumia. Unapojaribu kumkaribia, anakokota ubawa wake mmoja na kusonga mbali. Unapoendelea kumfuata ndege huyo, anaendelea kusonga mbali. Kisha kwa ghafula anaruka na kwenda. Ubawa wake haukuwa umeumia hata kidogo! Unajua huyo ndege alikuwa akifanya nini?—

Karibu na mahali ambapo ndege huyo alitua, alikuwa ameyaficha makinda yake kichakani. Ndege huyo alikuwa anaogopa kwamba unaweza kuyaona makinda yake na kuyaumiza. Kwa hiyo alijifanya ameumia ili uondoke. Unajua ni nani anayeweza kutulinda kama vile ndege anavyoyalinda makinda yake?— Katika Biblia, Yehova anafananishwa na ndege anayeitwa tai, ambaye husaidia makinda yake.—Kumbukumbu la Torati 32:11, 12.

Ndege huyu anayalindaje makinda yake?

 Mtoto anayependwa sana na Yehova ni Mwana wake mpendwa, Yesu. Kama Baba yake, Yesu alikuwa mtu wa roho na mwenye nguvu alipokuwa mbinguni. Yeye angeweza kujitunza. Lakini Yesu alipozaliwa kama mtoto duniani, hakuwa na nguvu. Alihitaji ulinzi.

Ili kutimiza yale Mungu alitaka afanye duniani, ilikuwa lazima Yesu akue kufikia utu uzima akiwa mkamilifu. Hata hivyo, Shetani alijaribu kumwua Yesu akiwa bado mchanga. Hadithi kuhusu jinsi Shetani alivyojaribu kumwua Yesu akiwa mtoto na jinsi Yehova alivyomlinda inasisimua sana. Je, ungependa kuisikia?—

Muda mfupi baada ya Yesu kuzaliwa, Shetani anafanya kitu kama nyota king’ae angani upande wa Mashariki. Watu wanaoitwa wanajimu, wanaochunguza nyota, wanaifuata nyota kwa kilometa mia kadhaa mpaka Yerusalemu. Walipofika waliuliza mahali atakapozaliwa yule atakayekuwa mfalme wa Wayahudi. Watu wanaojua yale ambayo Biblia husema kuhusu habari hiyo wanapoulizwa, wanajibu: “Bethlehemu.”—Mathayo 2:1-6

Baada ya wanajimu kumwona Yesu, Mungu anawapa onyo gani ambalo linamwokoa Yesu?

 Herode, mfalme mbaya wa Yerusalemu anaposikia kuhusu huyo mfalme mpya aliyezaliwa katika mji ulio karibu wa Bethlehemu, anawaambia wanajimu hivi: ‘Mtafuteni huyo mtoto mchanga, na mkiisha kumpata mniletee habari.’ Unajua ni kwa nini Herode anataka kujua mahali Yesu alipo?— Ni kwa sababu Herode ana wivu na anataka kumwua!

Mungu anamlindaje Mwana wake?— Wanajimu wanapompata Yesu, wanampa zawadi. Baadaye Mungu anawaonya katika ndoto wasirudi kwa Herode. Basi wakarudi kwao bila kurudi Yerusalemu. Herode anapogundua kwamba wanajimu wamerudi kwao, anakasirika sana. Basi ili amwue Yesu, Herode anaamuru wavulana wote chini ya umri wa miaka miwili huko Bethlehemu wauawe! Hata hivyo tayari Yesu alikuwa ameondoka.

Unajua jinsi Yesu anavyoponyoka?— Baada ya wanajimu kuanza safari ya kurudi nyumbani, Yehova anamwagiza Yosefu mumewe Maria aondoke na kukimbilia Misri. Huko, Yesu anaponyoka kuuawa na Herode mwovu. Miaka kadhaa baadaye, Maria na Yosefu wanaporudi kutoka Misri, Mungu anampa Yosefu agizo lingine. Anamwambia katika ndoto aende Nazareti, ambako Yesu angekuwa salama.—Mathayo 2:7-23.

Yesu anaokolewaje tena akiwa mchanga?

Unaona jinsi Yehova alivyomlinda Mwana wake?— Unafikiri ni nani walio kama yale makinda yaliyofichwa na mama yao kichakani au kama Yesu  alipokuwa mtoto? Je, wewe si kama wao?— Kuna watu ambao wanataka kukuumiza pia. Unajua ni akina nani?—

Biblia inasema kwamba Shetani ni kama simba angurumaye anayetaka kutumeza. Na kama vile tu simba anavyowashambulia wanyama wadogo, Shetani na roho wake waovu mara nyingi wanashambulia watoto. (1 Petro 5:8) Lakini Yehova ana nguvu kushinda Shetani. Yehova anaweza kuwalinda watoto wake au kurekebisha kitu chochote kibaya ambacho Shetani anawafanyia.

Katika Sura ya 10 ya kitabu hiki, je, unakumbuka kile ambacho Ibilisi na roho wake waovu wanajaribu kutushawishi tufanye?— Ndiyo, wanajaribu kutushawishi tufanye ngono ambayo Mungu anakataza. Lakini ni nani pekee wanaopaswa kufanya ngono?— Ni watu wazima wawili, yaani, mwanamume na mwanamke waliooana peke yao.

Hata hivyo inasikitisha kwamba watu wazima wengine wanapenda kufanya ngono na watoto. Wanapofanya hivyo, wavulana na wasichana wanaweza kuanza kufanya mambo mabaya ambayo wanajifunza kwa hao watu wazima. Pia wataanza kutumia viungo vyao vya uzazi kwa njia isiyofaa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa hapo zamani sana katika jiji la Sodoma. Biblia inasema kwamba watu wa Sodoma, ‘mvulana mpaka mzee,’ walijaribu kufanya ngono na wanaume waliomtembelea Loti.—Mwanzo 19:4, 5.

Kwa hiyo, kama vile Yesu alivyolindwa, wewe pia unahitaji kulindwa na watu wazima—hata na watoto wengine—wanaoweza kujaribu kufanya ngono nawe. Kwa kawaida watu hao watajifanya kuwa rafiki zako. Wanaweza hata kukupa zawadi ukiahidi kwamba hutawaambia wengine kuhusu tendo ambalo wanataka kufanya nawe. Lakini watu hao ni wenye ubinafsi, kama Shetani na roho wake waovu, na wanataka tu kujipatia raha. Nao wanajaribu kupata raha hiyo kwa kufanya ngono na watoto. Hili ni kosa baya sana!

 Unajua wanaweza kufanya nini ili wapate raha?— Wanaweza kujaribu kusugua-sugua viungo vyako vya uzazi. Au hata wanaweza kusugua-sugua viungo vyao vya uzazi kwenye viungo vyako. Lakini hupaswi kumwacha mtu yeyote achezee uume wako au uke wako. Usimruhusu hata ndugu yako au dada yako au mama yako au baba yako aguse viungo hivyo. Sehemu hizi za mwili wako ni za siri.

Unapaswa kusema nini na kufanya nini mtu akijaribu kukushika-shika kwa njia isiyofaa?

Unawezaje kujilinda usitendwe vibaya na watu wanaofanya mambo mabaya kama hayo?— Kwanza kabisa usimruhusu mtu yeyote achezee viungo vyako vya uzazi. Mtu yeyote akijaribu kuvichezea, sema kwa ujasiri na kwa sauti kubwa: “Niache! Naenda kukushtaki!” Naye akikuambia kwamba wewe ndiye mwenye makosa kwa lililofanyika, usimwamini. Si kweli. Nenda tu umshtaki hata akiwa nani! Unapaswa kumshtaki hata kama anasema kwamba tendo mnalofanya pamoja ni siri yenu nyinyi wawili tu. Hata kama anakuahidi zawadi nzuri au anakutisha, unapaswa kuondoka na kwenda kumshtaki.

Hatumaanishi kwamba uogope, lakini unapaswa kuwa mwangalifu sana. Wazazi wanapokuonya kuhusu watu au mahali ambapo panaweza kuwa hatari kwako, unapaswa kuwasikiliza. Ukiwasikiliza, utaepuka kuumizwa na mtu mbaya.

Soma jinsi unavyoweza kujilinda na mwenendo mbaya wa ngono katika Mwanzo 39:7-12; Mithali 4:14-16; 14:15, 16; 1 Wakorintho 6:18; na 2 Petro 2:14.