TAZAMA! meli ina taabu! Inavunjika-vunjika! Unawaona watu walioruka ndani ya maji? Wengine wamekwisha fika pwani. Yule ni Paulo? Na tujue mambo yaliyompata.

Waliookoka meli ilipovunjika

Kumbuka, Paulo amefungwa Kaisaria muda wa miaka miwili. Ndipo yeye na wafungwa wengine wanaingizwa ndani ya meli, wanaanza safari ya kwenda Roma. Wanapopita karibu na kisiwa cha Krete, wanapigwa na upepo mkubwa. Upepo huo unavuma kwa nguvu hata wanaume wanashindwa kuiongoza meli. Hawawezi hata kuliona jua mchana wala nyota usiku. Mwishowe, baada ya siku nyingi, wale walio katika meli wanakata tamaa ya kuokoka.

Ndipo Paulo anasimama na kuwaambia: ‘Hapana mtu kati yenu atakayepoteza uhai wake; meli peke yake itapotea. Maana usiku wa jana malaika wa Mungu alikuja kuniambia. “Usiogope, Paulo! Inakupasa usimame mbele ya Kaisari mtawala wa Roma. Mungu atawaokoa wote wale wanaosafiri nawe.”’

Kama saa sita za usiku hivi siku ya 14 baada ya kuanza upepo mkubwa, wafanya kazi ya meli wanajua kwamba maji yanazidi kuwa kidogo! Kwa sababu ya kuogopa kugonga miamba usiku, wanaangusha nanga zao. Kesho yake wanaona ghuba. Wanaamua kujaribu kupeleka meli huko pwani.

Basi, wanapozidi kukaribia pwani, meli inagonga mchanga na kukwama. Ndipo mawimbi nayo yanaanza kuipiga meli, inavunjika-vunjika. Mkuu wa jeshi anasema: ‘Ninyi nyote mnaoweza kuogelea jitupeni kwanza baharini mwogelee mpaka pwani. Wengine mwafuate, mshikilie vipande vya meli.’ Wanafanya hivyo. Kwa njia hiyo watu 276 waliokuwa melini wanafika pwani salama, kama malaika alivyoahidi.

Kisiwa hicho chaitwa Melita. Watu wa huko ni wenye fadhiili sana, wanawakaribisha wanaotoka melini. Wakati hali ya hewa inapokuwa nzuri zaidi, Paulo anaingizwa katika meli nyingine na kupelekwa Roma.

Matendo 27:1-44; 28:1-14.Maswali

  • Inakuwaje na meli ambayo Paulo anasafiri nayo inapopita karibu na kisiwa cha Krete?
  • Paulo anawaambia wale walio melini nini?
  • Kwa nini meli inavunjika-vunjika?
  • Mkuu wa jeshi anatoa maagizo gani, na watu wangapi wanafika kisiwani salama?
  • Kisiwa hicho kinaitwaje, na ni jambo gani linalompata Paulo hali ya hewa inapokuwa nzuri?

Maswali ya ziada