Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia

Hadithi ya 101: Yesu Anauawa

Hadithi ya 101: Yesu Anauawa

TAZAMA ubaya unaotokea! Yesu anauawa. Wamemtundika juu ya mti. Misumari imepigiliwa katika mikono na miguu yake. Kwa nini wanataka kumfanya Yesu hivyo?

Yesu akifa

Ni kwa sababu watu wengine wanamchukia Yesu. Unawajua? Mmoja wao ni malaika mbaya Shetani Ibilisi. Ndiye aliyeongoza Adamu na Hawa wasimtii Yehova. Shetani ndiye aliyeongoza adui za Yesu wafanye ubaya huo mkubwa.

Hata kabla ya Yesu kupigiliwa misumari kwenye mti, adui zake wanamtendea mabaya. Unakumbuka walivyokwenda kwenye bustani ya Geth·semane wakamkamata? Adui hao walikuwa nani? Viongozi wa dini. Na tuone yanayotokea baadaye.

Yesu anapokamatwa na viongozi wa dini, mitume wake wanakimbia. Wanamwacha Yesu peke yake akiwa na adui zake, kwa sababu wanaogopa. Lakini Petro na Yohana hawaendi mbali. Wanafuata waone linalompata Yesu.

Makuhani hao wanampeleka Yesu kwa mzee Anasi, aliyekuwa kuhani mkuu zamani. Kundi hilo halikawii huko. Kisha wanampeleka Yesu nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu wa sasa. Viongozi wengi wa dini wanakusanyika katika nyumba yake.

Hapo nyumbani pa Kayafa wanafanya hukumu. Watu wanaletwa ili waseme uongo juu ya Yesu. Viongozi wote wa dini wanasema: ‘Imempasa Yesu auawe.’ Ndipo wanamtemea mate usoni pake, na kumpiga ngumi.

Hayo yote yanapoendelea, Petro yuko nje ya ua. Ni usiku wenye baridi, basi watu wanawasha moto. Wanapootoa moto, mtumishi mmoja wa kike amtazama Petro, na kusema: ‘Huyu pia alikuwa pamoja na Yesu.’

‘Hapana!’ Petro ajibu.

Mara tatu watu wanamwambia Petro kwamba alikuwa pamoja na Yesu. Lakini kila mara Petro anakataa. Mara ile ya tatu Petro anaposema hivyo, Yesu anageuka na kumtazama. Petro anasikitika sana kwa kusema uongo. Anatoka nje na kuanza kulia.

Kunapoanza kupambazuka Ijumaa asubuhi, makuhani wanampeleka kwenye Baraza yao kuu. Wanazungumza huko jambo watakalomfanyia. Wanampeleka kwa Pontio Pilato, mtawala wa wilaya ya Yudea.

‘Huyu ni mtu mbaya,’ makuhani wanamwambia Pilato. ‘Imempasa kuuawa.’ Akiisha kumwuliza Yesu, Pilato anasema: ‘Sioni kosa lake.’ Ndipo anampeleka Yesu kwa Herode Antipa. Herode ndiye mtawala wa Galilaya, lakini anakaa Yerusalemu. Wala Herode haoni kosa la Yesu, basi anamrudisha kwa Pilato.

Pilato anataka kumfungua Yesu. Adui za Yesu wanataka mfungwa mwingine afunguliwe. Huyo ni mwivi Baraba. Sasa inakaribia kuwa mchana Pilato anapomtoa Yesu nje. Anawaambia watu hivi: ‘Tazameni! Mfalme wenu!’ Lakini makuhani wakuu wanapiga yowe hivi: ‘Mwondoe! Mwue! Mwue!’ Basi Pilato anafungua Baraba, nao wanamchukua Yesu akauawe.

Mapema alasiri ya Ijumaa Yesu anapigiliwa misumari juu ya mti. Wakosaji wawili wanatundikwa kila upande wa Yesu. Upesi kabla ya Yesu kufa, mmoja wa wakosaji hao anamwambia hivi: ‘Unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.’ Naye Yesu amjibu: ‘Nakuahidi kwamba utakuwa nami katika Paradiso.’

Je! hiyo si ahadi ya maana sana? Unajua paradiso hiyo anayoisema Yesu? Ile paradiso aliyofanya Mungu mwanzoni ilikuwa wapi? Duniani. Yesu atakapotawala mbinguni, atamfufua mtu huyo afurahie Paradiso mpya duniani. Hatuwezi kufurahia hilo?

Mathayo 26:57-75; 27:1-50; Luka 22:54-71; 23:1-49; Yohana 18:12-40; 19:1-30.Maswali

  • Ni nani hasa anayepaswa kulaumiwa kwa kifo cha Yesu?
  • Mitume wanafanya nini Yesu anapokamatwa na viongozi wa dini?
  • Ni jambo gani linalotukia katika nyumba ya kuhani mkuu Kayafa?
  • Kwa nini Petro alitoka nje na kulia?
  • Baada ya Yesu kurudishwa kwa Pilato, makuhani wakuu wanasema nini kwa sauti kubwa?
  • Yesu anafanywa nini mapema alasiri siku ya Ijumaa, naye anamwahidi nini mkosaji aliyetundikwa mtini kando yake?
  • Paradiso ambayo Yesu aliahidi itakuwa wapi?

Maswali ya ziada