Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia

Hadithi ya 80: Watu wa Mungu Wanatoka Babeli

Hadithi ya 80: Watu wa Mungu Wanatoka Babeli

KARIBU miaka miwili imepita tangu Babeli ulipotekwa na Wamedi na Waajemi. Sasa tazama yanayotokea! Ndiyo, Waisraeli wanatoka Babeli. Walikombolewa namna gani? Nani aliwakomboa?

Ni Koreshi (Kiro), mfalme wa Ajemi. Zamani kabla Koreshi hajazaliwa, Isaya, nabii wa Yehova, aliandika hivi: ‘Utafanya mapenzi yangu. Malango yatakuwa wazi kwa ajili yako uuteke mji.’ Naye Koreshi akaongoza katika kuuteka Babeli. Wamedi na Waajemi waliingia mjini usiku kupitia malango yaliyokuwa yameachwa wazi.

Lakini Isaya nabii wa Yehova alisema pia kwamba Koreshi angeamuru Yerusalemu na hekalu lake vijengwe tena. Je! Koreshi alitoa amri hiyo? Ndiyo. Hivi ndivyo Koreshi anawaambia Waisraeli: ‘Nendeni, sasa, Yerusalemu, mkajenge hekalu la Yehova, Mungu wenu.’ Waisraeli hawa sasa wanakwenda kufanya hivyo.

Waisraeli wakiondoka Babiloni

Lakini Waisraeli wote katika Babeli hawawezi kwenda safari ndefu Yerusalemu. Ni safari ndefu sana ya karibu kilomita 800 na wengi ni wazee au wagonjwa mno. Tena kuna sababu nyingine zinazowafanya wengine wasiende. Lakini Koreshi anawaambia wale wasiokwenda: ‘Wapeni fedha na dhahabu na zawadi nyingine wale wanaokwenda kujenga Yerusalemu na hekalu lake.’

Basi, Waisraeli hao wanaokwenda Yerusalemu wanapewa zawadi nyingi. Pia, Koreshi anawapa mabakuli na vikombe ambavyo Mfalme Nebukadreza alikuwa amechukua katika hekalu la Yehova wakati alipoharibu Yerusalemu. Watu hao wanakuwa na vitu vingi vya kuchukua.

Baada ya kusafiri miezi kama minne hivi, Waisraeli wanafika Yerusalemu kwa wakati barabara. Sasa ni miaka 70 tangu mji huo ulipoharibiwa, nayo nchi iliachwa utupu kabisa bila watu. Lakini ijapo sasa Waisraeli wameirudia nchi yao, watapata taabu, kama tutakavyojifunza halafu.

Isaya 44:28; 45:1-4; Ezra 1:1-11.Maswali

  • Kama picha inavyoonyesha, Waisraeli wanafanya nini?
  • Koreshi alitimizaje unabii wa Yehova uliotolewa na Isaya?
  • Koreshi anawaambia Waisraeli wasioweza kurudi Yerusalemu nini?
  • Koreshi anawapa watu vitu gani ili wavirudishe Yerusalemu?
  • Inawachukua Waisraeli muda gani kurudi Yerusalemu?
  • Ni miaka mingapi ambayo imepita tangu nchi ilipoachwa bila watu?

Maswali ya ziada