Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia

Hadithi ya 79: Danieli Katika Shimo la Simba

Hadithi ya 79: Danieli Katika Shimo la Simba

LO! LO! Ni kama Danieli ana taabu sana. Lakini wale simba hawamwumi! Unajua sababu? Nani aliyemweka Danieli katikati ya simba hawa wote? Na tuone.

Sasa mfalme wa Babeli ni Dario. Anampenda Danieli sana kwa sababu ni mwema na mwenye akili. Dario anamchagua Danieli awe mtawala mkuu katika ufalme wake. Hilo linawafanya watu wengine katika ufalme wamwonee wivu Daniele. Basi wanafanya hivi.

Dario

Wanamwendea Dario na kusema: ‘Tumekubaliana, Ee mfalme, utunge sheria kwamba kwa siku 30 mtu ye yote asiombe mungu ye yote wala mwanadamu ila wewe, Ee mfalme. Mtu akikataa kutii, atupwe kwenye simba.’ Dario hajui sababu watu hawa wanataka sheria hiyo itungwe. Lakini anaona inafaa, basi anaandikisha sheria hiyo. Sasa sheria hiyo haiwezi kubadilishwa.

Danieli anapopata habari ya sheria hiyo anaenda kwake na kusali, kama kawaida. Watu hao wabaya walijua Danieli hangeacha kumwomba Yehova. Wanafurahi, kwa sababu inaonekana mpango wao wa kumwondoa Danieli una matokeo.

Mfalme Dario anapojua kwa nini watu hao walitaka sheria hiyo itungwe, anasikitika sana. Lakini hawezi kuibadili sheria. Hivyo anaamuru Danieli atupwe katika shimo la simba.

Dario anahangaika hata anakosa usingizi usiku huo. Kesho yake anakwenda mbio kwenye shimo la simba. Unaweza kumwona pale. Anapaza sauti: ‘Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai! Je! Mungu unayetumikia amekuokoa usiliwe na simba hao?’

Danieli katika shimo la simba

‘Mungu alimtuma malaika wake,’ Danieli ajibu, ‘akafunga vinywa vya simba wasiniume.’

Mfalme anafurahi sana. Anaamuru Danieli atolewe katika shimo. Ndipo anaamuru wale watu wabaya waliotaka kumwondoa Danieli watupwe kwenye simba. Hata kabla ya kufika chini ya shimo, simba hao wanawakamata na kuvunja-vunja mifupa yao.

Kisha mfalme Dario anaandikia watu wote katika ufalme wake hivi: ‘Naamuru kila mtu aheshimu Mungu wa Danieli. Yeye anafanya miujiza mikubwa. Alimwokoa Danieli asiliwe na simba.’

Danieli 6:1-28.Maswali

  • Dario ni nani, naye anamwonaje Danieli?
  • Watu fulani wenye wivu wanamshawishi Dario afanye nini?
  • Danieli anafanya nini anaposikia kuhusu ile sheria mpya?
  • Kwa nini Dario ana wasiwasi sana hivi kwamba anakosa usingizi, na anafanya nini asubuhi inayofuata?
  • Danieli anamjibuje Dario?
  • Inakuwaje kwa wale watu wabaya waliojaribu kumwua Danieli, na Dario anawaandikia watu wote katika ufalme wake barua kuhusu nini?

Maswali ya ziada