Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia

Hadithi ya 59: Sababu Yampasa Daudi Akimbie

Hadithi ya 59: Sababu Yampasa Daudi Akimbie

BAADA ya Daudi kumwua Goliathi, Abneri mkuu wa jeshi anampeleka kwa Sauli. Sauli anapendezwa sana na Daudi. Anamfanya mkuu katika jeshi lake na kumchukua akakae katika nyumba ya mfalme.

Baadaye, jeshi linaporudi kupigana na Wafilisti, wanawake wanaimba hivi: ‘Sauli ameua maelfu, lakini Daudi makumi ya maelfu.’ Hilo lamfanya Sauli aone wivu, kwa sababu Daudi anaheshimiwa kuliko Sauli. Lakini Yonathani mwana wa Sauli haoni wivu. Anampenda Daudi sana, naye Daudi anampenda Yonathani pia. Hao wawili wanapeana ahadi kwamba watakuwa rafiki sikuzote.

Mfale Sauli akitupa mkuki

Daudi anajua sana kupiga kinubi, naye Sauli anapenda muziki anaopiga Daudi. Lakini siku moja wivu wa Sauli wamfanya atende jambo baya. Wakati Daudi anapopiga kinubi, Sauli anachukua mkuki wake na kuutupa, akisema: ‘Nitampigilia Daudi ukutani!’ Lakini Daudi apiga chenga (aepa), na mkuki wamkosa. Baadaye Sauli akosa tena kumpiga Daudi kwa mkuki wake. Basi Daudi anajua yampasa awe mwangalifu sana.

Unajua ahadi ya Sauli! Alisema angetoa binti yake awe mke wa yule mtu ambaye angeua Goliathi. Mwishowe Sauli anamwambia Daudi achukue Mikali binti yake, lakini kwanza yampasa aue Wafilisti adui 100. Ebu wazia hilo! Sauli anatumaini kwamba Wafilisti watamwua Daudi. Lakini hawamwui, hivyo Sauli anampa Daudi binti yake awe mke wake.

Siku moja Sauli anamwambia Yonathani na watumishi wake wote kwamba anataka kumwua Daudi. Lakini Yonathani anamwambia babaye hivi: ‘Usimwumize Daudi. Hajakukosea. Kila alichofanya kimekuwa msaada mkubwa kwako. Aliweka uhai wake katika hatari alipomwua Goliathi, na ulipoona, ukafurahi.’

Daudi akiukwepa mkuki

Sauli amsikiliza mwanawe, na kuahidi asimwumize Daudi. Daudi anarudishwa, naye anamtumikia Sauli tena nyumbani mwake kama zamani. Lakini, siku moja wakati Daudi anapopiga muziki, Sauli anamtupia Daudi mkuki wake tena. Daudi apiga chenga, mkuki unapiga ukuta. Hii ndiyo mara ya tatu! Sasa Daudi ajua yampasa akimbie!

Usiku huo Daudi aenda nyumbani kwake. Lakini Sauli anatuma watu fulani wakamwue. Mikali anajua mipango ya baba yake. Anamwambia mume wake hivi: ‘Usipoondoka usiku huu, kesho utakuwa umekufa.’ Inampasa Daudi ajifiche hapa na pale muda wa karibu miaka saba, Sauli asimwone.

1 Samweli 18:1-30; 19:1-18.Maswali

  • Kwa nini Sauli anamwonea Daudi wivu, lakini Yonathani, mwana wa Sauli, ni tofauti kwa njia gani?
  • Ni jambo gani linalotukia siku moja Daudi anapompigia Sauli kinubi?
  • Sauli anamwambia Daudi ni lazima afanye nini kabla ya kumwoa binti yake Mikali, na kwa nini Sauli anamwambia jambo hilo?
  • Daudi anapompigia Sauli kinubi, ni nini kinachotukia kwa mara ya tatu, kama picha inavyoonyesha?
  • Mikali anasaidiaje kumwokoa Daudi, na Daudi analazimika kufanya nini kwa miaka saba?

Maswali ya ziada

Pata Kujua Mengi Zaidi

VIDEO

Daudi—Alimtegemea Mungu

Daudi alifanya makosa maishani mwake na akakabili matatizo mengi, lakini hakuacha kamwe kumtumikia Mungu. Mfano wake mzuri unaweza kukusaidia uendelee kuwa mshikamanifu.