Samweli akimtia mafuta Sauli awe mfalme

MTAZAME Samweli anamwaga mafuta kichwani pa mtu. Ndivyo walivyokuwa wakimfanyia mtu waonyeshe amechaguliwa kuwa mfalme. Yehova anamwambia Samweli amwage mafuta kichwani pa Sauli (Saulo). Ni mafuta ya pekee yenye harufu nzuri.

Sauli hakudhani alifaa kuwa mfalme. ‘Mimi ni wa kabila la Benyamini, dogo zaidi katika Israeli,’ anamwambia Samweli. ‘Kwa nini wasema nitakuwa mfalme?’ Yehova anampenda Sauli kwa sababu hana kiburi. Ndiyo maana anamchagua kuwa mfalme.

Lakini Sauli si maskini wala mtu mdogo. Anatokana na jamaa tajiri, naye ana sura nzuri sana, mwanamume mrefu. Ni mrefu kuliko mtu ye yote katika Israeli! Sauli ni mwenye mbio sana kuliko watu wote, na mwenye nguvu sana. Watu wanafurahi kwa vile Yehova amemchagua Sauli awe mfalme. Wote wanaanza kupiga kelele hivi: ‘Uishi maisha marefu mfalme!’

Adui za Israeli ni wenye nguvu kama kawaida. Bado wanawafanyia Waisraeli matata mengi. Upesi baada ya Sauli kufanywa mfalme, Waamoni wanakuja kupigana nao. Lakini Sauli anakusanya jeshi kubwa, anashinda Waamoni. Jambo hilo linafurahisha watu kwa vile Sauli ni mfalme.

Wakati kunapita miaka, Sauli anaongoza Waisraeli kwenye ushindi mwingi juu ya adui zao. Sauli pia anapata mwana hodari jina lake Yonathani (Yonatana). Yonathani naye anasaidia Waisraeli kushinda vita vingi. Bado Wafilisti ni adui wabaya zaidi wa Israeli. Siku moja maelfu na maelfu ya Wafilisti wanakuja wapigane na Waisraeli.

Samweli anamwambia Sauli amngojee ndipo amtolee Yehova zawadi. Lakini Samweli anakawia kuja. Sauli anaogopa kwamba Wafilisti wataanza vita, basi anaanza peke yake kutoa dhabihu. Kisha Samweli anapokuja, anamwambia Sauli kwamba amekosa kutii. ‘Yehova atachagua mtu mwingine awe mfalme juu ya Israeli,’ asema Samweli.

Baadaye Sauli akosa kutii tena. Basi Samweli anamwambia: ‘Ni bora kutii Yehova kuliko kumtolea zawadi ya kondoo bora zaidi. Kwa kuwa hukumtii Yehova, Yehova atakuondoa usiwe mfalme wa Israeli.’

Twaweza kujifunza somo zuri kutokana na hayo. Yanatuonyesha ubora wa kumtii Yehova sikuzote. Pia, yanaonyesha kwamba mtu mzuri kama Sauli, anaweza kuwa mbaya. Sisi hatutaki hata kidogo tuwe wabaya, sivyo?

1 Samweli sura za 9 mpaka 11; 13:5-14; 14:47-52; 15:1-35; 2 Samweli 1:23.Maswali

  • Samweli anafanya nini katika picha, na kwa nini?
  • Kwa nini Yehova anampenda Sauli, na Sauli ni mtu wa aina gani?
  • Mwana wa Sauli anaitwa nani, na mwana huyo anafanya nini?
  • Kwa nini Sauli anatoa dhabihu badala ya kumngoja Samweli aitoe?
  • Tunajifunza nini kutokana na masimulizi juu ya Sauli?

Maswali ya ziada