Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia

Hadithi ya 32: Mapigo 10

Hadithi ya 32: Mapigo 10

TAZAMA picha hizi. Kila moja inaonyesha pigo ambalo Yehova alileta juu ya Misri. Katika picha ya kwanza unaweza kumwona Harui akiupiga Mto Nailo kwa fimbo yake. Alipoupiga, maji ya mto yakawa damu. Samaki wakafa, nao mto ukaanza kunuka vibaya.

Mapigo dhidi ya Wamisri

Kisha, Yehova akafanya vyura watoke katika Mto Nailo. Walikuwa mahali pote—katika majiko ya kuokea mikate, vikaangio, katika vitanda vya watu—mahali pote. Vyura hao walipokufa Wamisri waliwakusanya wengi sana, na nchi ikanuka vibaya.

Halafu Haruni akaipiga ardhi kwa fimbo yake, nayo mavumbi yakawa chawa. Hao ni wadudu wadogo wanaouma. Chawa walikuwa pigo la tatu juu ya nchi ya Misri.

Mapigo mengine yaliumiza Wamisri peke yao, si Waisraeli. Pigo la nne lilikuwa mainzi wakubwa waliojaa katika nyumba za Wamisri wote. Pigo la tano lilikuwa juu ya wanyama. Ng’ombe na kondoo na mbuzi wengi wa Wamisri wakafa.

Kisha, Musa na Harui wakachukua majivu na kuyatupa angani. Yakawa vidonda vibaya juu ya watu na wanyama. Hilo lilikuwa pigo la sita.

Baada ya hapo Musa akainua mkono wake kuelekea angani, naye Yehova akapeleka ngurumo na mvua ya mawe. Ilikuwa mvua ya mawe iliyo mbaya zaidi kuipiga Misri.

Pigo la nane lilikuwa kundi la nzige. Nzige hao wengi sana hawakuwa wameonekana kabla ya hapo wala baadaye. Walikula kila kitu ambacho mvua ya mawe haikuharibu.

Pigo la tisa lilikuwa giza. Kwa muda wa siku tatu giza zito liliifunika nchi, lakini Waisraeli wakawa na nuru katika makao yao.

Mwishowe Mungu akawaambia watu wake wapake damu ya mwana-mbuzi au mwana-kondoo juu ya milango yao. Kisha malaika wa Mungu akapita juu ya Misri. Malaika huyo alipoiona damu, hakuua mtu ye yote katika nyumba hiyo. Lakini katika nyumba zote ambazo damu haikupakwa juu ya milango, malaika wa Mungu aliua wazaliwa wa kwanza wa wanadamu na wa wanyama. Hilo lilikuwa pigo la 10.

Baada ya pigo hilo, Farao akawaambia Waisraeli waondoke. Watu wa Mungu wote walikuwa tayari kwenda, na usiku uo huo wakaanza kutoka Misri.

Kutoka sura ya 7 hadi 12.Maswali

  • Itazame picha, na ueleze mapigo matatu ya kwanza ambayo Yehova alileta juu ya Misri.
  • Mapigo matatu ya kwanza yalitofautianaje na yale mapigo mengine?
  • Eleza pigo la nne, la tano, na la sita.
  • Eleza pigo la saba, la nane, na la tisa.
  • Yehova aliwaambia Waisraeli wafanye nini kabla ya pigo la kumi?
  • Pigo la kumi lilikuwa nini, na ni jambo gani lililotukia baada ya pigo hilo?

Maswali ya ziada

Pata Kujua Mengi Zaidi

MIRADI YA IBADA YA FAMILIA

Mungu Amtuma Musa Nchini Misri

Musa na Haruni walikuwa wajasiri walipokuwa wakizungumza na Farao. Pakueni mazoezi haya na myazungumzie pamoja mkiwa familia.