Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia

Hadithi ya 15: Mke wa Lutu Alitazama Nyuma

Hadithi ya 15: Mke wa Lutu Alitazama Nyuma

LUTU na jamaa yake walikaa Kanaani pamoja na Ibrahimu. Siku moja Ibrahimu alimwambia Lutu hivi: ‘Hapa hapana nchi ya kufaa wanyama wetu wote. Tafadhali, tutengane. Ukienda huku, na mimi nitakwenda kule.’

Lutu akaitazama nchi. Akaona sehemu ya nchi iliyo nzuri sana yenye maji na majani mazuri mengi ya wanyama wake. Hiyo ilikuwa Wilaya ya Yordani. Basi Lutu alipeleka jamaa yake na wanyama huko. Mwishowe wakakaa katika mji wa Sodoma.

Watu wa Sodoma walikuwa wabaya sana. Lutu alisumbuliwa, maana alikuwa mtu mzuri. Hata Mungu alisumbuliwa. Mwishowe, Mungu alituma malaika wawili wakamwonye Lutu kwamba Mungu ataharibu Sodoma, na Gomora mji wa karibu, maana ni miji mibaya.

Malaika hao wakamwambia Lutu hivi: ‘Fanya haraka! Chukua mke wako na binti zako wawili mwondoke huku!’ Malaika mmoja alisema: ‘Kimbieni mponye uhai wenu! Msitazame nyuma. Kimbieni kwenye milima msiuawe.’

Lutu na binti zake walitii, wakatoka Sodoma. Lakini mke wa Lutu hakutii. Walipokwisha kutembea mwendo fulani kutoka Sodoma, mke alisimama akatazama nyuma, akawa nguzo ya chumvi. Unaweza kumwona katika picha?

Tunaweza kujifunza somo zuri kwa hayo. Yanatuonyesha kwamba Mungu anaokoa wale wanaomtii, lakini wale wasiomtii watapoteza uhai wao.

Mwanzo 13:5-13; 18:20-33; 19:1-29; Luka 17:28-32; 2 Petro 2:6-8.

Lutu akikimbia Sodoma


Maswali

  • Kwa nini Ibrahimu na Lutu walitengana?
  • Kwa nini Lutu alichagua kuishi Sodoma?
  • Watu wa Sodoma walikuwa wenye sifa zipi?
  • Malaika wawili walimwonya Lutu juu ya jambo gani?
  • Kwa nini mke wa Lutu akawa nguzo ya chumvi?
  • Tunaweza kujifunza somo gani kutokana na kisa cha mke wa Lutu?

Maswali ya ziada