UNAWEZA kuona Ibrahimu anafanya nini hapa? Ana kisu, ni kama anataka kumwua mwanawe. Kwa nini afanye hivyo? Na tuone kwanza namna Ibrahimu na Sara walivyopata mwana wao.

Ibrahimu akimtoa Isaka

Kumbuka, Mungu aliwaahidi kwamba wangezaa mwana. Lakini lilikuwa jambo gumu, kwa sababu Ibrahimu na Sara walikuwa wazee sana. Lakini Ibrahimu aliamini kwamba Mungu anaweza kufanya jambo gumu. Basi jambo gani lilitokea?

Mungu alipokwisha kutoa ahadi yake, mwaka mzima ukapita. Ndipo, Ibrahimu alipokuwa mwenye miaka 100 na Sara 90, wakazaa mtoto wa kiume jina lake Isaka. Mungu alikuwa ametimiza ahadi yake!

Lakini Isaka alipokuwa mtu mzima, Yehova alijaribu imani ya Ibrahimu. Akasema: ‘Mchukue mwana wako Isaka uende kwenye mlima ambao nitakuonyesha. Ukamwue huko mwana wako umtoe dhabihu.’ Lakini kumbuka, Mungu alikuwa ameahidi kwamba watoto wa Ibrahimu wangekaa Kanaani. Ingekuwa namna gani kama Isaka angekufa? Ibrahimu hakufahamu hilo, lakini alimtii Mungu.

Alipofika kwenye mlima, Ibrahimu alimfunga Isaka na kumweka juu ya madhabahu aliyojenga. Lakini alipotaka kumwua Isaka, malaika wa Mungu alitoa sauti kubwa: ‘Ibrahimu, usimwumize mtoto wala kumfanya lolote. Sasa najua kwamba unaniamini, kwa sababu hukuninyima mwana wako mmoja tu!’

Lo! Ibrahimu alimwamini Mungu sana! Aliamini kwamba hakuna jambo gumu kwa Yehova, hata angemfufua Isaka katika wafu. Lakini Mungu hakutaka Ibrahimu amwue Isaka. Basi Mungu aliongoza kondoo akamatwe na miti midogo iliyokuwa karibu. Kisha akamwambia Ibrahimu amtoe kondoo huyo awe dhabihu mahali pa mwana wake.

Mwanzo 21:1-7; 22:1-18.Maswali

  • Mungu alimwahidi Ibrahimu nini, na alitimizaje ahadi hiyo?
  • Mungu alijaribu imani ya Ibrahimu jinsi gani, kama picha inavyoonyesha?
  • Ibrahimu alifanya nini, ijapokuwa hakuelewa kwa nini Mungu alimwamuru kufanya jambo hilo?
  • Ni nini kilichotukia Ibrahimu alipochomoa kisu ili amwue mwanawe?
  • Imani ya Ibrahimu ilikuwa yenye nguvu kadiri gani?
  • Mungu alimwandalia Ibrahimu nini ili atoe dhabihu, na vipi?

Maswali ya ziada