Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia

Hadithi ya 12: Watu Wanajenga Mnara Mkubwa

Hadithi ya 12: Watu Wanajenga Mnara Mkubwa

IKAPITA miaka mingi. Wana wa Nuhu wakazaa watoto wengi. Watoto wao walikua na kuzaa watoto zaidi. Upesi kukawa na watu wengi duniani.

Mmoja wa watu hao alikuwa kijukuu wa Nuhu jina lake Nimrodi. Alikuwa mtu mbaya aliyewinda na kuua wanyama na hata wanadamu. Nimrodi pia alijifanya mfalme atawale watu wengine. Mungu hakumpenda Nimrodi.

Wakati huo watu wote walisema lugha moja. Nimrodi alitaka awakusanye wote ili awatawale. Unajua alilofanya? Aliwaambia watu wajenge mji na ndani yake mnara mkubwa. Watazame katika picha hii wakitengeneza matofali.

Yehova Mungu hakupendezwa na jengo hilo. Mungu alitaka watu watawanyike na kukaa pote duniani. Lakini wao walisema: ‘Njoni! Tujenge mji na mnara mrefu sana ufike mbinguni. Ndipo tutasifiwa sana!’ Watu hao walitaka wajiheshimu kuliko Mungu.

Kwa hiyo Mungu aliwaachisha kujenga mnara. Unajua namna alivyofanya? Aliwafanya waanze kusema lugha mbalimbali mara moja. Wajenzi hao hawakufahamiana tena. Ndiyo sababu mji wao ukaitwa Babeli, au Babiloni, maana yake “Mchafuko.”

Basi watu hao walianza kuondoka Babeli. Vikundi vya watu waliosema lugha moja vilikwenda kukaa pamoja sehemu nyingine za dunia.

Mwanzo 10:1, 8-10; 11:1-9.

Wajenzi wakijenga mnara mkubwa


Maswali

  • Nimrodi alikuwa nani, na Mungu alimwonaje?
  • Kwa nini watu walikuwa wakitengeneza matofali, kama unavyoona katika picha?
  • Kwa nini Yehova hakupendezwa na ujenzi huo?
  • Yehova alisimamishaje ujenzi huo wa mnara?
  • Mji huo uliitwaje, na jina hilo linamaanisha nini?
  • Watu walifanya nini baada ya Yehova kuvuruga lugha zao?

Maswali ya ziada