TAZAMA dunia hii! Kila kitu ni kizuri sana! Tazama majani na miti, maua na wanyama wote. Unaweza kumjua tembo na simba hapa?

Wanyama katika bustani ya Edeni

Bustani hii nzuri ilitokea namna gani? Na tuone Mungu alivyotuwekea dunia tayari.

Kwanza, Mungu aliumba majani mabichi yaifunike nchi. Alifanya namna zote za mimea na miti midogo. Mimea hiyo inapamba dunia. Zaidi ya hivyo, mimea mingi inatupa chakula kitamu sana.

Tena Mungu aliumba samaki waogelee katika maji na ndege waruke katika anga. Aliumba mbwa na paka na farasi; wanyama wakubwa na wadogo. Ni wanyama gani wanaokaa karibu na nyumba yenu? Je! si vizuri kufurahi kwa vile Mungu alitufanyia vyote hivyo?

Halafu, Mungu alifanya sehemu moja ya dunia kuwa ya pekee sana. Aliiita bustani ya Edeni. Ilikuwa nzuri sana. Kila kitu ndani kilikuwa kizuri. Mungu alitaka dunia nzima iwe kama bustani nzuri hii.

Lakini tazama tena picha hii ya bustani. Je! unajua kitu ambacho Mungu aliona hakipo? Tuone.

Mwanzo 1:11-25; 2:8, 9.Maswali

 • Mungu alitayarishaje dunia kuwa makao yetu?
 • Mungu aliwaumba wanyama gani mbalimbali? (Ona picha.)
 • Kwa nini bustani ya Edeni ilikuwa ya kipekee?
 • Mungu alitaka dunia nzima iwe nini hatimaye?

Maswali ya ziada

 • Soma Mwanzo 1:11-25.

  Mungu aliumba nini katika siku ya tatu ya uumbaji? (Mwa. 1:12)

  Ni jambo gani lililotokea katika siku ya nne ya uumbaji? (Mwa. 1:16)

  Mungu aliwaumba wanyama wa aina gani katika siku ya tano na siku ya sita? (Mwa. 1:20, 2125)

 • Soma Mwanzo 2:8, 9.

  Mungu aliweka miti miwili gani ya kipekee katika bustani, nayo iliwakilisha nini?