NJE ya safina, watu walikaa kama zamani. Bado hawakuamini kwamba Gharika ingekuja. Walicheka wee, wakacheka sana. Lakini upesi waliacha kucheka.

Watu na wanyama wenye woga wakiwa wamezingirwa na maji ya gharika

Mara moja maji yakaanza kuanguka. Yalimwagika kutoka angani kama vile unapomwaga maji kutoka ndoo. Nuhu alikuwa amesema kweli! Lakini sasa ilikuwa kuchelewa mno ye yote kuingia katika safina. Yehova alikuwa amefunga mlango sana.

Upesi mabonde yote yakafunikwa. Maji yakawa kama mito mikubwa. Yakaangusha miti na kupindua-pindua mawe makubwa, na kufanya kelele nyingi. Watu waliogopa. Wakapanda sehemu zilizoinuka zaidi. Afadhali wangemsikiliza Nuhu na kuingia katika safina mlango ulipokuwa bado kufungwa! Lakini sasa walichelewa mno.

Maji yakazidi kupanda juu sana. Siku 40 mchana na usiku maji yalimwagika kutoka angani. Yalifika hata kwenye vilele vya milima. Upesi hata vilele vya milima mirefu zaidi vilifunikwa kwa maji. Kama Mungu alivyokuwa amesema, watu na wanyama wote waliokuwa nje ya safina wakafa. Lakini kila aliyekuwa ndani alikuwa salama.

Nuhu na wanawe walikuwa wamefanya kazi nzuri ya kujenga safina. Maji yaliinua safina juu, ikaelea juu ya maji. Kisha siku moja, mvua ilipoacha kunya, jua lilianza kung’aa. Lo! maono gani! Kila mahali palikuwa bahari kuu moja. Safina peke yake ndiyo ilionekana ikielea juu ya maji.

Safina ikielea juu ya maji

Wale watu wakubwa mno walipotea. Hawakuonekana tena waumize watu. Wote pamoja na mama zao na watu wengine wabaya, walikuwa wamekufa. Namna gani baba zao?

Baba zao hawakuwa wanadamu kama sisi. Ni malaika waliokuwa wameshuka wakae duniani. Basi Gharika ilipokuja, hawakufa pamoja na watu wengine. Walivua miili ya kibinadamu wakarudi mbinguni wakiwa malaika. Lakini hawakuruhusiwa tena katika jamaa ya malaika wa Mungu. Wakawa malaika wa Shetani. Katika Biblia wanaitwa mashetani.

Basi Mungu alileta upepo, nayo maji ya Gharika yakaanza kupunguka. Miezi mitano ilipopita, safina hiyo ilisimama juu ya mlima. Zilipopita siku nyingi zaidi, wale waliokuwa katika safina walitazama nje wakaona vilele vya milima. Maji hayo yakazidi kupunguka.

Kisha Nuhu akamtoa kunguru katika safina. Kwa sababu hakuona mahali pa kusimama, alikuwa akiruka-ruka akienda na kurudi. Alizidi kufanya hivyo akirudi kila wakati, akisimama juu ya safina.

Njiwa

Nuhu alitaka kuona kama maji yamekauka duniani. Basi baada ya hapo alimtoa njiwa kutoka safina. Lakini njiwa huyo pia alirudi kwa sababu hakuona mahali pa kukaa. Nuhu alimtuma tena mara ya pili, akarudi akiwa na jani la mzeituni katika mdomo wake. Ndipo Nuhu alijua kwamba maji hayo yamekauka. Kisha Nuhu alimtuma tena njiwa mara ya tatu, mwishowe aliona mahali pakavu pa kukaa.

Ndipo Mungu akasema na Nuhu. Akamwambia: ‘Toka katika safina. Chukua jamaa yako yote na wanyama.’ Walikuwa wamekaa ndani ya safina muda wa zaidi ya mwaka mmoja. Tunafikiri wote walifurahi sana kutoka nje tena wakiwa hai!

Mwanzo 7:10-24; 8:1-17; 1 Petro 3:19, 20.Maswali

  • Kwa nini hakuna mtu yeyote aliyeweza kuingia ndani ya safina baada ya mvua kuanza kunyesha?
  • Yehova alifanya mvua inyeshe kwa siku na usiku ngapi, na maji yalifika mpaka wapi?
  • Ilikuwaje na safina maji yalipoanza kujaa duniani?
  • Je, wale watu wakubwa mno waliokoka Gharika, na vipi baba zao?
  • Safina ilikuwa wapi baada ya miezi mitano?
  • Kwa nini Nuhu alimwachilia kunguru kutoka katika safina?
  • Nuhu alijuaje kwamba maji yalikuwa yamepungua duniani?
  • Mungu alimwambia Nuhu nini baada ya yeye na familia yake kukaa katika safina kwa zaidi ya mwaka mmoja?

Maswali ya ziada