Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

 JAMHURI YA DOMINIKA

Uvumilivu Waleta Kitulizo

Uvumilivu Waleta Kitulizo

Kuhubiri kwa Tahadhari

Rafael Pared, anayetumikia Betheli na mke wake, Francia, alianza kuhubiri mwaka wa 1957 akiwa na umri wa miaka 18. Anakumbuka jinsi askari wa upelelezi  walivyokuwa wakimfuata alipoenda kuhubiri ili wamkamate pamoja na wale aliokuwa akihubiri nao. Rafael anasema, “Nyakati nyingine tulihitaji kukimbia kupitia vichochoroni na kuruka wigo ili tusikamatwe.” Andrea Almánzar anaeleza jinsi walivyofanya ili wasikamatwe: “Tulihitaji kujihadhari. Tukiwa utumishi tungehubiri nyumba moja kisha kuacha nyumba kumi kabla ya kuhubiri inayofuata.”

Mwishowe Twapata Kitulizo!

Kufikia 1959, Trujillo alikuwa ametawala kwa karibu miaka 30, lakini hali ya kisiasa ilikuwa ikibadilika. Juni 14, 1959, Wadominika ambao walikuwa mafichoni waliivamia Jamhuri ya Dominika kwa lengo la kumpindua Trujillo. Ingawa mpango huo haukufanikiwa na wanamapinduzi hao waliuawa au kufungwa gerezani, idadi kubwa ya maadui wa Trujillo walihisi kwamba serikali yake haikuwa imara na hivyo wakaongeza upinzani.

Januari 25, 1960, baada ya miaka mingi ya kushirikiana na serikali ya Trujillo, viongozi wa Kanisa Katoliki waliandika barua rasmi wakipinga ukiukaji wa haki za binadamu. Mwanahistoria Mdominika Bernardo Vega anaeleza: “Uvamizi wa Juni 1959 na kuteswa kwa wote waliohusika katika uvamizi huo, na baadaye kuteswa kwa wapinzani wa chini kwa chini, ulifanya kanisa limpinge Trujillo kwa mara ya kwanza.”

Jambo la kupendeza ni kwamba mnamo Mei 1960, serikali iliwaondolea marufuku Mashahidi wa Yehova. Baada ya miaka mingi ya marufuku, kitulizo kilipatikana kutoka chanzo kisichotarajiwa, yaani, Trujillo mwenyewe, baada ya kutoelewana na Kanisa Katoliki.