Trujillo Auawa

Kufikia mwaka wa 1960, utawala wa dikteta Trujillo ulishutumiwa na jamii ya kimataifa na ulikabili upinzani mkali ndani ya nchi. Wakati wa misukosuko hiyo ya kisiasa, Milton Henschel kutoka makao makuu alitembelea Jamhuri ya Dominika na kuhudhuria kusanyiko la siku tatu lililofanywa Januari 1961. Watu 957 walihudhuria hotuba ya watu wote, na 27 wakabatizwa. Wakati wa ziara yake, Ndugu Henschel aliwasaidia akina ndugu kupanga upya kazi ya kuhubiri na kuchora ramani za eneo.

Waangalizi wawili wa mzunguko, Enrique Glass na Julián López, walipewa mgawo wa kutembelea makutaniko. Julián alieleza hivi: “Mzunguko wangu ulikuwa na makutaniko mawili mashariki mwa nchi na makutaniko mengine yote yalikuwa kaskazini. Enrique alizungukia makutaniko yaliyosalia upande wa mashariki na yote ya kusini mwa nchi.” Ziara hizo zilirudisha mawasiliano kati ya makutaniko na tengenezo na kuyaimarisha kiroho.

Juu: Salvino na Helen Ferrari wakisafiri kwenda Jamhuri ya Dominika, 1961

Salvino na Helen Ferrari, wahitimu wa darasa la pili la Gileadi, waliwasili mwaka wa 1961. Uzoefu wao wakiwa wamishonari nchini Kuba uliwasaidia sana katika kazi kubwa ya mavuno ya kiroho katika Jamhuri ya Dominika. Salvino alitumikia akiwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi hadi alipokufa mwaka wa 1997, na Helen amekuwa mtumishi wa wakati wote kwa miaka 79, mingi kati ya hiyo akiwa mmishonari.

Muda mfupi baada ya Salvino na Helen Ferrari kuwasili, utawala mkatili wa Trujillo ulikoma alipopigwa  risasi akiwa ndani ya gari lake usiku wa Mei 30, 1961. Hata hivyo, kuuawa kwake hakukuleta utulivu wa kisiasa, na nchi hiyo iliendelea kuwa na misukosuko ya kijamii na kisiasa kwa miaka mingi.

Kazi ya Kuhubiri Yasonga Mbele

Wakati huohuo, wamishonari zaidi waliwasili nchini. William Dingman, mhitimu wa darasa la kwanza la Gileadi na mke wake Estelle, pamoja na Thelma Critz na Flossie Coroneos walihamishwa kutoka ofisi ya tawi ya Puerto Riko kwenda Jamhuri ya Dominika siku mbili tu baada ya Trujillo kuuawa. “Nchi hiyo ilikuwa na misukosuko tulipowasili,” alieleza William, “na kulikuwa na shughuli za kijeshi za hapa na pale. Kulikuwa na hofu ya kutokea kwa mapinduzi, hivyo wanajeshi walikuwa wakimkagua kila mtu barabarani. Tulisimamishwa katika vituo kadhaa vya ukaguzi, na mizigo yetu kukaguliwa. Kila kitu kilitolewa kwenye masanduku yetu, hata vitu vidogo sana.” Haikuwa rahisi kuhubiri chini ya machafuko hayo ya kisiasa.

Chini: Thelma Critz, Estelle, na William Dingman bado wako nchini Dominika, baada ya kutumikia kwa miaka 67 katika kazi ya umishonari

William alisema: “Wakati wa utawala wa dikteta Trujillo, watu walielezwa kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa Wakomunisti na watu hatari zaidi. . . . Hata hivyo, hatua kwa hatua tulifanikiwa kutokomeza chuki hiyo.” Baada ya kazi kuanza upya, watu wengi wenye mioyo minyofu walianza kukubali ujumbe wa Ufalme. Kufikia mwishoni mwa mwaka wa utumishi wa 1961 kulikuwa na mapainia wa pekee 33 nchini.