Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

2015 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova

 JAMHURI YA DOMINIKA

Tetemeko la Ardhi Nchini Haiti

Tetemeko la Ardhi Nchini Haiti

Kuwahubiria Watu Wanaozungumza Kichina

Katika mwaka wa 2005, ofisi ya tawi ilimweka rasmi Mwanabetheli Mchina, Tin Wa Ng, kuwa painia wa pekee ili awahubirie Wachina katika Jamhuri ya Dominika. Alizaliwa na kulelewa katika Jamhuri ya Dominika. Wazazi wake walitoka China na kuhamia jijini Santo Domingo.

Kutaniko la Kichina cha Kimandarini lilianzishwa Januari 1, 2008, jijini Santo Domingo, na mwaka wa 2011 kikundi cha lugha hiyo kikaanzishwa jijini Santiago. Wahubiri 70, kutia ndani mapainia wa kawaida 36 na mapainia wengi wasaidizi, huongoza wastani wa mafunzo ya Biblia 76 kila mwezi.

 Kuwatafuta Watu Wanaozungumza Kiingereza

Kufikia mwaka wa 2007, kulikuwa na wahubiri 27,466 katika makutaniko 376, na mafunzo ya Biblia 49,795, yalikuwa yakiongozwa. Hata hivyo, hakukuwa na kutaniko la Kiingereza. Hivyo, Aprili 2008, ofisi ya tawi iliwatuma wamishonari Donald na Jayne Elwell kuanzisha kikundi cha Kiingereza jijini Santo Domingo. Kwanza wahubiri wachache wenye bidii walitafuta mahali ambako wazungumzaji wa Kiingereza wanaishi. Kisha, wakapanga maeneo ili waweze kuhubiri kikamili.

Matokeo ya jitihada hizo ni kwamba kikundi cha Kiingereza jijini Santo Domingo kiliendelea kukua, na kutaniko la wahubiri 39 likaanzishwa Julai 2009. Hatua kama hizo zilichukuliwa katika maeneo mengine katika nchi hiyo. Kufikia Novemba 2011, kulikuwa na makutaniko saba ya Kiingereza na kikundi kimoja.

Mwanamke Kiziwi na Kipofu Ashikamana na Viwango vya Yehova

Painia wa pekee akiwasiliana na Lorys kwa kumfanyia ishara kwenye mikono yake

Lorys, mwenye ugonjwa unaosababisha uziwi na upofu (Usher Syndrome), alifiwa na wazazi alipokuwa mdogo. Alizaliwa kiziwi na alianza kupoteza uwezo wake wa kuona alipokuwa na umri wa miaka 16. Anaweza kuona kidogo mchana lakini usiku haoni kabisa. Njia pekee anayotumia kuwasiliana usiku ni kwa kufanya ishara akitumia mikono yake.

Wenzi wa ndoa mapainia wa pekee walikutana na Lorys alipokuwa na umri wa miaka 23. Wakati huo, alikuwa akiishi na mwanamume kiziwi pamoja na binti yao mwenye umri wa mwaka mmoja aliye na uwezo wa kusikia. Lorys alihudhuria mkutano wa kutaniko na kuvutiwa sana na mambo aliyojifunza.

 Bila kukawia Lorys alifanya mabadiliko maishani mwake. Kwa mfano, alipojifunza kwamba haikufaa kuendelea kuishi na mwanamume huyo bila kufunga ndoa, alimwambia kuhusu umuhimu wa kuhalalisha uhusiano wao na kumweleza kwamba yeye atashikamana na viwango vya maadili vya Biblia. Akiwa amestaajabishwa na msimamo wake thabiti, mwanamume huyo alikubali kufunga ndoa.

 Baada ya kufunga ndoa, Lorys akawa mhubiri kisha akabatizwa. Alipokuwa akijifunza na Mashahidi, Lorys alijifunza pia Lugha ya Ishara ya Marekani (ASL). Tangu wakati huo, amekuwa akimsaidia binti yao kujifunza ASL na kumfundisha kweli.

Tetemeko la Ardhi Laikumba Haiti

Jumanne, Januari 12, 2010, itakumbukwa daima na Wadominika na Wahaiti. Siku hiyo tetemeko baya sana la ardhi liliikumba nchi ya Haiti. Bila kukawia, Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova liliipa idhini ofisi ya tawi ya Jamhuri ya Dominika itume pesa katika ofisi ya tawi ya Haiti ili kuiwezesha kutoa msaada. Kwa kuwa kiasi cha pesa kilichohitaji kutumwa kilikuwa kikubwa sana, daktari wa Betheli, Evan Batista, mwenye urefu wa mita 1.9 na uzani wa kilo 127, alipewa mgawo wa kupeleka pesa hizo.

 Uamuzi wa kumtuma Ndugu Batista ulifaa kwa kuwa alipofika mpakani, alijulishwa kwamba wataalamu wa tiba walihitajika sana. Waathiriwa wengi wa tetemeko la ardhi walikuwa wakipelekwa kwenye Jumba la Kusanyiko lililo karibu na ofisi ya tawi ya Haiti kwa ajili ya matibabu. Akina ndugu wa Haiti walipojua kwamba Ndugu Batista ni daktari wa Betheli, waliwasiliana na ofisi ya tawi ya Jamhuri ya Dominika na kuomba abaki nchini Haiti. Ombi lao lilikubaliwa na muda mfupi baada ya tetemeko hilo, ndugu na dada zetu wa kiroho nchini Haiti walianza kupokea msaada.

Ndugu walishirikiana ili kusaidia baada ya tetemeko la ardhi mwaka wa 2010 nchini Haiti

Idara ya Ununuzi katika ofisi ya tawi ya Jamhuri ya Dominika iliwasiliana mara moja na watu wanaowaletea chakula kwa ukawaida. Hatimaye, zaidi ya kilo 6,800 za mchele na maharagwe na bidhaa nyingine muhimu zilinunuliwa na kutumwa nchini Haiti saa 8:30 usiku siku ya Alhamisi, Januari 14, na inaonekana huo ndio uliokuwa msaada wa kwanza kutoka nje ya nchi kufika mpakani. Baadaye siku hiyo, madaktari watatu zaidi kutoka Jamhuri ya Dominika walisafiri kwa saa saba kwa gari hadi ofisi ya tawi ya Haiti. Waliwasili jioni, lakini badala ya kupumzika, walienda moja kwa moja kuwahudumia watu waliojeruhiwa mpaka usiku wa manane. Siku iliyofuata, madaktari wengine wanne na wauguzi wanne waliwasili kutoka Jamhuri ya Dominika. Upasuaji ulifanyika chini ya mazingira magumu sana kwenye kibanda cha dharura kilichojengwa katika Jumba la Kusanyiko. Kwa juma moja, jumla ya madaktari na wauguzi 12 walikuwa wamewatibu majeruhi 300.

Kila siku, watu waliojeruhiwa sana walipelekwa katika Jamhuri ya Dominika kwa matibabu zaidi. Nyakati fulani, magari yaliyopeleka msaada nchini Haiti yalibeba watu waliojeruhiwa na kuwapeleka kwenye  vituo vya afya katika Jamhuri ya Dominika. Ofisi ya tawi ilipanga Vikundi vya Kuwatembelea Wagonjwa ili kuwatia moyo waliojeruhiwa na kuhakikisha kwamba wamepata dawa na mahitaji mengine. Makutaniko yaliwapa chakula na malazi watu wa familia ambao waliwasindikiza wapendwa wao waliojeruhiwa.

Mashahidi wa Yehova waligawanya kilo 450,000 hivi za bidhaa mbalimbali kutia ndani vifurushi vidogo 400,000 vya chakula

Jitihada za watu wa Yehova baada ya tetemeko hilo zilidhihirisha wazi ukweli wa maneno ya Methali 17:17 yanayosema: “Rafiki wa kweli anapenda nyakati zote, naye ni ndugu aliyezaliwa kwa ajili ya wakati wa taabu.” Mambo ambayo ndugu zetu walijionea yanaonyesha jinsi ambavyo Yehova amewategemeza watu wake waaminifu kupitia roho yake, undugu wa Kikristo, na amefanya hivyo hata wakati wa misiba. Kazi kubwa ya kutoa msaada iliendelea kwa miezi kadhaa. Mashahidi wa Yehova walitoa kilo 450,000 hivi za bidhaa mbalimbali, kutia ndani vifurushi vidogo 400,000 vya chakula. Ndugu na dada 78 wataalamu wa afya kutoka sehemu mbalimbali duniani walikuja na kujitolea kwa hiari kutumia muda na ujuzi wao, wakifanya kazi pamoja na wajitoleaji wengine wengi. *

^ fu. 1 Kwa habari zaidi, ona gazeti la Amkeni! la Desemba 2010, ukurasa wa 14-19.