KULIKUWA na uhusiano gani kati ya Trujillo na Kanisa Katoliki? Mchambuzi fulani wa masuala ya kisiasa alisema: “Katika kipindi kirefu cha utawala wa Trujillo, 1930-1961, Kanisa lilishirikiana na serikali ya Dominika kutegemeza taasisi mbalimbali; mtawala huyo alilipendelea Kanisa, nalo Kanisa likaunga mkono utawala wake.”

Mwaka wa 1954, Trujillo alisafiri kwenda Roma na akatia sahihi makubaliano na Papa. Germán Ornes, aliyekuwa mshirika wa karibu wa Trujillo aliandika hivi: “Kwa kuwa Kanisa la Dominika linamuunga mkono sana Trujillo, hilo limemwimarisha sana ‘Mkuu’ [Trujillo]. Makasisi, wakiongozwa na Maaskofu Wakuu Ricardo Pittini na Octavio Beras, ni kati ya waeneza-propaganda wakuu wa utawala huu.”

“Kila anapopata fursa,” akaendelea kusema Ornes, “Papa hutuma ujumbe wa kumsalimu Trujillo. . . . Katika Kongamano la Kanisa Katoliki mwaka wa 1956, lililofanywa huko Ciudad Trujillo ambalo lilifadhiliwa na Trujillo, Kadinali  Spellman, ambaye alikuwa mwakilishi maalumu wa Papa, alileta ujumbe wa pekee. Kadinali Spellman alisafiri kutoka New York na akapokewa kwa vishindo na Jenerali [Trujillo] mwenyewe. Siku iliyofuata, picha zao wakiwa wamekumbatiana zilichapishwa kwenye ukurasa wa kwanza wa magazeti yote nchini Dominika.”

Mwaka wa 1960, gazeti la Time liliripoti hivi: “Mpaka sasa, Trujillo amekuwa na uhusiano mzuri na kanisa. Askofu Mkuu Ricardo Pittini, Mkuu wa Kidini wa Amerika, ambaye sasa ana umri wa miaka 83 amepofuka, lakini miaka minne iliyopita alitia sahihi barua iliyoandikiwa gazeti la New York Times ikimsifu Trujillo na kusema kwamba ‘“dikteta” huyu anapendwa na kuheshimiwa na wananchi.’”

Hata hivyo, baada ya kuunga mkono utawala wa kikatili wa Trujillo kwa miaka 30, Kanisa Katoliki lilianza kubadili msimamo mambo yalipoanza kubadilika kisiasa. “Watu walipozidi kupinga utawala wa kidikteta,” mchambuzi huyo anaeleza, “na baadaye, jitihada za kuanzisha mfumo wa kidemokrasia nchini zilipoanza, Kanisa, ambalo kwa muda mrefu lilishirikiana na Trujillo, lililazimika kubadili msimamo.”

Hatimaye, mwaka wa 2011 Kanisa lililazimika kuwaomba radhi raia wa Dominika. Barua rasmi ambayo ilinukuliwa katika gazeti la Dominican Today ilisema: ‘Tunakiri makosa tuliyofanya kwa kutoshikamana na imani yetu, wito wetu, na majukumu yetu. Kwa hiyo, tunaomba msamaha na tunawasihi raia wote wa Dominika watuelewe na kutukubali.’