Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

2014 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova

 SIERRA LEONE NA GUINEA

1991-2001 ‘Tanuru ya Mateso’—Isa.48:10 (Sehemu ya 2)

1991-2001 ‘Tanuru ya Mateso’—Isa.48:10 (Sehemu ya 2)

Betheli Yavamiwa!

Mnamo Februari 1998, Jeshi la Kulinda Amani la Nchi za Afrika Magharibi (ECOMOG) lilianzisha mpango hususa wa kuyaondoa kabisa majeshi ya waasi katika jiji la Freetown. Inasikitisha kwamba Ndugu mmoja aliuawa kwa kipande cha kombora katika mapigano hayo makali.

Karibu wahubiri 150 hivi walikimbilia kwenye nyumba za wamishonari zilizokuwa Kissy na Cockerill. Laddie Sandy, mmoja kati ya walinzi wawili wa Betheli, anaeleza hivi: “Usiku mmoja, mimi na Philip Turay tulipokuwa kwenye zamu ya ulinzi, waasi wawili wa kikundi cha RUF walikuja Betheli na kutuamuru tufungue mlango. Tulipokuwa tukijaribu kujificha, wanaume hao walimiminia risasi kufuli la mlangoni ili walivunje. Jambo la ajabu ni kwamba kufuli hilo halikuvunjika, nao hawakukumbuka kuvunja vioo vya mlangoni. Wakaondoka wakiwa wamekasirika.

“Siku mbili baadaye, waasi hao walirudi usiku wakiwa pamoja na waasi wengine 20 hivi, wakati huu walikuwa wameazimia kabisa kuingia ndani ya jengo. Mara moja tukaijulisha familia ya Betheli na kukimbilia kwenye vyumba vilivyo chini ya jengo, mahali ambapo iliamuliwa mapema kwamba wote wakimbilie ili kujificha. Wanabetheli wote saba tukajificha kwenye giza nyuma ya mitungi miwili mikubwa, huku tukitetemeka kwa woga. Waasi hao walilivunja kufuli la mlangoni kwa risasi nao wakaingia ndani ya jengo. Mmoja wa waasi hao akasema kwa sauti kubwa, ‘watafuteni Mashahidi Yehova na mkate shingo zao.’ Tulijikunyata kimya waasi hao walipokuwa wakiiba na kupekua-pekua ndani ya jengo kwa muda wa saa saba. Mwishowe, baada ya kuharibu vitu vingi, walichukua vitu walivyotaka na kuondoka.

“Tulikusanya vitu vyetu na kukimbilia kwenye nyumba ya wamishonari iliyokuwa karibu katika eneo la Cockerill, ambayo zamani ilikuwa Betheli. Tukiwa njiani, tulivamiwa na kikundi kingine cha waasi. Tulifika huko tukiwa na wasiwasi mwingi sana, lakini tulifurahi kwamba tuko hai. Baada ya kupumzika kwa siku chache, tulirudi Betheli ili kufanya usafi.”

Miezi miwili baadaye, jiji la Freetown likawa chini ya udhibiti wa majeshi ya ECOMOG, hivyo wamishonari waliokimbilia nchini Guinea wakaanza kurudi jijini. Hata hivyo, hawakujua kwamba wangekaa kwa muda mfupi.

Operesheni Angamiza Kila Kitu

Miezi nane baadaye, mnamo Desemba 1998, mamia ya wajumbe walihudhuria Kusanyiko la Wilaya lenye kichwa “Njia ya Mungu ya Maisha” katika Uwanja wa Taifa jijini Freetown. Ghafla, walisikia mlipuko kwa mbali na moshi ulioneka­na ukipanda kutoka milimani. Jeshi la waasi lilikuwa limerudi!

Siku zilizofuata, hali katika jiji la Freetown ilizidi kuwa mbaya. Halmashauri ya Tawi ilikodi ndege ndogo na kuwahamisha wamishonari 12, Wanabetheli nane wanaotumikia katika nchi ya kigeni, na wajenzi wa kujitolea watano hadi katika jiji la Conakry. Siku tatu baadaye, Januari 6, 1999, waasi hao walianzisha kampeni ya kikatili iliyoitwa Operesheni Angamiza Kila Kitu. Waasi hao waliliharibu kwa kiasi kikubwa jiji la Freetown, na kuua karibu watu 6,000. Walikata mikono na miguu ya watu, wakateka nyara mamia ya watoto, na kuharibu maelfu ya majengo.

Ndugu fulani aliyekuwa kipenzi cha watu, Edward Toby, aliuawa kikatili sana. Zaidi ya wahubiri 200 walipewa mahali pa kukaa Betheli na kwenye nyumba ya wamishonari iliyokuwa Cockerill. Wengine walijificha katika nyumba zao. Mashahidi ambao walikaa katika nyumba ya wamishonari ya Kissy, iliyokuwa mashariki mwa mji huo, walihitaji msaada wa haraka sana wa matibabu. Hata hivyo, ilikuwa hatari sana kupita jijini. Ni nani angehatarisha uhai wake kwa ajili yao? Laddie Sandy na Philip Turay, walinzi jasiri wa Betheli walijitolea mara moja.

Philip anakumbuka hivi: “Kulikuwa na machafuko jijini Freetown. Wanajeshi waasi walisimamisha watu katika vituo vya ukaguzi na kuwasumbua. Kuliwekwa amri ya kutotembea kuanzia alasiri hadi asubuhi ya siku iliyofuata, na hivyo kufanya iwe vigumu kwetu kusafiri. Siku mbili baada ya kuanza safari yetu, tukafika katika nyumba ya wamishonari ya Kissy na kukuta kila kitu kimeporwa na nyumba kuchomwa.

“Tulipoangalia kwa makini eneo lililozunguka nyumba hiyo, tulimwona ndugu Andrew Caulker akiwa amejeruhiwa vibaya kichwani. Waasi hao walikuwa wamemfunga na kumpiga mara kadhaa kichwani kwa shoka. Jambo la ku­shangaza ni kwamba hakuuawa na alifanikiwa kutoroka. Tukampeleka hospitali mara moja, na pole pole alianza kupata nafuu. Baadaye alitumikia akiwa painia wa kawaida.”

(Kushoto kwenda kulia) Laddie Sandy, Andrew Caulker, na Philip Turay

Mashahidi wengine hawakuuawa au kujeruhiwa kwa sababu ya msimamo wao wa Kikristo wa kutounga mkono upande wowote. Ndugu mmoja anaeleza hivi: “Waasi hao walituamuru tujifunge vitambaa vyeupe kichwani na kucheza dansi barabarani ili kuonyesha kwamba tunawaunga mkono. Wakatuambia, ‘mkikataa, tutawakata mikono au miguu ama tutawaua.’ Tukiwa na woga, mimi na mke wangu tulisimama pembeni kidogo huku tukisali kwa Yehova kimyakimya ili atusaidie. Kijana fulani ambaye alikuwa jirani yetu na alishirikiana na waasi hao alipoona taabu yetu, akamwambia kamanda wao hivi: ‘Huyu ni “ndugu” yetu. Yeye hajihusishi na mambo ya siasa, hivyo tutacheza kwa niaba yake.’ Akiwa ameridhika, kamanda huyo aliondoka, nasi tukaharakisha kwenda nyumbani.”

Hali ilipoanza kutulia jijini, akina ndugu walianza tena kufanya mikutano na kwenda utumishini wakiwa wenye tahadhari. Wahubiri walivaa beji za kusanyiko ili kujitambulisha katika vituo vya ukaguzi. Ndugu waliosimama katika foleni hizo kwa muda mrefu walipata uzoefu mzuri wa kuanzisha mazungumzo ya Biblia.

Jiji lilipokumbwa na upungufu mkubwa wa kila aina ya bidhaa, ofisi ya tawi ya Uingereza ilituma maboksi 200 ya msaada. Billie Cowan na Alan Jones walisafiri kwa ndege kutoka Conakry hadi Freetown ili wakasaidie kupitisha maboksi hayo kutoka kwenye kituo kimoja cha ukaguzi baada ya kingine. Maboksi hayo yalifika Betheli kabla tu ya amri ya kutotembea jioni kuanza. James Koroma alisafiri mara kwa mara kwenda Conakry na kurudi na vitabu na bidhaa nyingine muhimu. Baadhi ya chakula hicho cha kiroho kiligawa­nywa kwa wahubiri katika maeneo ya mbali huko Bo na Kenema.

Msaada ukiwasili jijini Freetown

Mnamo Agosti 9, 1999, wamishonari waliokuwa jijini Conakry walianza kurudi Freetown. Mwaka uliofuata, kikosi cha jeshi la Uingereza kiliwaondoa waasi hao katika jiji la Freetown. Mapigano ya hapa na pale yaliendelea kwa muda, lakini kufikia Januari 2002 ilitangazwa rasmi kuwa vita vimeisha. Katika vita hivyo vilivyopiganwa kwa miaka 11, watu 50,000 waliuawa, watu 20,000 walilemazwa, nyumba 300,000 ziliharibiwa, na watu milioni 1.2 hawakuwa na makazi.

Tengenezo la Yehova lilikabilianaje na hali hiyo? Ni wazi kwamba Yehova alililinda na kulibariki tengenezo lake. Katika muda wote huo wa vita, watu 700 hivi walibatizwa. Mamia ya Mashahidi walikimbia maeneo ya vita, lakini bado idadi ya wahubiri nchini Sierra Leone iliongezeka kwa asilimia 50. Nchi ya Guinea ilikuwa na ongezeko la wahubiri zaidi ya asilimia 300! Hata hivyo, jambo muhimu zaidi ni kwamba watu wa Mungu waliendelea kuwa waaminifu washikamanifu. Wakiwa katika ‘tanuru ya mateso,’ walidumisha umoja na upendo wa Kikristo na “wakaendelea bila kuacha kufundisha na kutangaza habari njema.”Isa. 48:10; Mdo. 5:42.