Juni 28, 2013, Tovuti ya jw.org ilitangaza kwamba hivi karibuni Maktaba ya Watchtower KWENYE MTANDAO ilipatikana katika lugha 100. Hiyo ilikuwa hatua kubwa sana katika historia. Maktaba hiyo ina vifaa vya kufanyia utafiti kama vile vilivyo kwenye Watchtower Library, inayopatikana kwenye CD-ROM. Unaweza kutumia maktaba kwenye mtandao ukiwa na vifaa vinavyoweza kuunganishwa na Intaneti, kama vile kompyuta na simu za mkononi. Machapisho mengi katika maktaba hiyo yanaanzia mwaka wa 2000 na kuendelea. Pia Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya na mabuku ya Insight on the Scriptures yanapatikana katika lugha nyingi. Sehemu ya kufanyia utafiti inaweza kutafuta neno, sentensi au kifungu cha maneno kama tu ilivyo kwenye Watchtower Library. Unaweza kutumia maktaba hiyo kutafuta maandiko au habari fulani katika lugha moja na kupatanisha na lugha nyingine. Zifuatazo ni baadhi ya barua za shukrani kwa sababu ya kifaa hiki cha kufanyia utafiti:

“Asanteni sana kwa Maktaba ya Watchtower KWENYE MTANDAO. Nilipoona kifaa hiki kipya cha kujifunzia, nilithamini sana. Sina ujuzi mwingi wa kompyuta, hata hivyo ninaweza kusema kwamba kifaa hiki cha kufanyia utafiti kimebuniwa kwa ustadi wa hali ya juu sana. Upendo wenu kwa jirani, ndugu, na kwa Yehova unaonekana waziwazi. Jinsi maktaba hiyo ilivyopangwa inaonyesha kwamba mnatujali. Maktaba hii ni zawadi bora sana na wonyesho wa upendo na ukarimu wa Baba yangu wa mbinguni, Yehova. Asanteni sana.”—A., Argentina.

“Siamini! Leo alasiri nilitembelea Maktaba ya Watchtower, na lugha ya Krioli ya Haiti ni miongoni mwa lugha mpya zilizowekwa. Sikuwahi kufikiria kwamba lugha hiyo inaweza kuwekwa kwenye mtandao. Kwa kweli, sina la kusema! Yehova na abariki jitihada zenu zote na roho yake takatifu iendelee kuwaongoza.”—D.C., Marekani.