Kikundi fulani cha watafiti kilikuwa kikipekua mabonde na mapango yaliyo kwenye nyika ya Yudea, walipoingia ndani ya pango lililo kwenye mwamba mrefu. Je, wangepata vitu vyenye thamani, labda hati za kale kama vile Vitabu vya Kukunjwa vya Bahari ya Chumvi? Walifurahi kupata vitu mbalimbali vyenye thamani ambavyo baadaye viliitwa hazina ya Nahal Mishmar.

HAZINA hiyo iliyokuwa imefungwa kwa mkeka na kufichwa ndani ya ufa, ilipatikana Machi 1961. Ilikuwa na vyombo 400 hivi, vingi kati yavyo vikiwa vya shaba. Kulikuwa na mataji, fimbo za kifalme, vifaa vya kazi, rungu, na silaha nyingine. Vitu hivyo vinawasaidia wasomaji wa Biblia kuelewa jambo linalosemwa kwenye Mwanzo 4:22 kumhusu Tubal-Kaini aliyekuwa “mfuaji wa kila namna ya vifaa vya shaba na chuma.”

Bado kuna maswali mengi kuhusu chanzo cha hazina hiyo yenye thamani. Hata hivyo, uvumbuzi huo unaonyesha kwamba katika maeneo yanayotajwa katika Biblia, shaba ilikuwa ikichimbwa, kuyeyushwa, na kutengeneza vyombo mbalimbali tangu zamani za kale.

MIGODI YA SHABA KATIKA NCHI YA AHADI

Waisraeli walipokaribia kuingia Nchi ya Ahadi, Musa aliwaambia hivi: “Kutoka katika milima [ya nchi hiyo] utachimba shaba.” (Kumbukumbu la Torati 8:7-9) Wachimbuzi wa vitu vya kale wamepata migodi na maeneo ya kuyeyushia shaba huko Israel na Jordan, kwa mfano huko Feinan, Timna, na Khirbat en-Nahas. Maeneo hayo yanathibitisha nini?

Huko Feinan na pia Timna, kuna mashimo mengi madogo yaliyokuwa migodi ya shaba kwa zaidi ya miaka 2,000. Hata leo, maeneo hayo yana mawe yenye vipande vidogo-vidogo vya shaba. Wachimba migodi wa kale walifanya kazi ngumu ya kutafuta shaba wakitumia vifaa vilivyotengenezwa kwa mawe. Ili kupata shaba zaidi, walichimba ndani sana wakitumia vifaa vya chuma, na hivyo kupanua mapango na kutengeneza vijia vya chini ya ardhi. Kitabu cha Biblia cha Ayubu kinataja kazi hiyo ya kuchimba madini. (Ayubu 28:2-11) Ilikuwa kazi ngumu sana hivi kwamba kuanzia karne ya tatu hadi ya tano W.K., serikali ya Roma iliwahukumu wahalifu sugu na wafungwa wengine kufanya kazi kwenye migodi ya shaba huko Feinan.

Marundo makubwa ya uchafu uliotolewa kwenye shaba huko Khirbat en-Nahas (jina linalomaanisha “Mabaki ya Shaba”), yanaonyesha kwamba huenda shaba iliyeyushwa kwa wingi katika eneo hilo. Wasomi wanadai kuwa baada ya shaba kuchimbwa kwenye migodi iliyokuwa karibu kama  vile Feinan na Timna ililetwa huko ili isafishwe. Ili kuondoa uchafu, shaba ilitiwa ndani ya tanuru yenye moto wa makaa uliopulizwa kwa ustadi hadi kufikia nyuzi 1,200 Selsiasi kwa muda wa saa nane hadi kumi. Ili kupata kilo moja ya shaba safi, walihitaji kuyeyusha kilo tano za shaba iliyochimbwa. Kisha shaba safi ilitumiwa kutengenezea vyombo mbalimbali.

MATUMIZI YA SHABA KATIKA ISRAELI LA KALE

Kwenye Mlima Sinai, Yehova Mungu aliagiza kwamba shaba ambayo ingepatikana kwenye nchi hiyo itumiwe kutengeneza maskani na baadaye hekalu huko Yerusalemu lilijengwa kwa muundo wa maskani. (Kutoka, sura ya 27) Kabla ya kwenda Misri, huenda Waisraeli walijua kutengeneza vifaa vya chuma, au huenda walijifunza ustadi huo huko Misri. Wakiwa safarini kwenda kwenye Nchi ya Ahadi, walikuwa na uwezo wa kutengeneza sanamu ya kuyeyushwa ya ndama. Pia, walikuwa na uwezo wa kutengeneza vifaa vingi vya shaba vilivyotumiwa kwenye maskani, kama vile beseni kubwa, vyungu, vikaango, sepetu, na uma.—Kutoka 32:4.

Baadaye wakiwa jangwani, labda karibu na Punoni (inaelekea ni karibu na mji wa kisasa wa Feinan), eneo lenye shaba nyingi, watu walilalamika kuhusu mana na pia maji. Yehova aliwaadhibu kwa kuwatuma nyoka wenye sumu, na watu wengi wakafa. Waisraeli walipotubu, Musa aliingilia kati, na Yehova akamwagiza atengeneze nyoka wa shaba kisha amweke juu ya nguzo. Simulizi hilo linasema hivi: “Ikawa kwamba nyoka alipomuuma mtu naye akamtazama yule nyoka wa shaba, ndipo alipoendelea kuwa hai.”—Hesabu 21:4-10; 33:43.

SHABA YA MFALME SULEMANI

Sehemu nyingi za hekalu la Yerusalemu zilitengenezwa kwa shaba

Mfalme Sulemani alitumia shaba nyingi kurembesha hekalu huko Yerusalemu. Daudi, baba ya Sulemani, ndiye aliyekusanya kiasi kikubwa cha shaba hiyo alipowashinda Wasiria. (1 Mambo ya Nyakati 18:6-8) “Bahari ya kuyeyushwa” ya shaba ambayo ilitumiwa na makuhani kuoga, ilikuwa na uwezo wa kubeba lita 66,000 za maji na huenda ilikuwa na uzito wa tani 30. (1 Wafalme 7:23-26, 44-46) Kisha kulikuwa na nguzo mbili kubwa za shaba kwenye mwingilio wa hekalu. Zilikuwa na kimo cha mita 8, na juu yake zilikuwa na makombe yenye urefu wa mita 2.2. Nguzo hizo zilizokuwa na shimo katikati, zilikuwa na shaba yenye upana wa sentimita 7.5, na kipenyo cha mita 1.7. (1 Wafalme 7:15, 16; 2 Mambo ya Nyakati 4:17) Inashangaza tunapofikiria shaba nyingi iliyotumiwa kutengeneza vitu hivyo.

Nyakati za Biblia, shaba ilitumiwa pia katika shughuli za kila siku. Kwa mfano, tunasoma kuhusu silaha, mikatale, ala za muziki, na milango ya shaba. (1 Samweli 17:5, 6; 2 Wafalme 25:7; 1 Mambo ya Nyakati 15:19; Zaburi 107:16) Yesu alitaja pesa za “shaba” kwa ajili ya mikoba, na mtume Paulo alimtaja “Aleksanda yule fundi wa shaba.”—Mathayo 10:9; 2 Timotheo 4:14.

Bado wataalamu wa vitu vya kale na wanahistoria wanachunguza chanzo cha shaba nyingi katika nyakati za Biblia, na pia chanzo cha hazina ya Nahal Mishmar. Ingawa hivyo, kama Biblia inavyosema, nchi ambayo Waisraeli walirithi ilikuwa ‘nchi nzuri, ambayo kutoka katika milima yake wangechimba shaba.’—Kumbukumbu la Torati 8:7-9.