Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Kwa nini jiji la kale la Ninawi liliitwa “jiji la umwagaji wa damu”?

Mchoro wa ukutani wa wapiganaji waliobeba vichwa vya maadui waliotekwa wakivitupa kwenye rundo

Ninawi lilikuwa jiji kuu la Milki ya Ashuru. Lilikuwa jiji kubwa lenye mahekalu na maeneo yenye kuvutia, barabara pana, na kuta ndefu. Nabii Myahudi Nahumu aliliita “jiji la umwagaji wa damu.”—Nahumu 3:1.

Huo ni ufafanuzi unaofaa kwa sababu michoro ya ukutani katika jumba la mfalme Senakeribu huko Ninawi inathibitisha ukatili huo. Mchoro mmoja unaonyesha mtesaji aking’oa ulimi wa mfungwa aliyepigiliwa ardhini. Maandishi ya ukutani yanasema kwamba mateka walifungwa kwa minyororo iliyokuwa na kulabu zilizoingizwa puani au midomoni. Maofisa waliotekwa walidhihakiwa kwa kufungwa shingoni vichwa vya wafalme wao waliouawa.

Mtaalamu wa mambo ya Ashuru Archibald Henry Sayce anafafanua ukatili uliofuata baada ya mji kutekwa: “Vichwa vya wanadamu vilipangwa kama piramidi kwenye barabara ya mshindi; wavulana na wasichana walichomwa wakiwa hai au kuwekwa kando ili wateswe baadaye; wanaume walitundikwa, walichunwa ngozi wakiwa hai, walipofushwa, au kukatwa mikono na miguu, masikio na pua.”

Kwa nini Wayahudi walipaswa kuweka ukuta wa ukingoni kuzunguka paa za nyumba zao?

Wayahudi waliagizwa hivi na Mungu: “Ikiwa utajenga nyumba mpya, pia utafanya ukuta wa ukingoni kwa ajili ya dari [paa] lako, ili usiletee nyumba yako hatia ya damu kwa sababu mtu anaweza kuanguka kutoka hapo.” (Kumbukumbu la Torati 22:8) Ukuta wa ukingoni ulikuwa muhimu kwa ajili ya usalama, kwa sababu familia za Kiyahudi katika nyakati za Biblia zilitumia sana paa za nyumba zao.

Nyumba nyingi za Waisraeli zilikuwa na paa lililo tambarare. Paa lilikuwa mahali pazuri pa watu kuota jua, kufurahia hewa safi, au kufanyia kazi za nyumbani. Katika majira ya joto palikuwa mahali pazuri pa kulala. (1 Samweli 9:26) Mkulima angetumia paa kukaushia nafaka kabla ya kuzisaga au kukaushia tini na zabibu.—Yoshua 2:6.

Vilevile, paa lilitumiwa kwa ajili ya ibada, ya kweli au ya sanamu. (Nehemia 8:16-18; Yeremia 19:13) Mtume Petro alienda kwenye paa saa sita mchana ili kusali. (Matendo 10:9-16) Ikiwa paa lilifunikwa na matawi ya mzabibu au mtende, lilikuwa mahali pazuri sana pa kupumzikia.

Kitabu The Land and the Book kinasema kwamba nyumba za Waisraeli zilikuwa na ngazi zilizoelekea kwenye paa, upande wa “nje ya nyumba, lakini ndani ya ua wa nje.” Hivyo, mwenye nyumba angeshuka kutoka kwenye paa bila kuingia ndani ya nyumba. Hilo linatusaidia kuelewa onyo hili la Yesu kuhusu kuondoka haraka katika jiji ambalo lingeangamizwa: “Mtu aliye juu ya paa ya nyumba asishuke kuchukua mali kutoka katika nyumba yake.”—Mathayo 24:17.