Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Mnara wa Mlinzi—Toleo la Funzo  |  Agosti 2015

 KUTOKA KATIKA HIFADHI YA VITU VYETU VYA KALE

“Yehova Aliwaleta Ufaransa ili Mjifunze Kweli”

“Yehova Aliwaleta Ufaransa ili Mjifunze Kweli”

AKIWA mvulana mdogo, Antoine Skalecki alikuwa na farasi ambaye alitembea naye kila mahali. Alitembea pamoja na farasi wake alipokuwa akisafirisha makaa ya mawe kwenye mgodi ulio meta 500 chini ya ardhi. Antoine alilazimika kufanya kazi hiyo ngumu kwa saa tisa kila siku baada ya baba yake kujeruhiwa kwenye mgodi ulioporomoka. Wakati fulani, Antoine alinusurika kufa mgodini.

Vifaa vilivyotumiwa na wachimbaji wa makaa ya mawe, na mgodi ulioko Dechy, karibu na Sin-le-Noble, ambako Antoine Skalecki alifanya kazi

Antoine alikuwa miongoni mwa watoto wengi waliozaliwa nchini Ufaransa na wazazi Wapolandi katika miaka ya 1920 na 1930. Kwa nini Wapolandi walihamia Ufaransa? Nchi ya Poland ilipopata uhuru baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, watu waliongezeka sana na hivyo kukawa na tatizo la idadi kubwa ya watu. Kwa upande mwingine, Ufaransa ilipoteza zaidi ya wanaume milioni moja vitani na walihitaji sana wafanyakazi kwenye migodi ya makaa ya mawe. Kwa hiyo, Septemba 1919 serikali ya Ufaransa na Poland zilisaini mkataba wa uhamiaji. Kufikia mwaka wa 1931 idadi ya Wapolandi nchini Ufaransa ilifikia 507,800, na wengi wao waliishi kwenye maeneo yenye migodi kaskazini mwa nchi.

Wapolandi hao wachapakazi hawakuacha utamaduni wao, kutia ndani mtazamo wao wa kupenda dini. Antoine, ambaye sasa ana umri wa miaka 90, anakumbuka hivi: “Babu yangu, Joseph, aliyaheshimu Maandiko Matakatifu kama baba yake.” Siku ya Jumapili, Wapolandi walivaa mavazi bora kabisa walipokuwa wakienda kanisani, kama walivyofanya walipokuwa nchini mwao. Jambo hilo liliwachukiza baadhi ya Wafaransa wasiopenda dini.

Wapolandi wengi walikutana na Wanafunzi wa Biblia kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Nord-Pas-de-Calais. Wanafunzi hao walikuwa wakihubiri kwa bidii katika eneo hilo tangu mwaka wa 1904. Mnamo mwaka wa 1915, gazeti la Mnara wa Mlinzi lilianza kuchapishwa kila mwezi katika lugha ya Kipolandi, na The Golden Age (sasa Amkeni!) lilianza kuchapishwa katika lugha hiyo mwaka wa 1925. Familia nyingi zilifurahia habari za Kimaandiko zilizopatikana kwenye magazeti hayo na pia katika kitabu The Harp of God cha Kipolandi.

Familia ya Antoine iliwajua Wanafunzi wa Biblia kupitia mjomba wake, ambaye alihudhuria  mkutano kwa mara ya kwanza mwaka wa 1924. Mwaka huohuo, Wanafunzi wa Biblia walifanya kusanyiko la kwanza katika lugha ya Kipolandi huko Bruay-en-Artois. Siku chache baadaye, mwakilishi wa makao makuu, Joseph F. Rutherford, alifanya mkutano uliohudhuriwa na watu 2,000 katika mji huo. Baada ya kuona Wapolandi wengi waliohudhuria, Ndugu Rutherford aliwaambia hivi: “Yehova aliwaleta Ufaransa ili mjifunze kweli. Kwa hiyo, ninyi na watoto wenu mnapaswa kuwasaidia Wafaransa! Bado kuna kazi kubwa ya kuhubiri, na Yehova atasaidia kuongeza idadi ya wafanyakazi.”

Yehova Mungu alifanya hivyo! Wapolandi hao walihubiri kwa bidii kama walivyokuwa wakifanya kazi kwa bidii migodini! Baadhi yao walirudi Poland ili kuwaeleza wengine kweli zenye thamani walizojifunza. Teofil Piaskowski, Szczepan Kosiak, na Jan Zabuda walikuwa kati ya wale walioondoka Ufaransa ili wakaeneze habari njema nchini Poland.

Lakini waeneza-injili wengi Wapolandi walibaki Ufaransa na waliendelea kuhubiri kwa bidii pamoja na ndugu na dada zao Wafaransa. Katika kusanyiko lililofanywa mwaka wa 1926 huko Sin-le-Noble, watu 1,000 walihudhuria sehemu iliyofanywa kwa Kipolandi, na watu 300 katika sehemu ya Kifaransa. Kitabu cha Mwaka cha 1929 kiliripoti hivi: “Katika mwaka huo ndugu 332 Wapolandi walibatizwa.” Kabla ya Vita vya Pili vya Ulimwengu kuanza, makutaniko 32 kati ya 84 nchini Ufaransa yalikuwa ya Kipolandi.

Ndugu na dada Wapolandi nchini Ufaransa wakielekea kusanyikoni. Kibao kimeandikwa “Mashahidi wa Yehova”

Mwaka wa 1947, Mashahidi wengi wa Yehova walikubali ombi la serikali la kurudi Poland. Hata baada ya kuondoka, matokeo ya kazi yao na ya waumini wenzao Wafaransa yalionekana kupitia ongezeko la asilimia kumi ya wahubiri wa Ufalme katika mwaka huo. Kisha kukawa na ongezeko la asilimia 20, 23, na 40 kuanzia mwaka wa 1948 hadi 1950! Ili kuwazoeza wahubiri hao wapya, ofisi ya tawi ya Ufaransa ilianza kuwaweka rasmi waangalizi wa mzunguko mwaka wa 1948. Kati ya watano waliochaguliwa, wanne walikuwa Wapolandi, na Antoine Skalecki alikuwa miongoni mwao.

Mashahidi wa Yehova wengi nchini Ufaransa bado wana majina ya ukoo ya Kipolandi waliyorithishwa na mababu zao, ambao walifanya kazi kwa bidii migodini na katika utumishi wa shambani. Leo pia, wahamiaji wengi nchini Ufaransa wanajifunza kweli. Iwe waeneza-injili hao kutoka nchi nyingine watarudi nchini kwao au la, wanaiga bidii ya watangazaji wa Ufalme Wapolandi walioishi kabla yao.—Kutoka katika hifadhi ya vitu vyetu vya kale nchini Ufaransa.