Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Mnara wa Mlinzi (Toleo la Funzo)  |  Agosti 2015

Tunajifunza Nini Kutoka kwa Yoana?

Tunajifunza Nini Kutoka kwa Yoana?

WATU wengi wanajua kwamba Yesu alikuwa na mitume 12. Lakini huenda hawatambui kwamba baadhi ya wanafunzi walioshirikiana naye kwa ukaribu walikuwa wanawake. Yoana alikuwa mmoja wa wanawake hao.—Mt. 27:55; Luka 8:3.

Yoana alitimiza nini katika huduma ya Yesu, na tunaweza kujifunza nini kutokana na mfano wake?

YOANA ALIKUWA NANI?

Yoana alikuwa “mke wa Kuza, msimamizi wa Herode.” Inawezekana Kuza alikuwa msimamizi wa nyumba ya Herode Antipasi. Yoana alikuwa kati ya wanawake walioponywa na Yesu. Yoana na wanawake wengine walisafiri pamoja na Yesu na mitume wake.—Luka 8:1-3.

Marabi wa Kiyahudi walifundisha kwamba wanawake hawakupaswa kushirikiana wala kusafiri na wanaume ambao hawakuwa watu wao wa ukoo. Kwa kweli, wanaume wa Kiyahudi hawakuwa na kawaida ya kuzungumza na wanawake. Yesu hakufuata desturi hizo, badala yake alimruhusu Yoana na wanawake wengine waliomwamini wafuatane naye.

Yoana alikuwa tayari kudhihakiwa na jamii kwa sababu ya kushirikiana na Yesu na mitume wake. Wote ambao walimfuata Yesu walipaswa kuwa tayari kufanya mabadiliko maishani mwao. Yesu alisema hivi kuhusu wafuasi hao: “Mama yangu na ndugu zangu ni hawa wanaosikia neno la Mungu na kulitenda.” (Luka 8:19-21; 18:28-30) Inatia moyo sana kujua kwamba Yesu yuko karibu na wale wanaojidhabihu ili kumfuata!

ALIMHUDUMIA KWA MALI ZAKE

Yoana na wanawake wengine walimhudumia Yesu na mitume wake “kwa mali zao.” (Luka 8:3) Mwandishi mmoja anaeleza hivi: “Luka hawaelezi wasomaji wake kwamba wanawake hao walipika vyakula, waliosha vyombo na kushona nguo.” Anaongeza hivi, “Labda walifanya hivyo . . . , lakini Luka hazungumzii mambo hayo.” Inaonekana wanawake hao walitumia pesa, vitu, au mali zao kuwahudumia.

Yesu na mitume wake hawakufanya kazi za kimwili katika maeneo waliyohubiri. Hivyo, huenda ingekuwa vigumu kwao kupata pesa za kununua chakula na mahitaji mengine kwa ajili ya watu 20 hivi. Inaelekea walikaribishwa na watu, lakini si mara zote Yesu na mitume wake walitegemea ukarimu huo, kwa sababu walikuwa na “sanduku la pesa.” (Yoh. 12:6; 13:28, 29) Inawezekana Yoana na wanawake wengine walichangia ili kulipia gharama hizo.

 Watu fulani wanadai kuwa wanawake wa Kiyahudi hawakuweza kumiliki mali. Hata hivyo, nakala za maandishi ya wakati huo zinaonyesha kwamba mwanamke angeweza kumiliki mali kwa njia mbalimbali: (1) kwa kurithi mali kutoka kwa baba yake aliyekufa bila kuwa na watoto wa kiume, (2) kwa kupewa mali hizo, (3) kwa kugawana pesa na mume wake baada ya kutalikiana, (4) kutokana na mapato ya mashamba ya mume wake aliyekufa, au (5) mapato ya kibinafsi.

Bila shaka, wafuasi wa Yesu walichangia kile walichoweza. Huenda baadhi ya wafuasi wake walikuwa wanawake matajiri. Kwa kuwa Yoana alikuwa mke wa msimamizi wa Herode, watu fulani wanasema kwamba alikuwa tajiri. Inawezekana lile vazi la bei ghali lisilo na mshono alilovaa Yesu, alipewa na mmoja kati ya wanawake hao matajiri. Mwandishi mmoja anasema kwamba hilo lilikuwa vazi ambalo “asingeweza kupewa na wake za wavuvi.”—Yoh. 19:23, 24.

Maandiko hayaelezi waziwazi kwamba Yoana alitoa mchango wa pesa. Hata hivyo, alifanya kile alichoweza nasi tunaweza kujifunza kutokana na mfano wake. Ni hiari yetu kuamua ikiwa tutachangia masilahi ya Ufalme au la. Jambo muhimu ni kwamba Mungu anapenda tutoe kwa shangwe kile tunachoweza.—Mt. 6:33; Marko 14:8; 2 Kor. 9:7.

KABLA NA BAADA YA KIFO CHA YESU

Inawezekana Yoana na wanawake wengine “waliokuwa na kawaida ya kufuatana naye na kumhudumia alipokuwa Galilaya, na wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja na kupanda pamoja naye mpaka Yerusalemu” walishuhudia kuuawa kwa Yesu. (Marko 15:41) Wakati mwili wa Yesu ulipoondolewa kutoka kwenye mti wa mateso kwa ajili ya maziko, wanawake hao “waliokuwa wamekuja pamoja naye kutoka Galilaya, wakafuata, wakalitazama kaburi na jinsi mwili wake ulivyolazwa; nao wakarudi kutayarisha manukato na mafuta yaliyotiwa marashi.” Luka anasema wanawake hao walikuwa “Magdalene Maria na Yoana na Maria mama ya Yakobo,” ambao walirudi baada ya sabato na kumwona malaika aliyewaeleza kuhusu ufufuo wa Yesu.—Luka 23:55–24:10.

Yoana na wanawake wengine walifanya kile walichoweza kwa ajili ya Bwana wao

Inawezekana kwamba Yoana alikuwa miongoni mwa wanafunzi ambao walikusanyika pamoja huko Yerusalemu siku ya Pentekoste mwaka wa 33 W.K. (Mdo. 1:12-14) Kwa kuwa mume wa Yoana alifanya kazi kwa Herode Antipasi, huenda Yoana ndiye aliyemsimulia Luka habari za mtawala huyo, hasa kwa sababu ni Luka peke yake kati ya waandishi wa vitabu vya Injili anayemtaja Yoana kwa jina.—Luka 8:3; 9:7-9; 23:8-12; 24:10.

Tunaweza kujifunza mambo muhimu kutoka kwa Yoana. Alimhudumia Yesu kulingana na uwezo wake. Ikiwa mali zake zilitumiwa kumsaidia Yesu, mitume wake, na wanafunzi wengine waliosafiri na kuhubiri pamoja na Yesu, basi bila shaka hilo lilimletea furaha. Yoana alimhudumia Yesu na alishikamana naye wakati wa majaribu. Litakuwa jambo bora kwa wanawake Wakristo kuiga mtazamo huo mzuri.