Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Mnara wa Mlinzi—Toleo la Funzo  |  Desemba 2014

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Yeremia alimaanisha nini aliposema kwamba Raheli anawalilia wanawe?

Tunasoma hivi kwenye Yeremia 31:15: “Yehova amesema hivi, ‘Katika Rama sauti inasikiwa, maombolezo na kilio cha uchungu; Raheli akiwalilia wanawe. Amekataa kufarijiwa juu ya wanawe, kwa sababu hawako tena.’”

Raheli alikufa kabla ya wanawe wawili. Kwa hiyo, yale ambayo Yeremia aliandika miaka 1,000 baada ya Raheli kufa huenda yakaonekana kuwa si sahihi.

Yosefu alikuwa mwana wa kwanza wa Raheli. (Mwa. 30:22-24) Baadaye, Raheli alipata mwana mwingine ambaye aliitwa Benyamini. Lakini Raheli alikufa alipokuwa akimzaa mwana huyo wa pili. Kwa hiyo, swali ni: Kwa nini andiko la Yeremia 31:15 linasema kwamba alikuwa akilia kwa sababu wanawe “hawako tena”?

Ni muhimu kukumbuka kwamba baada ya muda, mwanawe wa kwanza, Yosefu, alimzaa Manase na Efraimu. (Mwa. 41:50-52; 48:13-20) Baadaye, Efraimu likawa ndilo kabila kubwa na lenye nguvu zaidi kati ya makabila yote ya ufalme wa kaskazini wa Israeli, nalo liliwakilisha makabila yote kumi. Kwa upande mwingine, kabila lililotokana na mwana wa pili wa Raheli, Benyamini, pamoja na kabila la Yuda, yalifanyiza ufalme wa kusini. Basi, kwa njia ya mfano, inaweza kusemwa kwamba Raheli alifananisha mama wote wa Israeli, yaani, mama waliokuwa katika ufalme wa kaskazini na ufalme wa kusini.

Kufikia wakati ambapo kitabu cha Yeremia kilikuwa kinaandikwa, tayari makabila kumi ya ufalme wa kaskazini yalikuwa yameshindwa na Ashuru na watu wake wengi walikuwa wamechukuliwa mateka. Hata hivyo, huenda baadhi ya wazao wa Efraimu walikimbilia eneo la Yuda. Katika mwaka wa 607 K.W.K., Wababiloni walishinda ufalme wa kusini wa Yuda wa makabila mawili. Inaonekana kwamba wakati wa ushindi huo, mateka wengi walipelekwa Rama, mji uliokuwa kilomita nane hivi kaskazini ya Yerusalemu. (Yer. 40:1) Huenda baadhi yao walichinjwa huko katika eneo la Benyamini ambako Raheli alizikwa. (1 Sam. 10:2) Kwa hiyo, Raheli anawalilia wanawe katika maana ya kwamba anawaombolezea Wabenyamini kwa ujumla au wale hasa waliokuwa Rama. Huenda pia andiko hilo likarejelea mama wote wa watu wa Mungu waliokuwa wakiomboleza vifo vya Waisraeli au kupelekwa kwao uhamishoni.

Vyovyote vile, maneno ya Yeremia kuhusu Raheli akiwalilia wanawe yalikuwa unabii ambao ulitimizwa karne nyingi baadaye wakati uhai wa Yesu akiwa mtoto mchanga ulikuwa hatarini. Mfalme Herode aliamuru kwamba watoto wote wa kiume waliokuwa chini ya umri wa miaka miwili huko Bethlehemu, jiji lililokuwa kusini mwa Yerusalemu, wauawe. Hivyo, wana hao hawakuwapo tena, walikuwa wafu. Hebu wazia kilio cha huzuni cha mama hao waliofiwa na wana wao! Ni kana kwamba kilio hicho kilisikika hata eneo la mbali sana la Rama lililokuwa upande wa kaskazini wa Yerusalemu.—Mt. 2:16-18.

Kwa hiyo, katika siku za Yeremia na katika siku za Yesu, maneno “Raheli anawalilia wanawe” yalionyesha huzuni ya mama Wayahudi ambao wana wao waliuawa. Bila shaka, wale waliokufa na kwenda katika “nchi ya adui,” kifo, wataweza kutoka mikononi mwa adui huyo wafu watakapofufuliwa.—Yer. 31:16; 1 Kor. 15:26.