Kurarua mavazi kulimaanisha nini katika nyakati za Biblia?

MAANDIKO yanataja hali mbalimbali zilizofanya watu wararue mavazi yao. Huenda si jambo la kawaida leo, lakini kwa Wayahudi lilionyesha hisia kali zilizosababishwa na kukata tamaa, huzuni, aibu, hasira, au kuomboleza.

Kwa mfano, Rubeni ‘aliyararua mavazi yake’ alipogundua kwamba hangeweza kumwokoa ndugu yake Yosefu aliyeuzwa utumwani. Baba yao, Yakobo, ‘alirarua nguo zake’ alipofikiri kwamba Yosefu alikuwa ameraruliwa na mnyama-mwitu. (Mwa. 37:18-35) Ayubu ‘alirarua koti lake’ alipoambiwa kwamba watoto wake wote wameuawa. (Ayu. 1:18-20) Mjumbe alikuja mbele ya Kuhani Mkuu Eli “huku mavazi yake yakiwa yameraruliwa” ili kumwambia kwamba Waisraeli wameshindwa vitani, wana wawili wa Eli wameuawa, na sanduku la agano limetekwa. (1 Sam. 4:12-17) Yosia aliposikia maneno ya Sheria yakisomwa na kutambua makosa ya watu wake, “akayararua mavazi yake.”2 Fal. 22:8-13.

Yesu aliposhtakiwa, Kuhani Mkuu Kayafa ‘aliyararua mavazi yake ya nje’ aliposikia jambo ambalo alidhani kimakosa kuwa ni kufuru. (Mt. 26:59-66) Mapokeo ya kirabi yaliagiza kwamba yeyote aliyemsikia mtu akikufuru jina la Mungu alipaswa kurarua mavazi yake. Hata hivyo, maoni mengine ya kirabi yaliyoandikwa baada ya uharibifu wa hekalu la Yerusalemu yalisema kwamba “siku hizi si lazima mtu ararue mavazi yake akisikia kufuru dhidi ya Jina la Mungu, kwa kuwa mavazi yake yatabaki matambara.”

Kwa kweli, ikiwa mtu aliyerarua mavazi yake hakuhuzunika kutoka moyoni, basi tendo hilo halikuwa na thamani yoyote machoni pa Mungu. Hivyo, Yehova aliwaambia watu wake ‘wararue mioyo yao, wala si mavazi yao; na wamrudie.’Yoe. 2:13.