Je, kanuni zinazopatikana katika Sheria ya Musa zilitumiwa kutatua migogoro ya kila siku katika taifa la kale la Israeli?

NDIYO, kuna nyakati ambapo zilitumiwa. Tuchunguze mfano mmoja. Andiko la Kumbukumbu la Torati 24:14, 15 linasema hivi: “Usimlaghai kibarua mwenye uhitaji na maskini, awe ni mmoja wa ndugu zako au ni mkaaji mgeni katika nchi yenu . . . [Ukifanya] hivyo, atamlilia Yehova, nawe utakuwa na hatia ya dhambi.”

Kigae kilichoandikwa ombi la mfanyakazi wa shambani

Kuna maandishi kuhusu ombi fulani lililofanywa katika karne ya saba K.W.K. Yalipatikana karibu na eneo la Ashdodi. Inaelekea yaliandikwa kwa ajili ya mfanyakazi fulani wa shambani ambaye inadaiwa alishindwa kumpelekea mwajiri wake kiasi cha nafaka walichokuwa wamekubaliana. Maandishi hayo yaliyoandikwa kwenye kigae yanasema hivi: “Baada ya mimi mtumishi wako [mlalamikaji] kumaliza kuvuna nafaka na kuihifadhi ghalani siku chache zilizopita, Hoshayahu mwana wa Shobay alikuja na kuchukua vazi langu, mimi mtumishi wako. . . . Wafanyakazi wenzangu wote tuliokuwa tukivuna nao kwenye jua kali wanaweza kutoa ushahidi . . . kwamba maneno ninayosema ni ya kweli. Sina hatia ya kosa lolote. . . . Ee gavana, ikiwa utaona kwamba si wajibu wako kunirudishia vazi langu mimi mtumishi wako, tafadhali fanya hivyo kwa sababu ya huruma! Usikae kimya huku mimi mtumishi wako sijarudishiwa vazi langu.”

Ombi hili “linatufunulia mengi zaidi ya hisia za mfanyakazi aliyetaka sana kurudishiwa [vazi lake],” anasema mwanahistoria Simon Schama. “Linaonyesha pia kwamba mlalamikaji alijua jambo fulani kuhusu utaratibu wa kisheria ulioandikwa katika Biblia, hususan sheria zinazopatikana katika Mambo ya Walawi na Kumbukumbu la Torati kuhusu kuwadhulumu maskini.”