KIKUNDI kidogo cha abiria waliokuwa ndani ya mashua iliyokuwa ikisafiri kwenye ghuba ya Belfast Lough, waliona mandhari nzuri ya milima iliyofunikwa kwa kijani kibichi na iliyoangazwa na miale ya jua la asubuhi. Ilikuwa Mei 1910. Miongoni mwa abiria hao, kulikuwa na mwanamume aliyeitwa Charles T. Russell, ambaye alikuwa akitembelea Ireland kwa mara ya tano. Ndugu Russell angeweza kujionea meli mbili kubwa zilizokuwa zikitengenezwa—meli ya Titanic ambayo baadaye ilikumbwa na msiba mkubwa na nyingine iliyoitwa Olympic. * Karibu na eneo hilo ambalo meli zilikuwa zikitengenezwa, kulikuwa na Wanafunzi 12 wa Biblia ambao walikuwa wamesimama kwenye gati wakisubiri awasili.

Miaka 20 hivi mapema, Ndugu Russell alikuwa ameamua kufanya ziara kadhaa nje ya Marekani akiwa na lengo la kutafuta njia bora zaidi ya kueneza habari njema ulimwenguni pote. Alianza ziara yake ya kwanza kwa kutembelea nchi ya Ireland, Julai 1891. Akiwa kwenye meli iliyoitwa City of Chicago, angeweza kuona machweo ya jua kwenye pwani ya mji wa Queenstown na huenda alikumbuka jinsi wazazi wake walivyokuwa wakimsimulia kuhusu nchi waliyotoka. Ndugu Russell na waandamani wake walipokuwa wakipita kwenye miji iliyokuwa imesafishwa vizuri na eneo la mashambani lenye kupendeza, waligundua kwamba nchi hiyo ilikuwa shamba ‘lililokuwa tayari kuvunwa.’

Ndugu Russell alitembelea Ireland mara saba. Inaonekana kwamba upendezi aliokuwa ameanzisha kwenye ziara yake ya kwanza ndio uliowafanya mamia ya watu na nyakati nyingine maelfu ya watu, waje kumsikiliza alipotembelea nchi hiyo katika ziara zilizofuata. Kufikia wakati alipofanya ziara yake ya pili Mei 1903, mikutano ya watu wote jijini Belfast na Dublin ilikuwa ikitangazwa magazetini. Russell alisimulia kwamba “watu walikuwa wakisikiliza kwa makini sana” alipokuwa akizungumzia kichwa “Ahadi Inayoambatana na Kiapo” ambapo alieleza kuhusu imani ya Abrahamu na baraka ambazo wanadamu watapata wakati ujao.

Kwa sababu ya upendezi ambao watu walionyesha nchini Ireland, Russell alitembelea nchi hiyo katika ziara yake ya tatu barani Ulaya. Asubuhi moja Aprili 1908, alipokuwa akishuka kwenye bandari ya Belfast, ndugu watano walikuwa hapo ili kumpokea. Jioni hiyo, hotuba yenye kichwa, “Kupinduliwa kwa Milki ya Shetani,” iliyokuwa imetangazwa mapema iliwavutia “wahudhuriaji 300 hivi” waje kusikiliza. Mpinzani mmoja miongoni mwa wahudhuriaji alinyamazishwa haraka kupitia ufafanuzi stadi wa Maandiko. Jijini Dublin kulikuwa na mpinzani matata zaidi—Bw. O’Connor , karani wa shirika la YMCA—ambaye alijaribu kugeuza umati wa watu zaidi ya 1,000 dhidi ya Wanafunzi wa Biblia. Ni nini kilichotukia?

Acheni turudi nyuma katika historia, tujaribu kuwazia mambo yaliyotokea wakati huo. Mwanamume anayependezwa na kweli za Biblia anaamua kuja kusikiliza hotuba ya watu wote iliyotangazwa kwenye gazeti, The Irish Times. Alikuwa karibu sana kukosa kiti katika ukumbi huo uliofurika watu. Mwanamume huyo anamsikiliza kwa makini sana msemaji mwenye mvi na ndevu nyingi, aliyevaa koti refu jeusi. Msemaji huyo anapoendelea kutoa hotuba yake, anatembeatembea huku na huku jukwaani, akitoa  ishara kwa uhuru, na kujenga hoja kwa ustadi akitumia andiko moja baada ya lingine na hivyo kufungua masikio ya uelewaji ya mwanamume huyo kuelekea kweli za Biblia. Hata bila kutumia kikuza sauti, sauti ya msemaji huyo inaenea kotekote katika ukumbi huo, naye anafaulu kunasa usikivu wa wasikilizaji kwa muda wa saa moja na nusu. Kisha, wakati wa kipindi cha maswali na majibu, O’Connor na rafiki zake wanamuuliza msemaji huyo maswali magumu lakini anafaulu kuyajibu kwa kutumia Biblia. Umati wa wahudhuriaji unapiga makofi kumshangilia msemaji. Baada ya mkutano huo, mwanamume huyo aliyependezwa anawaendea akina ndugu ili ajifunze mengi zaidi. Masimulizi ya watu waliokuwepo kwenye mikutano hiyo, yanaonyesha kwamba watu wengi walijifunza kweli kwa njia hiyo.

Katika ziara yake ya nne, Mei 1909, Ndugu Russell alisafiri pamoja na karani wake Ndugu Huntsinger ili watumie muda watakaokuwa safarini kuandika makala za Mnara wa Mlinzi. Waliondoka New York kwa meli ya Mauretania. Hotuba ya watu wote ambayo Ndugu Russell alitoa huko Belfast iliwavutia watu 450 waje kusikiliza, na 100 kati yao walilazimika kusimama kwa sababu hakukuwa na nafasi ya kutosha.

Ndugu C. T. Russell akiwa kwenye meli ya Lusitania

Ziara yake ya tano, iliyotajwa mwanzoni mwa makala hii haikutofautiana na ziara nyinginezo. Baada ya hotuba ya watu wote jijini Dublin, mwanatheolojia mmoja maarufu aliyekuwa ameletwa na O’Connor alijibiwa maswali yake kupitia Maandiko, jambo lililowafurahisha sana wahudhuriaji. Siku iliyofuata, ndugu hao walipanda mashua ya kusafirisha barua kwa kasi hadi Liverpool na kisha wakapanda meli maarufu iliyoitwa Lusitania kwenda New York. *

Tangazo la hotuba ya watu wote katika gazeti la The Irish Times, Mei 20, 1910

Pia, hotuba za watu wote ambazo Ndugu Russell alitoa katika ziara yake ya sita na saba nchini humo mwaka wa 1911, zilitangazwa magazetini. Katika majira ya kuchipua, Wanafunzi 20 wa Biblia jijini Belfast waliwakaribisha watu 2,000 waliokuja kusikiliza hotuba yenye kichwa “Maisha Baada ya Kifo.” Bw. O’Connor alikuja tena jijini Dublin pamoja na mwalimu mwingine wa dini aliyeuliza maswali, na kwa mara nyingine tena wasikilizaji walipiga makofi baada ya majibu ya Kimaandiko kutolewa. Ndugu Russell na wenzake walitembelea miji mingine pia katika kipindi cha vuli cha mwaka huo, na watu wengi walikuja kumsikiliza. O’Connor na wenzake 100 wenye vurugu walijaribu tena kuvuruga mkutano huo uliofanywa jijini Dublin, lakini kwa mara nyingine tena wasikilizaji walimshangilia msemaji.

Ingawa Ndugu Russell ndiye aliyetoa hotuba nyingi za watu wote wakati huo, alitambua kwamba “kazi hii haimtegemei mtu mmoja,” kwa kuwa “hii si kazi ya mwanadamu, bali ni ya Mungu.” Mikutano hiyo ambayo sasa inajulikana kuwa Mikutano ya Watu Wote, iliandaa fursa nzuri za kuwasilisha kweli za Kimaandiko. Hotuba hizo zilikuwa na matokeo gani? Hotuba za watu wote zilisaidia kueneza habari njema, na makutaniko mengi yakaanzishwa katika majiji mengi kotekote nchini Ireland.—Hifadhi yetu ya vitu vya kale nchini Uingereza.

^ fu. 3 Haikupita miaka miwili na meli ya Titanic ikazama.

^ fu. 9 Meli ya Lusitania ililipuliwa na kuzama karibu na pwani ya kusini mwa Ireland Mei 1915.