Kila mwaka kuanzia mwezi Julai, nyangumi jike aina ya southern right whale (Eubalaena australis) huwasili katika pwani ya kusini ya Santa Catarina, nchini Brazili. Nyangumi hao husafiri kwa maelfu ya kilomita kutoka maeneo ya mbali kusini mwa Antaktiki, ili wakazae na kulea watoto wao kwenye maji yenye kina kifupi. Kwa miezi kadhaa wenyeji na watalii walio kwenye ufuo wa bahari na juu ya majabali hufurahia kuwatazama nyangumi na watoto wao wakijipumzisha na kuchezacheza baharini! *

Viumbe Wakubwa wa Majini

Nyangumi jike hukua na kufikia urefu wa mita 16 hivi na uzito wa tani 80 hivi! Ana mwili mkubwa mweusi na madoa meupe tumboni. Ana kichwa kikubwa ambacho ni robo ya urefu wa mwili wake. Mdomo wake ni mrefu na umechongoka. Hana pezi mgongoni kama aina fulani za nyangumi. Anapoogelea, nyangumi huyo huupeleka mkia wake mpana juu na chini badala ya upande-upande kama wanavyofanya samaki wengine. Yeye hutumia mapezi yake kubadili upande anaoelekea, kama vile rubani anavyoelekeza ndege ya abiria.

Jambo la kushangaza ni kwamba licha ya ukubwa wao, nyangumi wana uwezo wa kustaajabisha wa kuruka na kufanya sarakasi. Unaweza kuwaona wakisimamisha mkia kwa muda mrefu, wakinyanyua mkia na kupiga maji kwa nguvu, na wakiruka juu kisha wanajitupa ndani na kurusha maji hivi kwamba yanaweza kuonekana kutoka mbali sana.

Sifa zao za Pekee

Ngozi ya kichwa cha nyangumi hawa ina madoa yenye wadudu wadogo wa kundi la krasteshia wanaojulikana kama chawa wa  nyangumi. Karina Groch ambaye ni mratibu wa mradi fulani nchini Brazili wa kuwachunguza nyangumi hao (Brazilian Right Whale Project) anaeleza hivi: “Kila nyangumi ana madoa ya pekee yanayotumiwa kuwatofautisha, kama vile alama za vidole vya wanadamu zinavyotofautiana. Wanapokaribia ufukweni tunapiga picha madoa yao na kuhifadhi picha hizo.”

Wanasayansi wanasema kwamba ni vigumu kutambua umri hususa wa nyangumi hawa kwa sababu aina hii ya nyangumi hawana meno. Wanakadiria kwamba nyangumi hawa huishi wastani wa miaka 65 hivi. *

Jinsi Wanavyokula

Nyangumi hao hula vijidudu vya majini vinavyoitwa krasteshia. Kwenye upande wa juu wa taya, wana kitu kama kichujio kilichofanyizwa kwa mifupa mingi midogo myembamba sana. Wanapoogelea, maji huingia kupitia midomo yao iliyofunguka na kuwanasa viumbe hao wadogo kwa kutumia kichujio hicho. Hivyo, nyangumi mmoja anaweza kula tani mbili hivi za vijidudu hao kwa siku.

Katika miezi ya Januari na Februari, nyangumi hao huenda kwenye Bahari ya Antaktiki ambako kuna chakula kingi na hivyo kutengeneza shahamu. Tabaka hilo la mafuta huwasaidia kutunza joto la mwili wanapokuwa kwenye maji yenye baridi na hulitumia kama chakula wanaposafiri.

Walipataje Jina Lao?

Kuanzia karne ya 18 na kuendelea, nyangumi hawa wanaoitwa southern right whales (jina linalomaanisha nyangumi sahihi wa kusini) waliwindwa sana katika Kizio cha Kusini. Walionwa kuwa ndio nyangumi wanaofaa kuwindwa. Kwa nini? Kwa sababu hawaogelei kwa kasi, walikamatwa kwa urahisi sana, hata na wavuvi waliotumia mikuki na mashua za mbao zilizo dhaifu. Mbali na hilo, tofauti na nyangumi wengine, nyangumi hawa huelea baada ya kuuawa kwa sababu wana shahamu nyingi sana. Jambo hilo liliwawezesha wavuvi kuwakokota kwa urahisi hadi ufukweni.

Kwa kuongezea, shahamu na kichujio cha mdomoni kilichofanyizwa kwa mifupa zilitumiwa sana wakati huo. Shahamu ilitumiwa kama mafuta ya kuwashia taa na pia kama kilainishi. Vichujio hivyo vilitumika kutengeneza nguo za aina fulani, fimbo za kuendeshea farasi, na miavuli. Vichujio vilivyopatikana katika nyangumi mmoja tu vingeweza kufidia gharama zote zilizotumika wakati wa uvuvi!

Mwanzoni mwa karne ya ishirini, nyangumi waliwindwa sana na hivyo idadi yao ikapungua hivi kwamba biashara hiyo ya nyangumi ikawa haina faida. Katika mwaka 1973 kituo cha mwisho cha uvuvi wa nyangumi kilifungwa nchini Brazili. Kufikia sasa aina fulani za nyangumi zimeanza kuongezeka ilhali nyingine zinakabili hatari ya kutoweka.

Aina hii ya nyangumi ni mfano mzuri sana wa viumbe wengi wa aina mbalimbali na walioumbwa kwa njia ya pekee. Ni uthibitisho wa hekima na nguvu za ajabu za yule aliyewaumba, Yehova Mungu.—Zaburi 148:7.

^ fu. 2 Maeneo mengine ambayo nyangumi hao huzaliana ni karibu na pwani za Afrika Kusini, Argentina, Australia, na Uruguai, kutia ndani na Visiwa vya Auckland.

^ fu. 8 Wanasayansi wamegundua aina tatu za nyangumi wanaopatikana katika kundi la right whale. Mbali tu na Eubalaena australis wanaopatikana katika Kizio cha Kusini, kuna aina nyingine mbili za nyangumi ambao hupatikana katika Kizio cha Kaskazini. Aina hizo ni Eubalaena glacialis na Eubalaena japonica.