Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Mjusi Mwenye Ngozi Yenye Miiba Inayofyonza Unyevu

Mjusi Mwenye Ngozi Yenye Miiba Inayofyonza Unyevu

MJUSI wa Australia mwenye ngozi yenye miiba (Moloch horridus) ana uwezo wa kufyonza unyevunyevu kutoka katika ukungu, hali ya hewa yenye unyevu, na mchanga uliolowa maji. Kisha, husafirisha maji hayo hadi mdomoni mwake ili kuyanywa. Jinsi gani? Huenda jibu linategemea uwezo unaostaajabisha wa ngozi ya mjusi huyo.

Mirija iliyo juu ya ngozi imeunganishwa kwa pamoja ili kupitisha maji mpaka kwenye mdomo wa mjusi huyo

Fikiria hili: Ngozi ya mjusi huyo imefunikwa na magamba. Baadhi ya wanasayansi wanasema kwamba huenda unyevunyevu au ukungu unaokusanywa kwenye magamba hupitishwa katika sehemu ngumu ya ngozi na kisha huingia katika mirija iliyo wazi inayopatikana katikati ya magamba. Mirija hiyo imeunganishwa kwa pamoja na imeelekezwa katika mdomo wa mjusi huyo.

Unapofikiria nguvu ya uvutano, mjusi huyo anawezaje kufyonza maji ambayo yanapanda miguuni, kisha mwilini mwake, na hatimaye mdomoni mwake? Mjusi huyo hufyonzaje unyevunyevu kutoka katika ardhi yenye maji kwa kusugua tumbo lake?

Watafiti wamegundua mbinu anayotumia mjusi huyo. Mirija iliyo juu ya ngozi ya mjusi imeunganishwa na mirija mingine iliyo chini ya ngozi. Muundo wa mirija hiyo huwezesha maji kupita sehemu nyembamba bila kuzuiwa na nguvu ya uvutano. Hivyo, ngozi ya mjusi huyo inafanya kazi kama sifongo.

Janine Benyus, rais wa Biomimicry Institute anasema kwamba kuiga uwezo huo wa kufyonza unyevu kunaweza kuwasaidia wahandisi kubuni mfumo wenye uwezo wa kuondoa unyevu katika hewa ili kupoza majengo vizuri zaidi na pia kutokeza maji ya kunywa.

Una maoni gani? Je, ngozi inayoweza kufyonza unyevu ya mjusi huyo mwenye miiba ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?