MAISHA yalikuwaje maelfu ya miaka iliyopita? Watu walifuata desturi zipi? Wachimbuzi wa vitu vya kale wanaweza kueleza kwa kiasi fulani. Ili kuelewa jinsi watu wa kale walivyoishi, ingefaa kuchunguza maandishi ya mwanaume aliyeandika kuhusu maisha ya kipindi alichoishi. Mwanaume huyo aliishi miaka 2,400 hivi iliyopita. Anaitwa Herodoto, mwanahistoria Mgiriki wa karne ya tano K.W.K. Kitabu chake kiliitwa The Histories.

Herodoto aliandika kuhusu chanzo cha vita vilivyopiganwa na Wagiriki na hasa chanzo cha uvamizi wa Waajemi katika mwaka wa 490 na 480 K.W.K., uliotokea alipokuwa bado mvulana. Herodoto aliandika mambo mengi kuhusu kila taifa lililoshambuliwa na Waajemi.

AANDIKA MENGI ZAIDI

Herodoto alikuwa msimuliaji stadi. Alipenda sana kuandika kwa usahihi masimulizi yake na kutia ndani mambo madogo-madogo ambayo alihisi yalihitajika ili kukamilisha masimulizi yake. Alifanikiwa sana ikizingatiwa kwamba hakutegemea kumbukumbu za Nchi zilizoandikwa ili kuhifadhi historia ya matukio kwa kuwa hazikutunzwa.

Wakati huo ni watu wachache tu waliotunza kumbukumbu, na wengi walifanya hivyo walipotaka kusifia matendo ya kishujaa kwa kuyaandika kwenye minara ya kumbukumbu. Hivyo, ili aweze kutunza kumbukumbu ya matukio, Herodoto alihitaji kutegemea mambo aliyojionea, hadithi, na maelezo ya watu walioshuhudia matukio mbalimbali. Herodoto alisafiri kila mahali ili kukusanya habari. Alilelewa katika mji wa Halicarnassus uliokuwa koloni la Ugiriki (ambao sasa unaitwa Bodrum, kusini mwa Uturuki) na alitembelea sana nchi ya Ugiriki.

Herodoto alisafiri kila mahali ili kukusanya habari

 Alitembelea upande wa kaskazini katika Bahari Nyeusi na Scythia, eneo la nchi ya Ukrainia ya sasa, na kusini huko Palestina na upande wa juu wa Misri. Kuhusu upande wa mashariki, inaonekana kwamba alifika Babiloni, na huenda alimalizia safari yake upande wa magharibi katika eneo lililokuwa koloni la Ugiriki, kusini mwa nchi ya Italia ya sasa. Popote alipotembelea, alitafuta na kukusanya habari kutoka katika vyanzo vinavyoaminika.

USAHIHI WA MASIMULIZI YA HERODOTO

Kipande cha hati za mafunjo cha kitabu The Histories

Habari alizokusanya Herodoto ni sahihi kadiri gani? Habari alizoandika kuhusu nchi alizotembelea na vitu alivyojionea zinaonwa kuwa sahihi. Ufafanuzi wake kuhusu desturi ambazo hazikujulikana Ugiriki—zilizofuatwa na Wasikithe wakati wa kuwazika wafalme au zile za Wamisri za kuhifadhi maiti—unapatana kwa kiasi fulani na mambo ambayo wachimbuzi wa vitu vya kale wamegundua. Inasemekana kwamba wingi wa habari alizokusanya kuhusu Misri “zinazidi habari zote za kale zilizoandikwa kuhusu nchi hiyo.”

Hata hivyo, pindi nyingine Herodoto alilazimika kutegemea habari zisizoaminika. Zaidi ya hilo, watu katika siku zake waliamini kwamba miungu ya kipagani ilihusika sana katika maisha ya wanadamu. Hivyo, si mambo yote aliyoandika yanakubaliwa na wanahistoria leo. Hata hivyo, Herodoto alijitahidi kutenganisha kati ya ukweli na hekaya. Alisema kwamba hakuamini kila kitu alichoambiwa. Alichunguza na kulinganisha habari alizokusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali kabla ya kufikia mkataa.

Huenda kitabu The Histories kina kazi zote za uandishi za Herodoto. Ni wazi kwamba alifanya kazi nzuri sana ikizingatiwa kwamba hakuwa na vyanzo vingi vya habari.