Mashirika mengi na watu binafsi wanaendelea na jitihada za kuboresha hali ya maisha barani Afrika. Pamoja na jitihada hizo, bara la Afrika bado linakabili matatizo mengi sana.

Uwindaji Haramu wa Vifaru

Jumla ya vifaru 1,004 waliuawa nchini Afrika Kusini katika mwaka wa 2013 tofauti na mwaka wa 2007 ambapo vifaru 13 tu waliuawa. Ingawa uwindaji huo ulifanya pembe za vifaru kupatikana kwa wingi, bado kuna uhitaji mkubwa wa pembe hizo hivi kwamba thamani ya kilo moja ya pembe inazidi thamani ya kilo moja ya dhahabu. Pembe moja inaweza kuuzwa kufikia dola nusu milioni za marekani.

JAMBO LA KUFIKIRIA: Je, serikali zitaweza kuondoa kabisa uasi-sheria?—Yeremia 10:23.

Utoaji Rushwa Usioripotiwa

Shirika la Transparency International linasema kwamba nchi za Afrika Mashariki zina takwimu za juu zaidi za vitendo vya utoaji rushwa duniani. Hata hivyo, asilimia 90 hivi ya watu wanaoombwa rushwa hawatoi taarifa. Msemaji wa shirika hilo nchini Kenya anasema hivi: “Inaelekea kwamba wananchi hawaamini ikiwa serikali zao zitachukua hatua yoyote baada ya kupokea taarifa za vitendo vya rushwa.”

BIBLIA INASEMA NINI? “Rushwa hupofusha watu wanaoona vizuri.”—Kutoka 23:8.

Waafrika Wanatumia Intaneti

Kulingana na Shirika la International Telecommunication Union, ilitazamiwa kwamba kufikia mwisho wa mwaka 2014 asilimia 20 hivi ya watu katika bara la Afrika wangekuwa wakitumia Intaneti. Idadi ya watu wanaotumia Intaneti kupitia vifaa vya mkononi barani Afrika inaongezeka mara mbili zaidi ya wastani ya watumiaji dunia nzima.