Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Januari 2015

“Najitahidi Kutofikiria Ugonjwa Wangu Kila Wakati”

“Najitahidi Kutofikiria Ugonjwa Wangu Kila Wakati”

“Nilihitaji msaada ili kuinuka kutoka kitandani na hata kujilaza. Nilipata maumivu makali nilipotembea. Nilikuwa na vidonda kooni na hivyo ilikuwa vigumu kumeza dawa. Pia niliugua vidonda ambavyo vilikuwa sugu na havikupona kwa urahisi. Nilitaabishwa na vidonda vya tumbo na kiungulia. Sikujua chanzo cha ugonjwa wangu. Nilikuwa na umri wa miaka kumi tu.”—Elisa.

Licha ya ugonjwa wake, Elisa hufurahia kuwafundisha wengine Biblia

SCLERODERMA—neno linalomaanisha ngozi ngumu—linafafanua ugonjwa ambao watu karibu milioni mbili na nusu duniani pote wanaugua. Aina ya ugonjwa huu inayowapata sana watoto inaitwa localized scleroderma, ambayo hufanya ngozi kukakamaa.

Hata hivyo, akiwa na umri wa miaka kumi, Elisa aligundulika kuwa na aina ya scleroderma inayoitwa systemic—ambayo huathiri ngozi na pia sehemu za ndani za mwili kama vile, figo, moyo, mapafu, na utumbo. Madaktari waliomtibu Elisa walidhani matibabu yangerefusha maisha yake kwa miaka mitano tu. Hata hivyo, sasa miaka 14 imepita na Elisa bado yuko hai. Hata ingawa hajapona kabisa, anadumisha mtazamo mzuri kuhusu maisha. Mwandishi wa Amkeni! alifanya mahojiano na Elisa kuhusu ugonjwa wake na jinsi ambavyo amefaulu kuvumilia.

 Ni lini ulipogundua kwamba ulikuwa na tatizo hili?

Nilipokuwa na umri wa miaka tisa, nilipata jeraha kwenye kiwiko cha mkono wangu, na nikapata maumivu makali sana. Kidonda kiliendelea kukua, na hakikupona upesi. Baada ya kupimwa damu niligundulika kuwa na ugonjwa wa systemic scleroderma. Kwa sababu afya yangu ilizidi kuzorota, tulihitaji kupata daktari mtaalamu wa kutibu maradhi haya.

Je, mlifanikiwa kumpata daktari?

Tulipata daktari wa magonjwa ya kuvimba kwa misuli na viungo vya mwili. Daktari huyo aliwaambia wazazi wangu kwamba matibabu ya kutumia kemikali yangesaidia kupunguza kuenea kwa ugonjwa wangu na kurefusha maisha yangu kwa miaka mitano zaidi, na labda hata kuudhibiti. Lakini kutumia aina hiyo ya matibabu kungedhoofisha kinga ya mwili wangu. Hata kuugua mafua kungekuwa hatari!

Bila shaka, maneno ya daktari hayakutimia!

Ndiyo—nashukuru, bado niko hai! Hata hivyo, nilipokuwa na umri wa miaka 12 nilianza kupata maumivu makali ya kifua ambayo yalidumu kwa dakika 30 hivi, na wakati mwingine mara mbili kila siku. Yalikuwa makali hivi kwamba nilipiga mayowe.

Maumivu hayo yalisababishwa na nini?

Madaktari waligundua kwamba kiwango changu cha hemoglobini kilikuwa kidogo sana, hivyo moyo wangu ulikuwa unafanya kazi kwa shida ili kupeleka damu kwenye ubongo. Nilipata matibabu na baada ya majuma machache tatizo hilo likapungua. Lakini katika kipindi hicho nilidhani kwamba lolote lingeweza kunipata, sikuwa na uhakika wa kuishi. Nilikata tamaa sana kwa kuwa nilihisi sikuwa na namna ya kudhibiti maisha yangu.

Miaka 14 imepita tangu ulipogunduliwa kuwa na ugonjwa huu. Sasa unaendeleaje?

Bado nahisi maumivu, na nina maradhi mbalimbali yanayotokana na ugonjwa wa scleroderma. Maradhi haya yanatia ndani; vidonda vya tumbo, matatizo ya mapafu, na kiungulia. Hata hivyo, najitahidi kutofikiria ugonjwa wangu kila wakati na kujihuzunikia. Nina mambo mengine ya kufanya.

Mambo yapi hayo?

Napenda kuchora, kushona nguo, na kutengeneza mapambo. Jambo lililo muhimu zaidi kwangu nikiwa Shahidi wa Yehova, ni kushiriki katika kazi ya kuwafundisha wengine Biblia. Hata wakati ambapo sina nguvu za kwenda kwenye nyumba za watu, nashirikiana na Mashahidi wengine wanapohubiri karibu na nyumbani. Hata nimeweza kuwafundisha wengine Biblia. Kuhubiri kumefanya niishi maisha yenye kusudi.

Kwa nini ufanye kazi ya kuwahubiria wengine ilhali wewe mwenyewe una matatizo yako?

Najua ujumbe ninaotangaza ni muhimu na una faida. Isitoshe, ninapojitahidi kuwasaidia wengine kwa njia hii, ninapata furaha zaidi. Hata afya yangu inaimarika! Wakati huo mimi husahau ugonjwa wangu.

Biblia imekusaidiaje kuwa na mtazamo mzuri?

Biblia inanikumbusha kwamba mateso yangu, na ya wengine pia, ni ya muda mfupi tu. Andiko la Ufunuo 21:4 linasema kwamba kwa muda wake alioweka, Mungu “atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena.” Kufikiria andiko hilo na mengine kumenisaidia kuamini ahadi za Mungu kuhusu wakati ujao—si tu kwa ajili ya wale wanaoteseka kutokana na magonjwa mbalimbali, badala yake kwa ajili ya kila mtu.