Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Januari 2015

 NCHI NA WATU

Kutembelea Kosta Rika

Kutembelea Kosta Rika

MIAKA 500 iliyopita, Wahispania walitembelea eneo hili kwa mara ya kwanza. Waliliita Kosta Rika (Pwani Yenye Utajiri), wakifikiri kwamba wangepata dhahabu nyingi. Hata hivyo, jitihada zao ziliambulia patupu. Leo, nchi hii inajulikana, si kwa madini yenye thamani, bali kama mojawapo ya nchi zenye mimea na viumbe wa aina nyingi zaidi duniani.

Watu wa Kosta Rika wanajulikana kama Ticos. Wanaitwa hivyo kwa sababu wana desturi ya kuongeza kiambishi “-ico” mwishoni mwa maneno ili kukazia udogo wa kitu au jambo. Kwa mfano, badala ya kusema “un momento” (subiri), wamezoea kusema “un momentico” (subiri kidogo). Katika mazungumzo yao kila siku utawasikia wakisema “¡pura vida!” (hakuna matata!) wanaposhukuru, wanapokubaliana, wanaposalimiana, au wanapoagana.

Kuna mimea na wanyama wengi wa ajabu kwenye misitu iliyoko nchini Kosta Rika, kama chura huyu (Agalychnis callidryas)

Mojawapo ya vyakula vinavyopendwa sana nchini Kosta Rika ni gallo pinto (jina linalomaanisha “jogoo mwenye madoadoa”). Kwanza wali na maharagwe hupikwa kando na kisha kuchanganywa na kutiwa vikolezo mbalimbali. Chakula hiki kinaweza kuliwa asubuhi, mchana, au usiku. Wenyeji wanapenda kinywaji  kiitwacho café chorreado, ambacho hutayarishwa kwa kuchuja kahawa kwenye kifaa maalumu kilicho na kitambaa.

Kuna makutaniko 450 hivi ya Mashahidi wa Yehova nchini Kosta Rika. Mikutano yao hufanywa katika lugha 10, kutia ndani Lugha ya Ishara (Alama) ya Kosta Rika na lugha ya Bibri na Cabecar—ambazo ni lugha za wenyeji wa nchi hiyo.

JE, WAJUA? Nchini Kosta Rika kuna mawe mengi ya mviringo yaliyochongwa. Jiwe kubwa zaidi lina kipenyo cha mita 2.4. Inakadiriwa kwamba baadhi ya mawe hayo yamekuwepo kwa zaidi ya miaka 1,400. Hakuna anayejua kwa nini yalichongwa!

Mawe ya mviringo